PAROKIA YA MT. YOSEFU MUME WA BIKIRA MARIA
MAGOMA TANGA
DEKANIA YA KOROGWE


Parokia ya Mt. Yosefu mume wa Bikira Maria (1976)
S.L.P 598, Magoma, Korogwe, Tanga
Tanzania

RATIBA YA IBADA:
JUMAPILI:
Misa: saa 01:00 Asubuhi.

SIKU ZA JUMA;
Jumatatu hadi Jumamosi saa 12:30 Asubuhi

Mapadre:
Pd. Donatus Kingazi: Paroko


Mt. Yosefu mume wa Bikira Maria
somo wa Parokia.
Sherehe yake ni kila
Tarehe 19 Machi


Nyumba ya mapadre

HISTORIA YA PAROKIA
Magoma kwa asilia ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Kilole, Korogwe. Parokia hii ipo chini ya milima ya Usambara ya kati pembezoni mwa kambi ya shamba la mkonge la Magoma. Mapadre toka Kilole walifika Magoma kutoa huduma za kichungaji kwa waumini walio katika eneo hilo na maeneo jirani ya Makumba, Mashewa, Kulasi, na Kerenge. Wengi wa waaumini waliokuwa katika sehemu hizi walikuwa ni waajiriwa katika mashamba hayo ya mikonge ambao walitokea mikoa ya magharibi na kusini mwa Tanzania. Kutokana na umbali kutoka Kilole hadi Magoma na vitongoji jirani na pia kutokana na ukubwa wa parokia hii, mapadre walitembelea maeneo haya mara moja au mara mbili tu katika mwezi. Kwa hali hii kazi kubwa ya uinjilishaji ilibakia ndani ya mikono ya makatekista ambao waliongoza ibadi za Dominika bila padre na pia kutembelea wagonjwa na kuongoza katika ibada za mazishi ya wa-Katoliki.
Katika mwaka 1976 mheshimiwa padre Nazzareno Natale, I.C. alitumwa Magoma kuanzisha parokia inayojitegemea katika Magoma. Lengo la uanzishaji wa parokia hii ulikuwa ni kuipunguza parokia ya Kilole na pia kuongeza chachu ya huduma za kanisa katika ukanda huu ulio mbali na makao makuu ya parokia. Akishirikiana na uongozi wa shamba la mkonge la Magoma pamoja na waumini wa maeneo hayo, padre Nazzareno aliweza kupata eneo kubwa la nchi kuweza kujenga parokia. Katika mwaka huo huo, padre Nazzareno alianza ujenzi wa parokia. Katika eneo hilo aliwea kujenga kanisa kubwa la kudumu, nyumba ya mapadre, nyumba ya masista, na shule ya watoto wadogo. Baada ya kukamilisha kazi hii kubwa ya ujenzi wa parokia, padre Nazzareno aliikabidhi parokia ya Magoma kwa askofu wa jimbo ambaye alimtuma mheshimiwa padre Zakaria Kayanza kuwa paroko na padre mkazi wa kwanza mzalendo kuwa hapo parokiani.
Pamoja na kuwepo kwa nyumba ya masista na shule ya chekechea parokiani hapo, hadi hivi sasa parokia haijapata kuwa na utume wa masista wakazi.
Katika siku za awali za uwepo wa parokia hii, waumini wengi wa eneo hili walikuwa wakiishi ndani ya kambi ya mkonge iliyo jirani. Kutokana na kudidimia kwa biashara ya zao la mkonge, wakazi wengi waliokuwa wakifanya kazi katika shamba hili waliondoka na kuifanya kambi hii kuwa tupu. Hivi sasa waumini wengi wanaofika kuabudu kwenye kanisa la parokia inabidi watembee umbali mrefu toka makao makuu ya mji wa Magoma ambayo yapo katika kitongoji cha Makangara.
Mabadiliko haya ya makazi ya watu yamemsukuma mheshimiwa padre Severine Msigiti paroko wa parokia hiyo kwa muda huu kuwa katika harakati za kuihamisha parokia hiyo kutoka ilipo sasa na kwenda Makangara.
Katika mwaka 2011 padre Msigiti aliweza kupata kiwanja kikubwa cha ujenzi wa makao haya ya parokia pembezoni mwa kitongoji cha Makangara ndani ya shamba la Mkonge la Magoma na tayari ameanza ujenzi wa jengo la Kanisa.