PAROKIA YA WAT. GREGORI NA KATARINA
KABUKU TANGA
DEKANIA YA HANDENI
Parokia ya Wat. Gregori na Katarina (1986) RATIBA YA IBADA: |
Mt. Gregori Mkuu Mt. Katharina wa Siena Wat. Gregori Mkuu na Katharina wa Siena |
Kanisa la Kabuku kwa ndani
| Grotto la Maria
| Nyuma ya masista wanaohudumu Kabuku
| Nyumba ya mapadre Kabuku |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Kabuku imejengwa kilometa kama tatu hivi mashariki ya mji mdogo wa Kabuku ambao umo pembezoni mwa barabara kuu
inayounganisha njia za panda za Segera na Chalinze. Hapo mwanzoni Kabuku ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Potwe. Mapadre
toka parokiani Potwe walikuwa wanasafiri kufika Kabuku na vijiji vilivyozunguka Kabuku kutoa huduma za kichungaji.
Historia ya uwepo wa u-Katoliki katika nchi ya Kabuku inakwenda nyuma kwenye miaka ya 1965. Muda ule idadi ya wa-Katoliki ilikuwa
ndogo sana. Kwa kuwa hakukuwa na jengo la kanisa katika kijiji cha Kabuku, mapadre waliofika hapo kwa huduma za kichungaji
waliadhimisha liturjia chini ya mti. Kwa kuwa mapadre waliotoka Potwe hawakuweza kuwa na maskani yao katika Kabuku kwa wakati
huo, makatekista wananchi walifanya kazi kubwa ya uinjilishaji katika sehemu hii. Historia inawakumbuka sana makatekista Peter
Kimara na Peter Mivakuo ambao walifanya kazi kubwa ya kuisimika imani Katoliki katika sehemu hii.
Shule ya kwanza ya msingi ilijengwa katika nchi ya Kabuku katika mwaka wa 1967 kutoa huduma ya elimu kwa watoto wa wakazi wa maeneo
haya ambao walikuwa wakiongezeka. Uwepo wa shule hii uliweza kutoa nafasi ya wak-Katoliki wa maeneo haya kufanyia ibada zao kwenye
moja ya madarasa ya shule hii. Wakati Hale ilipotangazwa kuwa parokia inayojitegemea, kigango cha Kabuku kilihamia Parokia ya Hale
na kuhudumiwa na mapadre toka parokiani hapo.
Katika mwaka 1974 chini ya uongozi wa mheshimiwa padre Ignatius Safari, kanisa dogo la muda lilijengwa Kabuku. Kukamilika kwa ujenzi
wa kanisa hili dogo, liliifanya jumuia ya ki-Katoliki katika Kabuku kuwa na nyumba yao maalumu ya ibada.
Mpanuko wa wakazi katika nchi ya Kabuku na majirani zake yalisukuma uwepo wa parokia inayojitegemea katika maeneo hayo. Katika mwaka
1986 Mhashamu Baba Askofu Maurus Komba alimtuma mheshimiwa padre Nazzareno Natale, I.C. kuiandaa Kabuku kuwa parokia inayojitegemea.
Kwa msaada mkubwa wa wafadhili kutoka katika nchi yake ya asili ya Italia, baba Nazzareno aliweza kujenga majengo kadha ya kadha
hapo Kabuku ikiwa ni kanisa la kudumu, nyumba ya mapadre, nyumba ya masista na baadaye shule ya sekondari ambayo aliikabidhi kwa
serikali kwa uendeshaji wake. Kadhalika aliweza kushiriki kikamilifu katika mradi wa maji ya bomba kwa ajili ya matumizi ya parokia
na vijiji vya jirani ya parokia. Mhashamu Baba Askofu Telesphor Mkude aliweza kulibariki kanisa la Kabuku katika mwaka wa 1992
lilipokamilika na kuitangaza Kabuku kuwa parokia inayojitegemea.