PAROKIA YA FAMILIYA TAKATIFU YESU, MARIA NA YOSEFU
KWEDIBOMA TANGA
DEKANIA YA HANDENI
Parokia ya Familiya Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu (1950) RATIBA YA IBADA: |
Familiya Takatifu Grotto la Bikira Maria |
Ndani ya kanisa Kwediboma | |
Eneo la kanisa | |
Altare ya kanisa la Kwediboma | |
Nyumba ya mapadre | |
Shamba jipya la migomba |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Kwediboma ipo ndani ya wilaya mpya ya Kilindi. Parokia ipo umbali wa kilometa 70 kusini-magharibi ya mji wa Handeni
pembezoni mwa barabara kuu inayounganisha miji ya Handeni na mikoa ya Arusha na Dodoma.
Hapo awali Kwediboma ilikuwa ni moja ya vigango vya Parokia ya Mhonda katika jimbo la Morogoro. Parokia ya Mhonda ni moja ya
parokia zilizoanzishwa na mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu waliosafiri wakitokea kwenye makao yao kule Bagamoyo. Wamisionari
hawa waliweza kufika Kwediboma kwa huduma za kichungaji mara mbili kwa mwaka kutokana na umbali kati ya Mhonda na Kwediboma
(kama kilometa 250).
Kwediboma haikuwa tu mbali na Mhonda lakini pia wenyeji wa maeneo hayo ambao ni wa-Zigua wengi wao walikuwa ni madhehebu ya
ki-Isilamu. Upungufu wa ujio wa huduma za kichungaji katika nchi ya Kwediboma ulisitisha mpanuko au kukua kwa imani ya ki-Katoliki
katika maeneo haya.
Ilikuwa baadaye sana ambapo wamisionari wa ki-Rosmini walifika katika Kwediboma na kuanza kujenga parokia. Katika mwaka 1950
mheshimiwa padre Eugen Arthurs, I.C. ambaye baadaye alikuwa askofu wa kwanza wa jimbo la Tanga akiwa na mheshimiwa padre Francis
Kennedy, I.C. walifika Kwediboma na kufanya utafiti yakinifu wa kuanzisha parokia katika maeneo haya. Baada ya kupata majibu ya
utafiti wao, waliona kwamba inawezekana kujenga parokia na mara walianza kujenga nyumba ya muda ya kuwawezesha kuishi mapadre.
Baadaye uongozi wa shirika la ki-Rosmini liliwatuma waheshimiwa mapadre Daniel McCaul, I.C. na Michael Reen, I.C. kuwa mapadre
wa kwanza wakazi wa parokia hii. Baada ya muda mfupi wa kuishi kwao pale, mapadre hawa waliweza kujenga nyumba ya kudumu kwa
ajili ya mapadre. Jumuia hii ya mapadre ilipaswa kurudi kuishi kwenye nyumba yao ya asili hapo parokiani baada ya kupata ujio
wa masista wa ki-Rosmini ambao walitumwa kufanya uchungaji hapo parokiani. Jumuia ya mapadre iliwapatia masista nyumba yao ili
waishi.
Katika historia ya parokia ya Kwediboma masista wa ki-Rosmini wamefanya kazi kubwa ya kichungaji toka siku zao wa awali kufika
hapo. Mara moja baada ya ujio wao, masista hawa walianzisha zahanati kwa ajili ya huduma za afya kwa wananchi wa hapa haswa kwa
wamama wajawazito na watoto. Watu wa Kwediboma walipaswa kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 70 kufika Handeni mjini kupata
huduma hii ya afya. Wenyeji wengi wa maeneo haya ambao ni wa-Isilamu walifurahishwa mno na zawadi ya zahanati ambayo masista hawa
waliileta katika nchi yao. Kingine ambacho kiliwafurahisha mno ilikuwa ni ari na uaminifu mkubwa wa masista hawa katika uboreshaji
wa afya za wananchi wa mahali hapa na vitongoji jirani. Hali hiyo iliwafanya wananchi wengi wa maeneo haya kuupenda U-Kristu na
kuwafanya wenyeji wengi kuupokea u-Kristu katika maisha yako. Wenyeji wengi wa muda mrefu katika nchi ya Kwediboma wanawakumbuka
na kuzikumbuka kazi njema za kitume zilizofanywa na masista Laura, Vianney, Getrude na Francis ambao walijitoa mno kwa wagonjwa.
Pamoja na masista hawa pia orodha nyingine ya masista ni akina sista Silvestra, Teresia, Rita Mektilde, Olimpia Alberta, Marisia,
Emma, Renata na Juditha.
Katika mwaka 1956 mapadre wa-Rosmini walijenga shule ya bweni ya kati parokiani Kwediboma. Shule hii iliweza kutoa elimu ya juu ya
kati kwa vijana wengi wakiume waliomaliza masomo ya shule za msingi za chini. Uhaba wa shule za ngazi hii ndani ya Kwediboma na
hata sehemu nyingine jimboni na hata nje ya jimbo ulidunisha maendeleo ya elimu ya msingi kwa wavulana wengi wenye uwezo. Wengi
wao waliishia safari yao ya elimu katika ngazi za chini za elimu ya msingi. Ufunguzi wa shule hii hapo Kwediboma ulikuwa ni
ukombozi mkubwa kwa vijana wengi wa kiume na familia zao. Kwa kupata elimu ya ngazi hii ya kati, vijana wengi waliweza kuendelea
na masomo yao ya sekondari. Vijana wengi waliofika kusoma shule ya kati ya bweni ya Kwediboma walifika hapo wakitokea sehemu
mbalimbali nchini kama vile maparokia mengine jimboni hadi nchi ya Kilimanjaro. Shule hii ilikuwa ni kitivo chema cha elimu bora
na pia chombo bora cha uinjilishaji ndani na nje ya jimbo. Mapadre wenyeji wa Tanga waliobahatika kupata elimu katika shule hii
ni akina Martin Maganga and Severine Msemwa. Utaifishaji wa mashule wa mwaka 1969 uliiondoa shule hii toka mikononi mwa uongozi
wa kanisa Katoliki na kuifanya shule ya serikali.
Rutuba katika nchi ya Kwediboma imeleta mwamko mkubwa katika shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali na hivi kuwa kivutio cha
wahamiaji wengi toka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Tanga. Watu wengi wahamiaji wamefika katika nchi ya Kwediboma na
vitongoji vyake kulima na kufuga wakitokea maeneo ya Lushoto, Arusha, Moshi, Same na Morogoro. Wahamiaji wengi waliofika hapa
kutoka nchi ya Kilimanjaro walikuwa ni wa-Katoliki wenye mizizi mirefu ya imani ya ki-Kristu. Uwepo wao hapa umeleta chachu kubwa
ya maisha ya ki-Kristu.
Hadi hivi sasa padre mzawa toka parokia hii ni: Paul Maulidi Shirima (2011).