c). Vikwazo vya Uinjilishaji
i). Uisilamu, Uarabu, na Mila za Wenyeji: Kazi yao kubwa ilikuwa kuupanda Ukristu katika udongo ambao ulikuwa una mizizi mirefu ya Uisilamu,
mila na desturi za Mashariki ya Kati na pia mila za wenyeji. Katika sehemu nyingine za nchi ya Tanga, wamisionari hawa walikumbana na vikwazo vingi. Pamoja na
ugumu huu wa mazingira ya kichungaji, wamisionari hawa waliendelea na kazi ya kichungaji bila kikomo.
ii). Uduni wa miundombinu: Kikwazo kingine cha kazi ya uinjilishaji wa wamisionari hawa katika nchi ya Tanga katika kipindi hiki ilikuwa ni
ugumu wa mawasiliano. Miundo mbinu ya mawasiliano ilikuwa duni mno. Sehemu nyingi hazikuwa na barabara na hata sehemu zile zilizokuwa na barabara, barabara
hizo zilikuwa duni mno. Hali hii iliwafanya wamisionari kutembea kwa miguu au kutumia farasi au punda kuweza kuvifikia vigango au jumuia za Wakristu sehemu
za mashambani. Mara nyingine wamisionari walikwenda sehemu za mbali kupeleka Sakramenti kwa wagonjwa. Mara nyingine kwa sababu ya umbali toka parokiani hadi
kwa Mkristu mgonjwa, basi walifika kwenye nyumba ya mgonjwa na kukuta mgonjwa amekwishafariki na hata kuzikwa. Basi katika hali hiyo waliishia kubariki
kaburi.
iii). Lugha na mila ngeni za wenyeji: Changamoto jingine kwa wamisionari hawa lilikuwa ni lile la lugha. Katika kipindi hiki cha
uinjilishaji, watu katika Tanganyika walikuwa wakiishi katika jumuia za kikabila na sio za kitaifa. Kila kabila lilikuwa likiishi katika eneo lake la
kijiografia na lilikuwa likiishi mila zake na kuzungumza lugha yao. Lugha ya kabila moja ilikuwa tofauti kabisa na lugha ya kabila la jirani. Hivi
wamisionari wa mwanzo walipaswa kujifunza lugha na mila za makabila haya ili kuweza kufanya kazi bora ya kuinjilisha. Katika mkoa wa Tanga kulikuwa na
zaidi ya makabila nane. Makabila hayo ni: Wadigo wa mwambao wa Tanga, Wabondei wa nchi ya Muheza, Wasambaa walioishi katika milima ya Usambara, na Wazigua
walioishi maeneo ya Korogwe na Handeni. Pia katika sehemu za Usambara magharibi kulikuwa na makabila ya Kipare na Kimbugu. Ndani ya maeneo mengi ya mashamba
ya mkonge na chai kulikuwa na makabila mengi ya kutoka bara za kusini mwa nchi na magharibi ya nchi ambao pia walidumisha lugha na mila zao. Makundi haya
yalikuwa ni ya Warundi, Waha, Wanyarwanda, Wangoni, Wamakonde, Wahehe, Wabena na wengineo wengi. Wamisionari wa mwanzo walipaswa kujifunza mila na desturi
za makabila haya na pia kujifunza lugha zao. Kwa wamisionari waliofanya kazi katika nchi ya Tanga walisaidika kidogo kutokana na mpanuko wa lugha ya Kiswahili
katika maeneo haya. Hivi katika sehemu nyingi waliweza kutumia lugha ya Kiswahili kwa watu wa umri mdogo kwani polepole lugha hii ilikuwa inakua. Pamoja na
kujifunza mila na desturi hizi za makabila haya, wamisionari hawa iliwabidi kujifunza mila, desturi, na dini za Mashariki ya kati kwani athari ya mila na
dini hii ilikuwa kubwa kwa wazalendo wa mazingira haya ya mkoa wa Tanga.
iv). Uhaba wa Fedha na Uhaba wa Mapadre: Wamisionari hawa wa mwanzo walikumbana na tatizo la uhaba wa watenda kazi katika eneo kubwa
la kuinjilisha katika mkoa mzima wa Tanga. Kadhalika vyanzo vyao vya fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kichungaji jimboni ilikuwa ni michache mno.
Sadaka toka kwa wananchi zilikuwa ndogo mno. Kwa kiasi kikubwa wamisionari hawa walipaswa kutegemea ufadhili toka kwa ndugu zao wa ulaya ambao nao hawakuwa
na rasilimali nyingi. Uhaba wa fedha na uhaba wa watumishi wa Injili ulipunguza kasi ya kujenga miundo mbinu ya uchungaji haraka.
d). Mwisho wa kipindi cha Prefekture ya Tanga:
Wakati wamisionari wa Kirosmini walipofika Tanga mwaka 1948 walipokea parokia nne toka wa mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu. Parokia
hizo zilikuwa ni Tanga, Mlingano, Korogwe, na Gare. Hadi mwisho wa kipindi cha Prefekture ya Tanga kulikuwa na ongezeko la parokia kadhaa. Parokia
zilizoongezeka zilikuwa zile za Lushoto na Kwediboma
katika mwaka wa 1950, Parokia ya Mazinde-Ngua katika mwaka 1951, Potwe na Rangwi katika mwaka wa
1953. Ongezeko hili la parokia liliwezekana tu baada ya waasisi Warosmini
wa mwanzo walipoweza kupata ongezeko la wamisionari wengine toka Ulaya.
MATUKIO MUHIMU 1893-1958
Kipindi hiki kilishuhudiwa kuzaliwa Parokia mbalimbali, kuongezeka
kwa Wakristu na kukua kwa miito ya Kitawa na Upadre. Wamisionari
waliofika Tanga walijitahidi kuanzisha vituo vya uinjilishaji. Vituo
hivyo baadaye vikawa Parokia. Parokia hizo ndizo zilizotoa sura
ya kuweza kuanzishwa kwa Jimbo la Tanga.
1893 Kanisa la Mtakatifu Anton wa Padua Chumbageni-Tanga.
1897 Kanisa la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni na Mtakatifu Gerald -Gare
1902 Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Mbingu Mlingano
1937 Kanisa la Bikira Maria Mshindi-Kilole
1950 Kanisa la Ekaristi Takatifu Lushoto
1950 Kanisa la Familia Takatifu- Kwediboma
1951 Kanisa la Maria Mama wa Mateso-Mazinde Ngua
1953 Kanisa la Bwana Wetu Yesu Kristu Mfalme-Potwe
1953 Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Rangwi
1. SEHEMU YA KWANZA: KARNE YA
16 - 1947
MBEGU ZA MWANZO ZA UKATOLIKI TANGA,
3. SEHEMU YA TATU: 1959 -
1969
TANGA YAWA JIMBO: ASKOFU EUGENE ARTHURS, I.C.
4.
SEHEMU YA NNE: 1970 - HADI LEO
UONGIZI WA WENYEJI: MAASKOFU KOMBA, MKUDE, BANZI, KIANGIO
|