KANISA KATOLIKI TANGA

Historia

 

SEHEMU YA NNE: 1970 - HADI LEO

UONGIZI WA WENYEJI: MAASKOFU KOMBA, MKUDE, NA BANZI

A. MHASHAMU ASKOFU MAURUS GERVAS KOMBA (1970 - 1988)

Kipindi hiki kinaanza na uongozi wa Askofu Mzalende, Askofu Maurus Komba, akifuatiwa na Askofu Telesphory Mkude mwaka 1988, Askofu Anthony Banzi mwaka 1994 na kisha Askofu Thomas Kiangio mwaka 2023

a). Uteuzi wa Askofu Maurus

Huyu ni askofu wa kwanza Mwafrika katika Jimbo la Tanga. Alitangazwa kuteuliwa kuwa askofu wa Tanga Desemba 15, 1969 wakati ambapo tangazo la kujiuzulu kwa Askofu Arthurs lilipotangazwa.

b). Kutawazwa kwa Askofu Maurus

Askofu Mteule Maurus Komba alitawazwa kuwa askofu wa Tanga March 15, 1970. Askofu kiongozi aliyemtawaza na kumsimika alikuwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, aliyekuwa askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Maaskofu watawaza wasaidizi walikuwa askofu mstaafu wa Jimbo la Tanga Eugene Aurthurs I.C. na askofu mstaafu wa Jimbo la Peramiho (baadaye Songea) kule mkoani Ruvuma Mhashamu Askofu na Abate Eberhard (Hermann) Spiess, O.S.B.

c). Ni Nani Huyu?

Tangazo la kutangazwa kwa mheshimiwa padre Maurus kuwa askofu wa Jimbo la Tanga liliwashitua watu wengi katika Tanga. Watu wengi wa Tanga wenyeji na wamisionari hawakumfahamu padre huyu. Wale wachache waliomfahamu walikuwa ni wenyeji wa mkoa wa Ruvuma waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba ya mkonge na chai yaliyokuwa mkoani Tanga.

Wakati padre Maurus Gervas Komba alipotangazwa kuwa askofu wa Tanga, alikuwa ni Naibu wa Askofu wa Jimbo la Songea liliongozwa na Mhashamu Askofu Yakobo Yafunani Komba. Nafasi hiyo ya unaibu alihama nayo toka Jimbo la Peramiho baada ya kufanya kazi kwa muda kadhaa chini ya askofu na abate mstaafu Eberhard (Hermann) Spiess, O.S.B.

d). Historia Fupi ya Askofu Maurus

Mheshimiwa padre Maurus Komba alikuwa mzaliwa wa Parokia ya Litembo katika Wilaya ya Mbinga. Kwa asili yeye ni wa kabila la Kimatengo, kabila linaloishi sehemu za milimani katika Wilaya ya Mbinga mkoni Ruvuma. Alifanya elimu ya msingi katika shule ya Litembo na baadaye alikwenda kufanya masomo ya sekondari kule Kigonsera kabla ya kujiunga na masomo ya falsafa na tauhidi katika Seminari Kuu ya Peramiho. Baada ya kukamilisha masomo yake hayo alipadirishwa Julai 15, 1954 na kuwa padre wa Jimbo la Peramiho. Katika miaka yake ya awali kama padre alifanya shughuli za kichungaji katika nafasi ya padre msaidizi na baadaye kama paroko katika parokia za Mbinga, Mbangamao na Mkumbi zote zikiwa katika Wilaya ya Mbinga. Baadaye aliteulikwa kuwa Naibu wa Askofu wa Jimbo la Peramiho ambalo baadaye lilibadilika kuwa Jimbo la Songea.

Hivi mpaka wakati mheshimiwa padre Maurus G. Komba anateuliwa kuwa askofu wa Tanga, alikuwa amebobea katika utume wake wa kichungaji na pia akiwa na mang'amuzi mazito ya uongozi katika kanisa kwa kufanya kazi na waumini, mapadre wenyeji na wamisionari masista, mapadre, na mabruda.

e). Askofu Mteule na Mapadre Wenyeji Wamisionari Toka Peramiho

Historia inaonyesha kwamba askofu mteule hakuwa mgeni Tanga hivi kwani mapadre wenzake wananchi toka Jimbo la Peramiho/Songea walikwisha kuja na kufanya umisionari katika Jimbo la Tanga kabla ya ujio wake. Baba Askofu Arthurs aliwaomba mapadre hao kutoka Peramiho kuja kufanya uchungaji Jimboni Tanga kwa wananchi wengi wa mikoa ya kusini waliokuwa wakifanya kazi mkoani Tanga. Kwa makandokando haya, askofu mpya mteule alikuwa kwa kiasi hafahamiki na kwa kiasi fulani anafahamika kwa wana-Tanga. Alipofika Tanga, askofu mteule alikutana na matabaka mengi ya kijamii na kidini mazingira yaliyokuwa tofauti ya hali iliyokuwamo katika jimbo lake la nyumbani. Namba ya Wakatoliki katika Tanga ilikuwa ni ndogo sana kulinganisha na Peramiho. Namba ya mapadre na masista wamisionari na wenyeji pia ilikuwa ndogo sana kulinganisha na ile ya Peramiho. Mapadre wazalendo wakati anatawazwa kama askofu wa Tanga walikuwa watatu tu.

f). Siku za Mwanzo za Askofu Mteule Jimboni Tanga

Baba askofu mteule aliwasili jimboni Tanga mwezi Januari 1970 kuweza kulifahamu Jimbo kabla ya kutawazwa kwake. Kwa mwezi wote uliofuatia aliweza kusafiri katika kila parokia ya jimbo na kukutana na mapadre na mabruda waliofanya kazi jimboni. Katika ziara hiy aliweza kukutana na masista pamoja na waumini wa jimbo. Zoezi hili lilimletea picha bora kwa wenyeji wake waliompenda kutokana na moyo wake wa ucheshi na upendo. Hivi hadi muda wa kutawazwa kwake ulipofika Machi 15, 1970, wana-Tanga wengi walikuwa wanamfahamu kwa kiasi kikubwa na walifurahia kuhudhuria sherehe yake za kutawazwa kule Chumbageni. Kuwa na askofu mzalendo katika Tanga haikuwa rahisi kuzoeleka kwa wana Jimbo la Tanga waliokuwa wamezoea kazi za wamisionari wazungu.

Pamoja na ugeni wa wana-Tanga kuwa na kiongozi mzalendo, Askofu Maurus aliwasaidia sana wana-Tanga kujisikia karibu na uongozi huo kutokana na tabia yake ya uchakaramu, upendo, kushukuru, na kutambua vipaji vya watu. Alikuwa mtu wa upendo na shukurani. Kwa kweli alikuwa amejiandaa kuwatumia watu wa Mungu katika Jimbo la Tanga kwa upendo na ukweli. Alitanya kila jitihada ya kukutana na wanajimbo katika ngazi zote za Jimbo, parokia, na vigangoni. Alichukua nafasi ya kuzungumza na watu na kuwasikiliza kwa makini.

g). Mang'amuzi ya Miaka Mitano ya Mwanzo ya Uaskofu
 
Katika miaka mitano ya mwanzo ya uaskofu wake jimboni Tanga, Askofu Maurus alianza kuhisi upungugu wa wamisionari wa Kirosmini jimboni. Mapadre wachache wapya wamisionari walikuwa wanakuja jimboni. Umri wa wale waliopo ulikuwa unazidi kuwa mkubwa na baadhi yao walikuwa wakirudi Ulaya kwa sababu kadha wa kadha. Baba Maurus alijaribu kutembelea Ireland na hata Amerika ya Kaskazini akiwa na lengo la kufanya kampeni ya kupata wamisionari mapadre na mabruda zaidi kwa ajili ya uchungaji Tanga. Majibu aliyoyapata huko hayakutia moyo kabisa.

Mang'amuzi haya yalimfanya baba askofu Maurus kuanza kufanya kampeni ya kina ya kupata miito ya mapadre na watawa ndani ya jimbo. Japo aliendelea kupata waseminari kutoka maparokiani, hakuridhika sana na mfumo wa kupeleka waseminaristi hapo kwenye seminari ya umoja wa majimbo kule Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro Jimboni Morogoro. Baba askofu Maurus aliona kwamba nafasi ambazo tunapata kupeleka waseminari kule Morogoro ilikuwa ni finyu mno. Njaa ya kuwa na seminari ndogo ya jimbo ilikuwa kubwa mno ndani ya roho ya baba askofu. Binafsi alikuwa na mang'amuzi ya pekee ya ubora wa kuwa na seminari ndani jimbo. Katika jimbo lake la nyumbani kule Peramiho waliweza kupata miito mingi kwa kuwa na seminari ndogo ya Likonde na pia kuwa na seminari kubwa ya Peramiho. Vitalu hivyo vililea miito mingi na mizuri.


h). Askofu Maurus Aanzisha Seminari Ndogo ya Jimbo

Njozi ya kuwa na seminari ndogo ya Jimbo la Tanga ilikuwa ukweli katika mwaka wa 1976. Katika mwaka wa 1974 Warosmini walimkabidhi baba Askofu Maurus majengo mazuri ya iliyokuwa shule yao ya kimataifa ya bweni kule Soni. Shule ile iliyofahamika kama shule ya Mtakatifu Mikaeli ilikuwa ikifundisha watoto wanaume wa kizungu na wa kiasia ambao wazazi wao walikuwa wakifanya kazi katika taasisi za kikoloni Afrika ya Mashariki. Kutokana na kupungua kwa wafanyakazi wa Kizungu na Kiasia katika Afrika Mashariki basi hata idadi ya watoto waliojiunga na shule ya Mtakatifu Mikaeli ilipungua na kuishinikiza. Hivi mara baada ya kupata majengo hayo, baba askofu alimtuma mheshimiwa padre Gerald Chilambo kukusanya vijana toka jimboni na kuanza seminari katika mwaka 1975. Japo baba Chilambo alipata vijana kadhaa katika mwaka huo hakuweza kuisajili seminari mwaka huo hadi ilipofika mwaka 1976.

Kwa kuanzishwa kwa seminari ndogo ya Soni, vijana wengi toka maparokia yote ya jimbo waliweza kupata nafasi ya kujiunga katika malezi ya shule hii. Kwa msaada mkubwa wa masista na mapadre wa Jimbo la Tanga na pia kwa ukarimu mkubwa wa wamisionari walikuokuwa wanafanya kazi jimboni (Warosmini na Wabenediktini), seminari ilianza, ikakua, na ikazaa matunda. Kabla mhashamu baba askofu Maurus kustaafu uongozi wa Jimbo la Tanga, aliweza kupadirisha mapadre sita walioanza malezi yao ya awali katika seminari ya Soni. Mapadre hao ni John Mahundi (1985), Severine Yagaza (1986), Charles Mhina (1987), Laurent Mapunda (1987), Joseph Mbenna (1987), and Leopold Nyandwi (1987). Katika kipindi kizima cha uongozi wake, kipindi cha miaka 18, baba askofu Maurus Komba alipadirisha jumla ya mapadre wa jimbo 26.

i). Miito ya Masista Wenyeji

Katika safari zake za kichungaji maparokiani kote, baba askofu Maurus hakusinzia kuhimiza miito. Kwa moyo wake wote alishirikiana na uongozi wa masista wa jimbo COLU kuhimiza miito ya masista na ubora wao kimwili na kiroho.

j). Ufunguzi wa Parokia Mpya
Katika kipindi cha uaskofu wake, Baba Askofu Maurus alifungua parokia mpya kumi. Sababu kuu za kufungua parokia hizi kumi ilikuwa ni: kuongezeka kwa idadi ya Wakatoliki jimboni, ukubwa wa parokia zilizokuwepo, ongezeko la watenda kazi katika shamba la mizabibu haswa kwa upande wa mapadre wazalendo.
Parokia ya Pangani ilifunguliwa katika mwaka 1973 kutoka katika eneo la Parokia ya Mtakatifu Teresa, Tanga.
Parokia ya Hale ilifunguliwa mwaka 1974 kutoka katika eneo la Parokia ya Potwe.
Parokia ya Handeni ilizaliwa mwaka 1976 toka katika Parokia ya Kwediboma.
Mwaka huo huo wa 1976 Parokia ya Sakharani ilizaliwa toka katika Parokia ya Gare.
Katika mwaka huo huo wa 1976 Parokia ya Malindi ilianzishwa toka Parokia ya Gare.
Katika mwaka 1985 parokia mbili zilianzishwa. Parokia hizi ni Amani toka katika parokia ya Muheza na
Parokia ya Mtakatifu Petro-Pongwe Saruji toka katika Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga.
Parokia ya mwisho katika utawala wake ilikuwa ni Parokia ya Mombo iliyozaliwa mwaka 1986 na ilitoka katika eneo la Parokia ya Mazinde.

k). Siku za Mwisho za Uongozi wa Askofu Maurus

Afya ya mhashamu baba askofu Maurus Komba ilianza kuterereka katika mwaka wa 1983 wakati alipoanza kupata msaada wa matibabu ya ugonjwa wa moyo katika hospitali ya Litembo, wilayani Mbinga. Matatizo ya ugonjwa wa moyo hayakusimama kabisa katika mwaka huo. Matatizo haya yaliendelea na kupunguza mno nguvu ya utendaji wake wa kazi. Kwa nguvu na upendo wake wote aliokuwa nao kwa Jimbo la Tanga, baba askofu Maurus aliendelea kulihudumia Jimbo la Tanga hadi Vatikani ilipokubali ombi lake la kujiuzulu hapo Januari 18, 1988. Baada ya kujiuzulu kwake na baada ya kulikabidhi jimbo kwa askofu aliyemfuatia, baba askofu Maurusi alirudi Jimboni Mbinga kuishi maisha ya askofu mstaafu. Baba Maurus Komba aliishii hapo Mbinga hadi Februari 23, 1996 alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 73. Mwili wa Askofu Maurus Komba umezikwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Aloisi Gonzaga, ambalo lililokuwa kanisa kuu la mwanzo la Jimbo la Mbinga kabla ya kuhamisha makao makuu ya Jimbo hilo kwenda kule yaliko sasa.

ONGEZEKO LA PAROKIA CHINI YA UONGOZI WA MHASHAMU BABA ASKOFU MAURUS KOMBA 1970-1987

Kipindi hiki kilishuhudiwa na ongezeko la Parokia kumi:

1973 Kanisa la Bikira Maria Nyota ya Bahari-Pangani

1974 Kanisa la Bikira Maria Malkia na Mama-Hale

1976 Kanisa la Mtakatifu Paulo Wana wa Ibrahim- Handeni

1976 Kanisa la Mtakatifu Yosef Mume wa Bikira Maria -Magoma

1976 Kanisa la Mtakatifu Yosef Mfanyakazi-Sakharani

1976 Kanisa la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu-Malindi

1985 Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Amani-Amani

1985 Kanisa la Mtakatifu Petro Mtume -Pongwe Saruji

1986 Kanisa la Watakatifu Gregori na Katarina-Kabuku

1986 Kanisa la Mtakatifu Yosef Mume wa Bikira Maria-Mombo

B. MHASHAMU ASKOFU TELESPHORE MKUDE (1988 - 1993)

a). Kuteuliwa kwa Askofu Telesphore Mkude
Mhashamu Askofu Telesphore Mkude aliteuliwa kuwa askofu wa tatu wa Jimbo la Tanga akiwa askofu wa pili mzalendo hapo Januari 18, 1988. Tarehe ya uteuzi wake ilienda sambamba na tarehe ya kukubaliwa kujiuzulu kiti cha kiaskofu cha Jimbo la Tanga kwa mhashamu Bishop Maurus Komba. Askofu mteule Telesphore Mkude alikuwa padre wa Jimbo la Morogoro. Hadi uteuzi wake kuwa askofu wa Jimbo la Tanga, askofu mteule alikuwa Naibu wa Askofu wa Jimbo la Morogoro na pia mlezi wa kiroho wa masista wa Mgolole. Askofu mteule alitawazwa kuwa askofu wa Tanga katika madhehebu yalifayofanyika Aprili 26, 1988 katika viwanja vya kanisa kuu la kiaskofu Jimboni Tanga. Askofu kinara aliyemtawaza alikuwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, aliyekuwa askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam na maaskofu vinara washiriki walikuwa mhashamu Maurus Komba, askofu mstaafu wa Jimbo la Tanga na Adrian Mkoba, askofu wa Jimbo la Morogoro.

Bishop Telesphor Mkude

b). Miaka ya Mwanzo ya Askofu Mkude Tanga
i). Ujio wa Baba Mtakatifu Yohani Pauli II Tanzania: Toka siku aliyopokea madaraka ya kuwa askofu wa Tanga, askofu Mkude aliendelea kazi njema ya uchungaji jimboni iliyoanzwa na watangulizi wake. Toka mwanzo alinza kufanya kazi kwa bidii ya kulichunga kundi lake kwa upendo. Moja ya kazi za kubwa katika miaka ya mwanzo wa uongozi wake ilikuwa ni kuliandaa Jimbo la Tanga na kanisa zima la Tanzania katika mapokezi ya kihistoria ya ujio wa Baba Mtakatifu Yohane Pauli II katika Tanzania, ujio uliofanyika Septemba 1 - 5, 1990. Baba askofu Mkude aliuunganisha ujio wa kihistoria wa Baba Mtakatifu Tanzania katika uchungaji wake wa jimbo kwa kuwaalika wana-Tanga kujiandaa kimwili na kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio huo mkubwa wa mchungaji mkuu wa kanisa.
ii). Mjengo wa uongozi jimbo: Toka siku za mwanzo za uongozi wake, askofu Mkude alipenda kujenga muundo wa wazi na sahihi wa uongozi wa kijimbo. Alizitoa ofisi za jimbo toka kwenye nyumba ya askofu ya Razkazoni kuja kwenye makao makuu ya jimbo Chumbageni. Katika mwendo huo alianza kufanya kampeni za ujengwaji mwa makao mkuu ya kichungaji jimboni pale Chumbageni. Kampeni hii iliendelea muda wote wa ungozi wake japo hakuweza kunza ujenzi wa kituo hiki hadi alipofika askofu Anthony Banzi.

iii). Nyumba ya malezi Gare: Mwaka 1991 Askofu Mkude alinza nyumba ya malezi ya waseminari kule Gare kuweza kuwalea waseminari waliomaliza masomo ya sekondari na ambao walikuwa wanaelekea kwenye masomo ya filosofia. Alimteua mheshimiwa padre John Kika Zuakuu kuwa mkurugenzi wa kituo hicho. Baadaye kituo hiki kilihamia Shashui karibu na Soni Seminari.


c). Miito Mitakatifu Jimboni
Baba askofu Mkude alikuwa katika mstari wa mbele wa kazi kubwa ya kulea miito ya huduma kanisani. Alihimiza mengi katika makuzi na ubora wa malezi pale seminarini Soni. Alimteua mheshimiwa padre George Mhuza kuwa gombera wa Soni Seminari na pia alipigania sehemu ya eneo la Soni Seminari kurudishwa mikononi mwa seminari kutoka kwa wananchi waliolichukua eneo hilo katika miaka ya nyuma. Askofu Mkude aliendelea kulea malezi ya mapadre kwa kuhimiza mafungo ya mapadre ya kiroho na pia umoja kushiriki na kuudumisha umoja wa mapadre jimbo UMAWATA.


d). Wamisionari na Masista Jimboni
Baba askofu Mkude aliendelea kufanya kazi na kuwahimiza wamisionari jimboni katika mchango wao mkubwa katika shughuli za kichungaji. Alizitambua kazi zao njema jimboni. Alizitambua na kuzihimiza kazi za masista wa jimbo na wamisionari katika jimbo. Katika kipindi chake cha uongozi masista wazalendo walizidi kutanua huduma zao za kichungaji ndani na nje ya Jimbo la Tanga.

e). Ufunguzi wa Parokia mpya
Katika wakati wa uongozi wake kama askofu wa Tanga, askofu Mkude alifungua parokia tatu jimboni. Parokia hizo ni Parokia ya Soni mwaka 1989 iliyomegeka kutoka Parokia ya Gare. Parokia ya Mtakatifu Matias Mulumba mwaka 1990 iliyomegeka kutoka Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga. Parokia ya Manundu mwaka 1991 iliyomegeka kutoka Parokia ya Kilole.

f). Taasisi ya Afya
Askofu Mkude hakuwa nyuma katika maswala ya Afya ya jamii. Katika uongozi wake, baba askofu alisimama vyema kuanzisha Hospitali ya Tumaini iliyopo maeneo ya Kisosora jijini Tanga. Kituo hiki cha afya kimekuwa ni jibu kubwa katika maswala ya afya ya mapadre na masista jimboni Tanga na haswa kwa wananchi wa jiji la Tanga na majirani zake.
g). Mwisho wa Uongozi wa Askofu Mkude
Uongozi wa askofu Telesphore Mkude jimboni Tanga ulimalizika Aprili 5, 1993 alipoteuliwa kuwa askofu wa Jimbo la Morogoro kufuatia kujiuzulu kwa kiti hicho kwa mhashamu Askofu Adrian Mkoba. Askofu Mkoba alijiuzulu kuwa askofu wa Morogoro Novemba 6, 1992.
Katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake jimboni Tanga, askofu Mkude aliweza kupadirisha mapadre kumi kuwa mapadre wa Jimbo la Tanga.

 

C: KIPINDI CHA MPITO (APRILI 10, 1993 - JUNI 10, 1994)

Baada ya baba Askofu Mkude kuondoka Tanga kwenda Morogoro, mheshimiwa padre Casmir Magwiza alichaguliwa kuwa padre kiongozi wa Jimbo la Tanga, nafasi aliyoishikilia kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi Askofu Anthony Banzi alipoteuliwa kuwa askofu wa Tanga. Katika kipindi hiki cha zaidi ya mwaka mmoja, padre Magwiza alifanya kazi njema jimboni ya kuwaongoza waumini wa Tanga kuishi imani yao ya ki-Kikristu. Pia aliwaandaa waumini wa Tanga kuweza kumpokea askofu wao mpya na kufanya naye kazi.

 

D: MHASHAMU ASKOFU ANTHONY BANZI (1994 - 2020)

a). Kuteulikwa kwa Mheshimiwa Padre Anthony Banzi

Vatikani ilimteua mheshimiwa padre Anthony Banzi aliteuliwa kuwa Askofu wa Tanga hapo Juni 10, 1994. Baba Banzi alitawazwa kuwa Askofu wa Tanga hapo Septemba 15, 1994. Yeye ni padre wa Jimbo la Morogoro na kabla ya uteuzi wake kuwa askofu wa Tanga alikuwa ni Gombera na Jalimu la falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho kule Moshi. Askofu kiongozi aliyemtawaza alikuwa Mwadhama Polycarp Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam na maaskofu wasaidizi katika kutawazwa kwake walikuwa Mhashamu Askofu Telesphore Mkude, askofu wa Jimbo la Morogoro na Mhashamu Askofu Josephat Louis Lebulu ambaye alikuwa askofu wa Jimbo la Same (baadaye askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha).

b). Uongozi Mahiri wa Askofu Banzi

Baba askofu Banzi amelipatia Jimbo la Tanga uongozi mahiri katika kipindi cha kumaliza Karne ya 20 na kuijongelea Karne ya 21. Kwa nguvu za kutosha amezienzi shughuli za kichungaji jimboni mwote na kwa namna zote njema. Amelipatia kipaumbele swala la kuhimiza miito jimboni na kuuenzi utume wa masista wetu wa COLU jimboni.

Bishop Anthony Banzi

c). Elimu ya Juu kwa Mapadre wa Jimbo

Askofu Banzi amezibariki na kuhimiza elimu ya juu kwa mapadre wa jimbo kwa kuwapeleka masomoni mapadre hawa kwenye vyuo vikuu ndani na nje ya nchi. Mapadre kadha wa kadha wamesomo katika vyuo vikuu kule Nairobi Kenya, Italy, Austria, na Amerika ya Kaskazini. Kwa mapadre hawa kupata elimu ya juu kumewawezesha mapadre hao kufanya utume pekee ndani ya jimbo na hata nje ya jimbo la Tanga kwenye taasisi za kanisa kitaifa na kimataifa kama kule Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, vyuo viandamizi vya SAUT, seminari kubwa nchini na hata AMECEA.

d). Ujenzi wa Majengo ya Jimbo

Baba askofu Banzi alianza ujenzi wa jengo la ofisi za kichungaji jimboni, jengo ambalo harakati zake za awali zilianzishwa na askofu aliyemtangulia. Kadhalika askofu Banzi amesimamia ujenzi wa jengo kubwa la Baba Mtakatifu Yohane Pauli II jengo ambalo limekuwa na huduma ya malazi na chakula kwa wageni wetu wafikao jimboni. Jengo hili linaiangalia Bahari ya Hindi. Pia baba askofu Banzi ameweza kupanua nyumba ya askofu kule Raskazoni kitu ambacho kimekuwa baraka kubwa kwa wageni wengi wafikao uaskofuni. Zaidi ya kupanua nyumba yake pia aliweza kupata jengo kubwa jirani ya makao yake kutoka Mamlaka ya Mkonge na ameweza kulifanya jengo hilo kuweza kukarimu wageni wetu wa jimbo.

e). Kalenda ya Matukio Jimboni

Kichungaji, baba askofu Banzi ameweza kuratibu kalenda ya matukio jimbo ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kuratibu shughuli za kijimbo katika ngazi ya jimbo na pia katika ngazi ya parokia.

f). Utume wa Masista Wenyeji Jimboni

Toka afike jimboni Tanga askofu Banzi amekuwa bega kwa bega katika kulea miito ya masista wenyeji jimboni. Katika kipindi chake ameendelea kushirikiana na masista hawa na kuendelea kuwahimiza katika utume wao ndani ya kanisa la Tanga na kanisa la ulimwengu. Utume wa masista wa COLU umeendelea kupamba moto katika ngazi za shirikani, maparokiani, na hata katika majimbo mengi ya Tanzania.

g). Utume wa Wamisionari Jimboni

Baba askofu Banzi aliendelea kuzitambua na kuzikumbatia kazi njema ambazo mashirika yetu ya wamisionari yamekuwa yakizifanya ndani ya jimbo la Tanga. Mapadre na mabruda katika shirika la Warosmini hivi sasa ni wenyeji wakati hapo walipofika mwanzo katika mwaka 1948 walikuwa wote ni Wazungu. Warosmini hawa wamekuwa ni sehemu kubwa ya kazi ya uinjilishaji Jimboni Tanga. Hadi hivi sasa wanahudumia parokia zaidi ya sita jimboni zikiwa ni parokia za Gare, Lushoto, Mombo, Kwalukonge, Kwai na Mtakatifu Petro Saruji. Askofu Banzi aliendelea kufanya kazi na mapadre na mabruda wa Kibenediktini ambao hivi sasa wanahudumia parokia mbili za Soni na Mabughai. Askofu Banzi aliendelea kufanyakazi na mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu ambao wana nyumba yao ya malezi kule Magamba Lushoto. Kadhalika aliendelea kuuezi utume wa dada zetu masista wa Damu Azizi ya Yesu ambao ni wakongwe katika Tanga na kwa muda huu wapo kule Kifungilo na Lushoto. Baba Banzi alikuwa karibu kabisa na utume wa muda mrefu wa sista Karen wa shirika la masista wa Dada Wadogo wa Mtakatifu Francis wa Asisi wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu anayefanya utume kwa Wamasai kule Handeni. Baba Banzi aliweza kuyakaribisha jimboni mashirika kadha ya kadha ya wamisionari. Aliwakaribisha mapadre wa Kazi za Roho Mtakatifu (ALCP/OSS) ambao hivi sasa wanafanya kazi za kichungaji katika Parokia ya Kabuku. Aliendelea kuyakaribisha mashirika kadha kadha ya kitawa kuishi ndani ya Jimbo wakati yakitafuta njia za kujitegemea na kuinjilisha. Hivi sasa tunao Wapashenisti ambao wana utume wa kilimo kule Zeneti, Muheza. Pamoja nao ni masista wa shirika la IVREA. Kule Mivumoni Pangani wapo watawa wa Kifransiskani wakiwa na utume wa kilimo pia. Kule Pangani mjini masista wa Roho Mtakatifu kutoka Moshi wameweza kuanzisha nyumba ya ukarimu. Masista wa Shirika la Mtakatifu Gema Galgani kutoka Dodoma wamefungua

nyumba yao ya kilimo kule Chang'ombe, Segera/Hale wakati masista wa shirika la Huruma ya Mungu nao wamefungua nyumba yao na shamba kule Mailikumi, Korogwe.

Pamoja na mashirika hayo hapo juu, Baba Banzi aliwaalika masista wa Collegine kufanya utume ya malezi ya watoto wa mitaani kule kitongoji cha Bombo jijini Tanga. Pamoja nao bado tunao watawa wa Shirika la Roho Mtakatifu ambao wana nyumba yao ya unovisi kule Magamba Lushoto.

h). Uinjilishaji na Teknologia

Baba Banzi alikuwa mstari wa mbele kujizingirisha na uinjilishaji kutumia teknolojia zilizopo katika Karne ya 21. Katika muda wa uongozi wake amebariki na kusukuma kwa karibu sana uanzishwaji wa Radio Huruma ambayo inaendelea kuinjilisha jimbo zima. Aliweza kumwandaa mheshimiwa padre Richard Kimbwi kuweza kuongeza elimu ya kitaalamu katika uendeshaji na uhandisi wa radio hiyo. Pamoja na utume kwa njia ya radio, askofu Banzi pia alibariki na kusukuma kuwepo kwa tovuti ya jimbo ambayo ni kiungo kikubwa katika shughuli za kichungaji kwa wana-Tanga katika ulimwengu wa utandawazi. Hivi sasa Jimbo la Tanga linaweza kupatikana katika tovuti yake rasmi www.dioceseoftanga.org.

i). Utume wa Makatekista Jimboni

Baba askofu Banzi aliutambua sana utume wa makatekista katika kuliinjilisha Jimbo la Tanga hapo nyuma, sasa, na siku zote mbeleni. Kwa hali na mali baba askofu amewahimiza makatekista na pia kupigania haki zao na kuendelea kuboresha maandalizi ya kazi zao. Katika uongozi wake, kulikuwa na uongozi maridhawa wa kuangalia malezi ya makatekista kijimbo kimwili, kiroho, na kitaaluma. Baba Banzi aliiboresha sana Idara ya Katekesi Jimbo kuweza kujihusisha mno katika kujenga programu mahsusi kukuza elimu ya walimu hao wa dini. Kumekuwa na warsha kadha wa kadha ndani ya jimbo kuwaboresha makatekista. Baba Banzi alijenga chuo cha kusomesha makatekista pale Parokia ya Mlingano. Chuo hiki kilifunguliwa rasmi kwa baraka zake siku ya Jumamosi Machi 2, 2013.

j). Ufunguzi wa Parokia Mpya Jimboni

Toka alipoingia jimboni Tanga, Baba Banzi aliweza kufungua parokia mpya sita Parokia hizo ni zile za:
Tekwa (2001) iliyotoka ndani ya Parokia ya Sakharani,
Kwalukonge (2001) iliyotoka Parokia ya Mombo.
Parokia ya Mkuzi (2003) iliyotoka Parokia ya Kwai.
Parokia ya Mabughai (2010) iliyotoka Parokia ya Lushoto.
Amboni (2011) toka Parokia ya Mtakatifu Anthoni Tanga, na
Parokia ya Mtindiro (2011) toka Parokia ya Muheza.
Kadhalika hadi mwaka huu wa 2013 alikwisha zitangaza parokia tarajiwa tatu ambazo ni:
Misozwe toka Parokia ya Mlingano,
Mkalamo toka Parokia ya Pangani, na
Donge toka kwenye Parokia ya Mtakatifu Matias Mulumba Tanga.

k). Upadirisho wa Mapadre wa Jimbo

Toka atawazwe kuwa askofu wa Tanga katika mwaka 1994 hadi mwaka huu wa 2020, askofu Banzi aliweza kupadirisha mapadre 36 wa jimbo. Hiyo ni namba kubwa mno ya watendakazi katika shamba la mizabibu. Ni kutokana na baraka hii, basi mhashamu Banzi aliweza kuwa na uwezo wa kuweza kuwatuma baadhi ya mapadre wa jimbo kwenda kufanya elimu ya juu na pia kuweza kushiriki vyema katika kushiriki kuzijenga taasisi za Kanisa la Tanzania kwa kupeleka baadhi ya mapadre kufanya utume kule SAUT na seminari kubwa za umoja wa majimbo.

l). Askofu wa Kwanza Mwana-Tanga

Ni katika kipindi cha uongozi wa jimbo wa mhashamu askofu Anthony Bazi basi padre mwana Tanga aliteuliwa kuwa askofu. Hapo Jumamosi Februari 16, 2013 Vatikani ilimtangaza mheshimiwa padre Titus Joseph Mdoe, padre mzawa wa Jimbo la Tanga kuwa askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam. Hili limekuwa tukio la kihistoria katika jimbo la Tanga kwa kupata askofu mzawa toka jimbo hili liundwe hapo mwaka 1958. Askofu Mteule Mdoe ni mzawa wa Jimbo la Tanga toka Parokia ya Gare na alipadirishwa Juni 24, 1986 na kufanya kazi jimboni Tanga kama padre msaidizi, paroko, mkurugenzi wa miito jimbo, na pia mkurugenzi wa vijana jimbo. Hivi karibuni alitumwa kufanya utume katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Tanzania cha Nyota ya Bahari kule Mtwara ambako alikuwa mtunza fedha. Ni katika nafasi hiyo basi aliitwa kuwa askofu msaidizi.

m). 20.12.2020 Kifo cha Askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Tanga

Askofu Anthony Mathias Banzi alikuwa ni Padre wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Alikuwa ni Askofu wa nne wa Jimbo Katoliki la Tanga. Alizaliwa tarehe 28.10.1946 huko Tawa, Morogoro. Alipata Daraja Takatifu la Upadre tarehe 29.07.1973 huko Jimboni Morogoro. Tarehe 10.06.1994, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga. Tarehe 15.09.1994 alisimikwa na kuwekwa Wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga katika Kanisa kuu la Mt. Anthony wa Padua Tanga. Tarehe 15.09.2019 aliadhimisha Jubilei yake ya miaka 25 ya Uaskofu katika Jimbo Katoliki la Tanga na hivi kuwa Askofu wa kwanza kutimiza 25 katika kulitumikia Jimbo la Tanga. Tarehe 20.12.2020, Askofu Anthony Banzi baada ya kuugua kwa muda kidogo aliitwa na Bwana akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Amezikwa katika Kanisa kuu la Mt. Anthony wa Padua akiwa pia ni Askofu wa kwanza kuzikwa katika Kanisa hilo la Jimbo. Amefariki akiwa na miaka 74 ya kuzaliwa, 47 ya Upadre na 26 ya Uaskofu.

m). 07.06.2023 Padre Thomas Kiangio Ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga

Askofu Mteule Thomas John Kiangio alizaliwa 17.03.1965 katika Kijiji cha Mazinde Ngua, Kata ya Mazinde Ngua, katika Wilaya ya Korogwe katika Mkoa wa Tanga. Wazazi wake ni Baba John Mussa Kiangio na Mama Paulina Ally Suba. Mwaka 1975 hadi 1981, alipata Elimu ya Msingi Mazinde Ngua, Mazinde. Safari yake ya masomo na majiundo ya Kikasisi ilianzia seminari ndogo Mtakatifu Yosefu-Soni 1982 na baadaye Seminari Ndogo ya Mt. Petro iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro, kati ya Mwaka 1987 hadi mwaka 1989. Aliendelea na masomo ya Falsafa, Seminari Kuu ya Mt. Anthony, Ntungamo Jimbo Katoliki Bukoba kati ya mwaka 1989 hadi 1991. Aliendelea na masomo ya Taalimungu, Seminari Kuu ya Mt. Karol Lwanga, Segerea Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kati ya mwaka 1991 hadi 1997. Mwaka 1994-95 alifanya mazoezi ya shughuli za Kichungaji katika Parokia ya Mlingano. Mwaka 1995, alipata mafunzo ya Afya ndani ya mwaka wa Kichungaji huko Bugando, Jimbo kuu la Mwanza. Alipata Daraja Takatifu la Ushemasi mnamo tarehe 01.01.1997, katika Kanisa Kuu la Anthony Tanga. Alipata Daraja Takatifu la Upadre 16.07.1997, Parokia ya Mama Bikira Maria Mama wa Mateso, Mazinde Ngua. Baada ya Upadrisho alihudumu katika nafasi na sehemu zifuatazo: Mwaka 1997 mpaka 1998, Paroko Msaidizi Parokia ya Ekaristi Takatifu, Lushoto. Mwaka 1998 mpaka 1999, Mlezi na Mwalimu na Gombera Msaidizi wa Seminari Ndogo ya Mt Yosefu Soni, Tanga.
Mwaka 1999 hadi 2004, alitumwa na Jimbo Katoliki la Tanga kwenda Nchini Italia kujiendeleza zaidi na masomo na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Taalimungu (Dogma), katika Chuo cha Kipapa cha Urbaniana, Roma. Baada ya kurejea Nchini Tanzania, alitumwa katika Seminari Ndogo ya Mt. Yosefu Soni, kama Gombera tangu mwaka 2005 hadi 2013.Tangu Mwaka 2013 mpaka 2020, Askofu Mteule alikuwa Katibu Mkuu wa Jimbo. Baada ya Kifo cha aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Hayati Askofu Anthony Mathias Banzi, Askofu Mteule alihudumu kama Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Tanga tangu 24.12.2020 hadi 07.06.2023 alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.

bp_thomas_kiangio
Askofu Thomas Kiangio


1. SEHEMU YA KWANZA: KARNE YA 16 - 1947
MBEGU ZA MWANZO ZA UKATOLIKI TANGA,

2. SEHEMU YA PILI: 1948 - 1958
PREFEKTURE YA TANGA: WAROSMINI MIAKA YA AWALI

3. SEHEMU YA TATU: 1959 - 1969

TANGA YAWA JIMBO: ASKOFU EUGENE ARTHURS, I.C.