e). Vikariati ya Kilimanjaro:
Kazi ya uinjilishaji ya mapadre wa Roho Mtakatifu iliweza kuonekana toka Mlima Kilimanjaro hadi Tanga kwa upande wa mashariki na pia hadi
Mbulu na Dodoma kwa upande wa magharibi. Katika mwaka 1910 Shirika la Enezo la Imani la Vatikani liliunda Vikariati ya Kilimanjaro ambayo
eneo lake lilipanuka toka Kilimanjaro hadi kufika Arusha, Mbulu, na Dodoma kwa upadre wa magharibi na Same hadi pwani ya Tanga kwa upande
wa mashariki. Katika mwaka 1933 Baba Mtakatifu Pius XII alimteua mheshimiwa padre Joseph Byrne, C.S.Sp (padre wa Roho Mtakatifu) kuwa
askofu wa kwanza wa Vikariati ya Kilimanjaro.
Kwa kuwa Vikariati ya Kilimanjaro ilikuwa na eneo kubwa la utawala kama inavyoonekana hapo juu na pia kwa kuwa idadi ya Wakristu ilikuwa
inaongezeka siku hadi siku, baba askofu Joseph Byrne aliiomba Vatikani kutuma vikundi vingine vya mapadre kutoka katika mashirika ya
kimisionari kumsaidia. Ombi lake lilipokelewa vyema na katika mwaka 1948 kikundi cha mapadre wa ki-Rosmini kilitumwa kufanya kazi katika
Vikariati ya Kilimanjaro. Pia katika wakati huo huo, Vatikani ilituma vikundi vingine viwili vya wamisionari kufanya kazi katika Vikariate
hiyo. Vikundi hivyo vilikuwa ni vya mapadre wa ki-Palotini na wale wa-Pashenisti. Ujio wa vikundi hivi vitatu vya watumishi wa Injili katika
shamba hili la mizabibu katika Vikariate ya Kilimanjaro vilileta baraka kubwa. Kwa kuwa na watenda kazi hawa kulimwezesha mhashamu baba
askofu Joseph Byrne kuvigawanya kiutume. Baba askofu Byrne aliwatuma Warosmini kwenda katika nchi ya Tanga, Wapalotini kwenda nchi
ya Mbulu, na Wapashenisti kwenda nchi ya Dodoma. Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu walibakia katika maeneo ya Kilimanjaro, Arusha, na
Same.
f). Wamonaki wa Kitrapisti katika Tanga
Katika mwaka 1895 wamonaki wawili wa Kitrapisti kutoka katika Abasia ya Watrapisti kule Afrika ya Kusini waliwasili Tanga na mara walikwenda
Lushoto. Walipofika huko waliwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Sir Krestlin na kumuomba shamba ambalo wangeweza kuanzisha makao yako.
Sir Krestlin hakukubaliana na ombi lao. Inasemekana kwamba Sir Krestlin alikuwa ni mtoto wa mchungaji wa Kiluteri. Yeye kama Mlutereri
hakuwapenda Wakatoliki katika nchi ya Lushoto ambayo tayari ilikuwa ina vituo kadha wa kadha vya Waluteri. Hivi hakutaka kuwa na matatizo
na Waluteri wenzake. Wamonaki hawa hawakuridhika na maamuzi ya kiongozi huyu wa wilaya. Na hata hivyo hawakuweza kufanya kitu bali kufunga
safari na kujirudia Tanga.
Mwaka mmoja na nusu baada ya kukataliwa kwao, wamonaki hawa wa Kitrapisti walirudi tena kwenye uongozi wa wilaya ya Lushoto na ombi lilelile
la kuomba sehemu ya nchi ili kuweza kujenga kituo chao. Safari hii waliweza kukubaliwa kupata sehemu ya kujisimika. Uongozi wa wilaya
ulikwisha badilika. Wamonaki hawa walipewa hekari 400 katika maeneo ya Irente na pia hekari 160 za msitu katika maeneo ya Gare. Baada ya
kupata sehemu hizo mbili, walianza kujenga makao yao kule Gare. Hadi kufikia mwaka 1904 walikwisha kuwa na majengo matano kule Gare,
majengo ambayo bado yamesimama hadi leo hii katika misheni ya Gare. Hii inathibitisha ubora ya ufundi wao katika teknolojia ya ujenzi.
Watawa hawa wa Kitrapisti hawakujishughulisha na shughuli za kichungaji katika nchi za Gare na Irente. Lengo lao kubwa katika sehemu hizi
lilikuwa ni kusimika makao yao na kuishi maisha yao ya kitawa. Pamoja na lengo lao hili bado waliweza kuchachusha maisha ya Kikristu kwa
wenyeji waliowazunguka. Wenyeji kadha wa kadha waliupokea Ukristu. Baadhi ya wale walioupokea Ukristu pengine hawakuwa na mizizi ya ndani
ya Ukristu bali pengine walivutwa na mali za wamonaki hawa. Masimulizi yanasema kwamba kanisa la wamonaki lilijaa waumini wengi siku za
Jumapili zilizofuatia wao kuchinja ng’ombe au nguruwe. Pengine waumini hawa walitegemea kupata kitoweo toka kwenye ukarimu wa wamonaki.
Wakati sehemu kubwa ya Watrapisti ilikuwa Gare, sehemu yao ndogo ilikuwa katika eneo lao la Irente. Uwepo wa wamonaki hawa kule Gare na Irente
unatamkwa wazi kuwa ni mbegu ya Ukatoliki katika nchi ya Usambara na hawa katika nchi za Gare, Mhelo, na Irente.
Kutokana na mabadiliko ya kiutawala katika shirika lao, wamonaki hawa wa Kitrapisti waliondoka Gare na Irente/Mhelo katika mwaka 1906 kurudi
kwenye nyumba yao mama kule Afrika Kusini. Katika kipindi hiki kifupi ambacho wamonaki hawa walikuwepo katika misheni ya Gare, waliweza kufiwa
na wanachama wao kadhaa ambao makaburi yao bado yapo Gare hadi hivi sasa. Watawa wao waliofia na kuzikwa Gare ni: Pd. Leonard aliyekufa
Septemba 26, 1897, Emmanuel aliyekufa Desemba 18, 1900, na Fr. Leander aliyefariki Mei 14, 1900. Kuondoka kwa wamonaki wa Kitrapisti katika
nchi ya Usambara mwaka 1906 ilikuwa ndiyo mwisho wa historia yao katika nchi ya Tanga. Kama tulivyoona hapo juu, alama walizoziacha za Ukristu
na utamaduni bado ziliendelea kubaki katika maeneo hayo hata baada ya kuondoka kwao.
|