|
|||
|
|||
SEHEMU YA TATU: 1959 - 1969 TANGA YAWA JIMBO: ASKOFU EUGENE ARTHURS, I.C. Askofu wa Kwanza Jimbo la Tanga, Askofu
Eugene Arthurs. |
|||
b). Askofu Eugen Arthurs, I.C: 1958 - 1969 c). Vuguvugu Katika Jamii ii). Misigano ndani ya wageni: Vuguvugu la kisiasa katika Tanganyika halikuonekana tu kati ya tabaka la watawala wa kikoloni na watawaliwa (wenyeji) kama inavyoonekana hapo juu, lakini pia hata ndani ya wazungu watawala wenyewe. Mahusiano kati ya Wajerumani na Waingereza hayakuwa mazuri sana. Kusigana kwao kiitikadi kulikojionyesha hata kabla ya Vita Kuu ya Pili kulizidi kuonekana hata baada ya vita. Mahusiano haya yalijionyesha pia katika kazi za umisionari. Wamisionari wa Kijerumani walipaswa kuondoka kwenye vituo vyao vya kichungaji katikaTanganyika baada ya vita. Kwa mfano katika mwaka 1945 mheshimiwa padre Michael Cottrell aliyekuwa Mrosmini alinyimwa viza yake ya kufanya kazi Tanganyika kwa sababu tu alionekana na picha ya askari wa Kijerumani. Kwa hali hiyo alikataliwa kufanya kazi katika koloni la Waingereza. Pia katika mwaka 1950 mchungaji mmoja wa Kiluteri aliyeitwa Gleiss alilumbana na padre Stiegler Mkatoliki. Padre Stiegler (Mwingereza) alitaka kujenga shule mahali fulani ambapo wanakijiji hawakukubaliana napo. Ukweli wa hadithi hii ni kwamba siyo kwamba wanakijiji walikataa shule kujengwa katika eneo hilo bali mchungaji Gleiss (Mjerumani) hakutaka padre Stiegler (Mwingireza) kujenga shule hiyo katika eneo lile. Lumbano lile lilimazika tu wakati mchungaji Mjerumani alipoondoka katika eneo lile na kuelekea nchi ya Vuga. Huku nyuma basi padre Stiegler aliweza kutimiza azma ya kujenga shule ile pale kijijini. iii). Askofu Arthurs na Madai ya Uhuru: Askofu Arthurs alikuwa ni kiongozi mahiri kwa watu wake. Kwa kufahamu vyema vuguvugu la kisiasa katika kipindi chake cha uongozi, alipenda kuwa mchungaji mwema wa kondoo wake wote. Alifahamu wazi kwamba kundi lake la kondoo lilikuwa ni mchanganyiko mkubwa wa kimataifa na kikamakabila. Katika miaka ya 1959/60 katika Tanga, kulikuwa na mgomo mkubwa wa wafanyakazi wa reli. Mgomo huu ulichukua muda mrefu kumalizika. Mgomo huu uliongozwa na uongozi wa TANU, chama kilichokuwa kinaongoza kupigania uhuru wa wenyeji toka kwenye ukoloni. Askofu Arthurs alifahamu adhari kubwa hasi ya mgomo huu kwa wafanyakazi wa reli. Kwa ufahamu huu, baba askofu Arthurs alianza kampeni ya kijimbo kuanzisha mfuko wa fedha kuwasaidia wafanyakazi walioathirika na mgomo huu. Yeye binafsi alichangia paundi 500 katika mfuko huu na alimteua mheshimiwa padre Sean Madden, I.C. kusimamia mfuko huu. Hapo April 27, 1960 katikati ya vuguvugu kubwa la mapambano ya kudai uhuru, baba askofu Arthurs aliandika waraka wa kichungaji kwa mapadre na waumini wake kueleza msimamo wa jimbo katika maswala ya kisiasa. Aliwatahadharisha mapadre wake wasitumie makanisa na maeneo yake kama viwanja wa kisiasa. Aliandika, "Katika majengo ya kanisa na hata katika viwanja vyake kusiwe na matangazo wala mikutano ya kisiasa." Katika kipindi chote cha uaskofu wake, Askofu Arthurs alikuwa ni mtu rahimu na mpenda amani. Alikuwa na amani na uongozi wa serikali. Hapo Novemba 30, 1961 baba askofu alilialika Jimbo lote la Tanga kuuombea uhuru wa Tanganyika.
d). Uhuru wa Tanganyika na Mtaguso Mkuu wa Vatikani II Kwa maongozi ya Mungu Jimbo la Tanga lilikuwa linaandaliwa kukumbana na mabadiliko makubwa ambayo yalijitokeza ndani ya
Kanisa Katoliki ulimwenguni na pia ndani ya nchi ya Tanganyika. Nchi ya Tanganyika ilijipatia uhuru wake hapo Desemba 9, 1961. Kadhalika ndani ya kanisa Baba Mtaktifu Yohane wa XXII
alitangaza Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani hapo Oktoba 11, 1962, mtaguso uliochukua muda wa miaka mitatu. Ni Baba Mtakatifu Paulo VI aliyeufunga Mtaguso huo hapo Desemba 8, 1965.
Uhuru wa Tanganyika na Mtaguso wa Pili wa Vatikano vilileta vuguvugu kubwa katika maisha ya watu na pia katika maisha ya kanisa. Kanisa la Tanga la kabla ya uhuru na kabla ya Mtaguso halikuwa sawasawa tena baada ya matukio hayo makubwa kutokea. Kanisa lilipata changamoto la kuyaona mabadiliko na kuyapokea mabadiliko hayo katika maisha ya kanisa katika kipindi kipya. e). Mfumo wa Shule Katoliki za Jimbo f). Ongezeko la Wamisionari Katikati ya miaka 1957 na 1970 karibia mapadre wamisionari 28 kutoka Ireland, Italia, na Uingereza walifika kufanya utume katika Jimbo la Tanga. Walipaswa kukua katika kipindi hiki cha mpito katika historia ya nchi ya Tanganyika na katika historia ya Kanisa la Ulimwengu. Mabadiliko mengi yalijitokeza katika wakati huo yalimwalika kila mtu kushiriki katika jinsi ya kufikiri na kutenda. Kwa ujio wa wamisionari wapya mapadre jimboni Tanga kulimwezesha baba askofu Arthurs kufungua parokia mpya na hata kufungua ofisi mpya kijimbo. Ufunguzi wa parokia mpya
ulifuatia katika kuzigawanya parokia za awali ambazo zilikuwa kubwa mno. Kutoka katika eneo la Parokia ya Gare kuliundwa parokia ya Kwai katika mwaka 1965 na Parokia ya Kongoi katika
mwaka 1966. Kutoka eneo la Parokia ya Mlingano kuliundwa parokia ya Muheza katika mwaka 1969 na kutoka eneo la Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga
kuliundwa Parokia ya Maramba katika mwaka 1970.
g). Tanganyika/Tanzania Motomoto Polepole maofisi mengi ya kiserikali na ya mashirika binafsi yalianza kushikiliwa na wenyeji wa Kitanganyika baada ya wazungu wakoloni kuondoka. Katika mwaka 1964 kulikuwa na mapinduzi katika nchi ya Unguja. Mara baada ya mapinduzi hayo, Unguja ilifanya muungano na Tanganyika na kuunda taifa jipya la Tanzania. Katika mwaka 1966 lugha ya Kiswahili ilichanguliwa kuwa lugha ya taifa la Tanzania. Mwaliko ndani ya Kanisa la Ulimwengu kutumia lugha za wenyeji katika liturjia yaliendana sambamba na Kanisa la Tanzania kuipokea lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya madhehebu ya Ibada. Hivi wamisionari wapya waliofika Tanga waliweza kujifunza lugha ya Kiswahili kwa kujizamisha katika jamii na mashule kujifunza lugha. Katika mwaka 1967 taifa la Tanzania liliipokea Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kuwa siasa ya nchi. Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilitoa miongozo kuelezea wazi maana halisi ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa hii iliwaalika Watanzania kujiingiza ndani kabisa katika mfumo wa kuishi na kufanya kazi pamoja za kiuchumi. Katika sehemu nyingi za nchi, kuliazishwa vijiji vya ujamaa ambavyo vilipokea watu toka kwenye vijiji vya jadi. Kanisa Jimbo lilibidi kusoma alama zote hizi za nyakati na kuweza kuboresha shughuli za kichungaji kuendana na mabadiliko hayo. h). Askofu Arthurs na malezi ya miito Katika uongozi wake kama Askofu wa Tanga, Askofu Arthurs alikuwa na moyo wa kulea mito ya kipadre na kitawa ndani ya wenyeji. Alifahamu wazi kwamba siku moja Kanisa la Tanga litahitaji kuongozwa na wenyeji wa Tanga. i). Wamisionari wenyeji toka Jimbo la Peramiho: Askofu Arthurs alifahamu kwamba katika Tanga kulikuwa na Wakatoliki wengi waliotoka mikoa ya bara kuja kufanya kazi katika mashamba ya mikonge na chai. Kwa ufahamu huu alipeleka ombi kutoka katika Jimbo la Peramiho kuomba mapadre wazalendo wa jimbo hilo kuja kufanya kazi ndani ya Jimbo la Tanga haswa katika sehemu zile ambazo zilikuwa na watu wengi toka mkoa wa Ruvuma. Mapadre Eligius Kapinga, Bernard Ndunguru na John Haule walifika Jimboni Tanga toka Jimbo la Peramiho kama wamisionari.
ii). Miito ya masista wenyeji: Muda huohuo baba askofu alihamasisha miito toka ndani ya vijana wa jimbo. Alikuwa mstari wa mbele katika uboreshaji wa
miito ya masista na hata aliteua mapadre wake kuwa mapadre walezi kule katika konventi ya masista wa jimbo Rangwi. Kadhalika bab askofu aliwapokea masista kuwa sehemu
kubwa ya kazi ya unjilishaji katika maparokia.
iii). Miito ya mapadre wenyeji: Baba askofu Arthurs aliwapeleka vijana wenyeji seminari ndogo na seminari kubwa kuwaandaa kuwa mapadre wa jimbo. Kabla ya kustaafu kwake kama askofu wa Tanga aliweza kupadirisha mapadre watatu wazalendo. Mapadre hawa ni: Odilo Mtoi (1960), Vincent Ushaki (1968) na Gerald Chilambo (1969). Nje ya mapadre hawa watatu aliowapadirisha, pia mapadre kadhaa ambao walifuatia kupadirishwa katika miaka ya 1970 hadi 1976 walipitia katika mikono yake ya malezi. Baadhi ya mapadre hawa ni: Vitus Nkondola (1970), Ignas Safari (1972) and Martin Maganga (1972). iv). Utume wa makatekista wa Jimbo: Kwa kufahamu umuhimu wa uinjilishaji katika mazingira ya Tanga, baba askofu Arthurs aliona umuhimu mkubwa wa utume wa makatekista na pia ubora wa elimu yao. Kwa mwendo huu alianzisha chuo cha makatekista kule katika Parokia ya Kwai ambacho kingesomesha makatekista na familia zao katika elimu ya dini. Chuo cha makatekista cha Kwai kilijengwa kwatika miaka ya mwanzoni wa 1960. Kutokana na udhaifu wa majengo ya chuo hiki, chuo hiki kilipaswa kufungwa mda mchache baadaye. Japo chuo hiki hakikudumu kwa muda mrefu, kiliweza kusomesha makatekesta wachache ambao utume wao katika Jimbo umekuwa na matokeo makubwa ya imani. Baadhi ya makatekesta waliosoma chuo cha Kwai ni Sebastian Maghambo alifanya utume wake katika Parokia ya Lushoto. Titus Shekibuah alifanya utume wake Parokia ya Sakhrani (kigango cha Kwehangala). Edward Joseph Shemdoe aliyefanya utume wake kule Parokia ya Mlingano, baadaye Parokia ya Sakharani kigango cha Kwekitui na baadaye Parokiani Gare. Paul Chipaini aliyefanya utume wake Parokia ya Kilole. I). Siku za mwisho mwisho za Uongozi wa Askofu Arthurs i). Mshituko wa Moyo: Siku zilivyozidi kusonga mbele afya ya baba askofu Arthurs ilianza kudidimia kutokana na ugonjwa wa moyo. Katika mwisho wa mwaka 1967 alipata shikikizo la moyo. Alikwenda kupata huduma ya tiba katika hospitali kule Mombasa, Kenya. Mwezi Novemba 1967, mkuu wa Warosmini duniani Don Giovanni Gaddo alimtembelea baba askofu hospitalini Mombosa. Baada ya kutoka huko alirudi Tanga na Novemba 29, 1967 kulikuwa na kikao cha askofu katika Parokia ya Kilole. Hapo Don Gaddo aliwashirikisha mapadre wote kwenye kikao kwamba baba askofu Arthurs alikuwa na nia ya kujiuzulu utume wa kiaskofu kutokana na uduni wa afya yake. ii). Lipi linafuatia sasa: Mei 31, 1968 Mwadhama Kardinali Agagian alimwandikia waraka Padre Kiongozi wa Warosmini Don Gaddo kumuomba maoni yake juu ya kupata askofu msaidizi katika Jimbo la Tanga. Katika mwezi Aprili 1968 mwakilishi wa Baba Mtakatifu Tanzania alikutana na askofu Arthurs na pia washauri wa askofu pale Parokiani Kilole katika harakati zake za kutathimini hali halisi ya Jimbo la Tanga. iii). Sherehe za Miaka 100 ya Ukatoliki Tanzania: Katika mwezi wa Julai 1968 wakati wa sherehe za Miaka 100 ya kazi ya uinjilishaji katika Tanzania, sherehe zilizofanyika kitafaifa kule Dar Es Salaam kwa mshindo mkubwa, Balozi wa Vatikani alitangaza rasmi kwamba umekuwa ni uamuzi wa Kanisa kwamba tokea mwaka ule maaskofu wote wapya watachaguliwa kutoka katika mapadre wazalendo na siyo kutoka kwa wamisionari tena. Hii ilikukuwa ni kuweza kuoanisha siasa ya kanisa na siasa ya nchi ambapo viongozi wengi wa serikali na mashirika ya uma walichaguliwa kutoka kwa wananchi wazawa. iv). Kujiuzulu kwa Askofu Arthurs: Katika mwezi August 1968 baba Askofu Arthurs alipeleka ombi lake Vatikani la kujiuzulu kiti cha uaskofu. Desemba 15, 1969 ombi la baba askofu Arthurs kujiuzulu uaskofu lilikubaliwa na Vatikani. Tamko hili lilileta mshituko kwa mapadre na waumini wa Jimbo la Tanga kwani kiongozi huyu alipendwa na wengi. Pamoja na mshituko huo, tamko hili lilileta nafuu kwa askofu Arthurs ambaye sasa alikuwa mdhaifu zaidi. Basi Askofu Eugene Aurhurs aliliongoza Jimbo la Tanga kwa kipindi cha miaka 19 (miaka tisa kama Prefekti na miaka 10 kama Askofu). Baada ya kujiuzulu kwake uaskofu, askofu Aurthurs alirudi Ireland ambako aliishi huko na kufariki dunia Februari 23, 1978 akiwa na umri wa miaka 64. ONGEZEKO LA PAROKIA CHINI YA UONGOZI WA MHASHAMU BABA ASKOFU EUGEN ARTHURS 1958 - 1970 Kipindi hiki kilishuhudiwa na kuzaliwa kwa Parokia mpya tano: 1959 Kanisa la Mtakatifu Teresa-Barabara ya 20-Tanga 1965 Kanisa la Mtakatifu Fransisko Ksaveri-Kwai 1966 Kanisa la Mtakatifu Patris-Kongoi 1969 Kanisa la Yesu Mfufuka Muheza 1970 Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili-Maramba
1. SEHEMU YA KWANZA:
KARNE YA 16 - 1947 2.
SEHEMU YA PILI: 1948 - 1958 4.SEHEMU YA NNE: 1970 - HADI LEO UONGIZI WA WENYEJI: MAASKOFU KOMBA, MKUDE, BANZI, KIANGIO
|