PAROKIA YA BIKIRA MARIA MSHINDI
KILOLE TANGA
DEKANIA YA KOROGWE
Parokia ya Bikira Maria Mshindi (1937) RATIBA YA IBADA: |
Bikira Maria Mshindi Makaburi ya mapadre wa jimbo |
Kanisa la Kilole |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Kilole ilianzishwa katika miaka ya 1936. Hii ni moja ya parokia nne za awali katika jimbo iliyoanzishwa na mapadre wa
shirika la Roho Mtakatifu. Parokia hii ipo katika mji wa Korogwe hatua chache pembezoni mwa barabara kuu inayounganisha miji ya
Tanga, Moshi na Handeni. Wakati mapadre wa shirika la Roho Mtakatifu walipoondoka maeneo ya Tanga mheshimiwa padre Benedikti
Forsyth, I.C. alitumwa kuwa paroko wa kwanza m-Rosmini wa parokia hii hapo mwaka 1948. Eneo la parokia hii kama vile ilivyokuwa
kwa maeneo ya parokia zote za awali, lilikuwa ni kubwa mno. Wakati mmoja parokia ilikuwa na zaidi ya vigango 50 ambavyo vingi kati
ya hivyo vilikuwa ndani ya mashamba ya mkonge na chai yaliyotawanyika katika nchi za Mswaha, Magoma, Mashewa, Kwashemshi, Dindira,
Magunga Cheke, Kwagunda, hadi Ambangulu na Dindira.
Mapadre waki-Rosmini waliihudumia parokia hii hadi katika mwaka1976 walipoikabishi parokia hii kwa jimbo. Katika mwaka huo Baba
askofu alimtuma mheshimiwa padre Odillo Mtoi katika parokia hii kuwa padre mkazi na paroko wa kwanza mwanajimbo.
Kutokana na ukubwa wa parokia hii ya Kilole na pia kutokana na ongezeko la wakazi katika maeneo haya, parokia kadha wa kadha
ziliendelea kuzaliwa kutoka parokia hii. Parokia hizo ni Potwe, Magoma, na kwa hivi karibuni Manundu.
Masista kutoka shirika la masista wa Mama Yetu wa Usambara wamekuwa wakihudumia katika parokia ya Kilole kwa muda mrefu. Kazi zao
za kichungaji parokiani hapo zimechachusha maisha ya imani kwa wananchi wa parokia hii. Katika parokia hii masista wetu wameweza
kufundisha chekechea, kuongoza mafundisho ya dini parokiani na katika shule za msingi za karibu, na pia kuwa na uchungaji wa uwepo
wao na maisha yako ya kiimani.
Katika miaka ya karibuni, uongozi wa jimbo umeiteua parokia ya Kilole kuwa moja ya vituo vya hija jimboni Tanga. Pia jimbo limeteua
parokia ya Kilole kuwa ni sehemu maalumu ya makaburi ya mapadre wa Jimbo la Tanga.
Parokia ya Kilole imo katika changamoto kubwa la kuweza kuwa na jengo kubwa la kanisa kuweza kukidhi kuongezeka kwa watu na waumini
katika eneo hili. Jengo hilo kubwa na jipya pia litaweza kujibu hadhi ya parokia hii kuwa parokia iliyo katikati ya jimbo na sehemu
ambayo matukio mengi ya kijimbo hufanyika. Jengo la kanisa la hivi sasa lilijengwa mwaka 1937 na kwa kweli ni dogo na mara nyingi
katika matukio mengi ya kiparokia na ya kijimbo yanawaacha waumini wengi nje.
Tangu kipindi cha uongozi wa parokia cha mheshimiwa padre Casmir Magwiza 2002 – 2008, juhudi za kujenga kanisa hili jipya zilianza.
Katika kipindi hicho kiwanja kilipatikana ndani ya eneo la parokia, ramani ya jengo ilipatikana, na pia ujenzi ulianza kwa uchimbaji
wa msingi wa jengo na pia kuanza kuweka msingi. Kutokana na sababu zilizojitokeza wakati huo, ujenzi huo ulisimama.
Katika kipindi hiki cha uongozi wa parokia wa mheshimiwa padre Joseph Sekija (toka 2008 hadi hivi sasa 2013), harakati zimeanza
tena kuwahamasisha wana parokia waliopo na marafiki wa parokia hii kuweza kuendelea na zoezi la ujengaji wa jengo jipya. Kukamilika
kwa jengo hili kutasaidia mno katika kukidhi mahitaji ya wanaparokia na pia mahitaji ya shughuli za jimbo katika parokia hii iliyo
katikati ya jimbo na pia parokia iliyoteuliwa kufanya shughuli nyingi za ngazi ya jimbo.
Mapadre wazawa wa Parokia hii ya Kilole ni: Msgr Severine Msemwa (1975), Severine Yagaza (1986),
Nemes Kiama (1999), na Gerard Kaberega (2000).