PAROKIA YA WAT. PAULO NA IBRAHIMU
HANDENI TANGA
DEKANIA YA HANDENI
Parokia ya Wat. Paulo na Abrahamu (1976) RATIBA YA IBADA: |
Mt. Abrahamu Mt. Paul Mtme Wat. Paul na Abrahamu |
Ofisi ya Parokia | |
Ukumbi wa parokia | |
Baadhi ya waamini wa jamii ya kimasai katika ibada wakiimba |
HISTORIA YA PAROKIA
Hapo awali Handeni ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Kwediboma. Mapadre toka Kwediboma walitembelea Handeni kwa utume wa kichungaji
na halafu walirudi tena Kwediboma. Japo Handeni imekuwa makao makuu ya wilaya ya Handeni, idadi yake ya wa-Kristu wa-Katoliki
ilikuwa ndogo sana. Wenyeji wengi wa Handeni na vitongoji vyake ni wa madhehebu ya ki-Isilamu. Wa-Katoliki na wa-Kristu wa
madhehebu mengine waishio Handeni wamekuwa ni waajiriwa kwenye taasisi binafsi au za serikali au wahamiaji waliofika hapa kwa
shughuli zao za maisha. Japo idadi ya wa-Katoliki imekuwa ndogo, jimbo Katoliki lilipata changamoto ya kuweza kuwa na parokia
yake katika makao haya makuu ya wilaya.
Katika miaka ya mwanzoni ya 1970, uongozi wa jimbo la Tanga ulimtuma mheshimiwa padre John Haule (padre mmisionari kutoka Jimbo
la Songea) kutoa huduma za kichungaji kwa waumini walio katika mji wa Handeni. Padre Haule aliishi katika nyumba ya kupanga toka
kwa mwananchi kwa kuwa jimbo halikuwa na nyumba yake kwa matumizi ya padre. Katika mwaka 1976, mheshimiwa padre Odilo Hueppi, OSB
aliwasili Handeni akitokea Abasia ya ki-Benediktini ya Ndanda akiwa na lengo la kufanya uchungaji wa muda mrefu jimboni Tanga.
Padre Hueppi alikuwa na mitazamo miwili ya utume. Mitazamo hiyo ilikuwa ni utume kwa wananchi wakazi wa Handeni na pia utume kwa
jamii ya ki-Masai ambayo ina asili ya uchungaji wa ng'ombe na hivi ni watembezi katika kutafuta malisho ya mifugo yao. Kwa mtazamo
huu wa uchungaji na kwa ushirikiano wa karibu wa sista Karen ambaye ni mtaalamu wa tiba za wanyama, waliweza kuwa mitume halisi wa
jamii ya ki-Masai katika Jimbo la Tanga.
Tokea padre Hueppi awasili Handeni, aliweza kuijenga parokia ya Handeni kuwa kituo kikubwa cha uchungaji wa kanisa Katoliki.
Aliweza kujenga kanisa kubwa la kuabudia na pia kuweza kujenga nyumba ya mapadre, nyumba ya masista, nyumba nyingi ambazo zinatumika
kama makao ya wa-Masai wafikapo mjini Handeni toka mbugani, na pia aliweza kujenga nyumba nyingi za kupangisha wananchi kama mradi
maalumu wa kuisaidia parokia kujiendesha. Kwa kujenga makao haya makuu ya parokia, padre Hueppi alijenga mradi mkubwa wa maji ya
mvua yaliyovunwa toka katika paa za nyumba zote hizi na kuyaingiza katika visima vilivyokuwa na uwezo wa kukusanya zaidi ya
lita 60,000 za ujazo. Mradi huu wa maji umekuwa mkombozi mkubwa kwa wanajumuia wanaoishi au kufikia katika makao haya ya parokia
haswa ukizingatia kwamba mji wa Handeni una uhaba mkubwa wa maji. Pamoja na majengo yote hayo, padre Hueppi aliweza kuendelea na
ujenzi wa shule ya chekechea, shule ya maarifa ya nyumbani kwa wasichana, na pia zahanati ya wanyama.
Padre Hueppi alifariki katika mwaka 1998. Tokea wakati huo, parokia ilikabidhiwa kwa askofu wa jimbo ambaye amekuwa akiwatuma
mapadre wa jimbo kuishi hapo na kutoa huduma za kichungaji. Sista Karen ameendelea kuwepo parokiani hapo akiendelea na utume wake
kwa wa-Masai kama mganga wa mifugo yao na nuru kubwa ya Injili.
Mapadre wazawa wa Parokia ya Handeni ni: Lawrence Mapunda (1987) na Emmanuel Mavengero (1989).