PAROKIA YA MT. AGUSTINO WA HIPO
MANUNDU TANGA
DEKANIA YA KOROGWE
Parokia ya Mt. Agustino wa Hipo (1991) RATIBA YA IBADA: |
Mt. Agustino wa Hipo Nyumba ya mapadre |
|
HISTORIA YA PAROKIA
Historia ya mji wa Manundu imetokea katika eneo la mashamba ya wenyeji wa ki-Nyamwezi na ki-Sukumu toka mikoa ya bara ambao
waliyatumia maeneo haya kwa kilimo cha viazi vitamu. Tokea siku za ukoloni mji wa Korogwe na makao makuu ya wilaya ya Korogwe
yalikuwa katika kitongoji cha Old Korogwe ambako kulikuwa na stesheni mashuhuri ya garimoshi, maduka, soko kubwa, na ofisi za
serikali.
Makuzi ya idadi ya watu na mabadiliko ya kisiasa basi yaliuhamisha polepole mji wa Old Korogwe na kuanza mji mpya wa “New Korogwe”
au Manundu. Katika miaka ya mwanzoni mwa 1970 mji wa Manundu ulikuwa mdogo sana. Baadaye makao ya serikali ya wilaya yalipohamia
Manundu basi wananchi wengi walivutwa kuanza kujenga makazi yako katika sehemu hii ya Korogwe.
Pamoja na kukua kwa makazi ya watu katika mji mpya wa Manundu, bado wakazi wa-Katoliki wa mji huu pamoja na wakazi wa mji Old
Korogwe waliendelea kutembea kwenda kupata huduma za kanisa katika makao makuu ya Parokia ya Kilole. Idadi ya wa-Katoliki
ilivyozidi ongezeka katika mji huu wa Manundu uliualika uongozi wa Parokia ya Kilole kufikiri tofauti jinsi ya kutoa huduma zake
za kichungaji. Uongozi huo ulianza kutekeleza mkakati huu kwa kuanzisha kigango kipya cha Manundu. Katika siku za awali za kigango
hiki, ibada za misa zilikuwa zinasomwa kwenye darasa la Shule ya Msingi Boma. Idadi ya wahudhuriaji ilipoongezeka, uongozi wa Chuo
cha Elimu ya Taifa Korogwe ulitoa bwalo lake la chakula kutumika siku za Jumapili asubuhi kwa madhehemu ya Misa. Idadi wa waumini
waliohudhuria ibada za misa katika bwalo hili ilizidi kuwa kubwa. Waumini hawa walikuwa ni wanachuo na wafanyakazi wa chuo hicho
cha ualimu pamoja na waumini wengi toka vitongoji vya Manundu, Magunga Hospitali, Kwasemangube, Mtonga, Mto wa Mbu na Kwamkole.
Katika mwendo wa miaka 1980 kati, mheshimiwa padre Sammuel Itatiro (R.I.P) aliyekuwa paroko wa Parokia ya Kilole wakati huo
akishirikiana na waumini wa Manundu na uongozi wa serikali ya wilaya ya Korogwe aliweza kupata eneo kubwa la kujenga parokia mpya
ya Manundu. Wazo hili lilipokelewa kwa furaha na waumini wa Manundu. Ni katika miisho ya miaka ya 1980 ambapo ufadhili wa kujenga
parokia ya Manundu ulipatikana chini ya uongozi wa mheshimiwa padre Athanas Meixner, OSB. Ujenzi wa jengo la Parokia ya Manundu
ulianza mwaka 1989 na ulikamilika vyema mwezi Mei 1990.
Misa Takatifu ya kwanza katika jengo hili jipya ilisomwa siku ya Mei 27, 1990. Waumini wengi wa kigango hiki cha Manundu walijawa
cherekochereko na shukurani kwa Mungu katika tukio hili na walilijaza jengo hili la kanisa. Baba askofu alimteua mheshimiwa padre
Fraternus Mbuya kuwa paroko wa kwanza wa parokia hii mpya wakati wa kutabarukiwa jengo hili la kanisa siku ya Novemba 10, 1996.
Jengo na parokia hii viliwekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Augustino wa Hippo.
Japo Parokia ya Manundu iliundwa na kuwa na paroko wake padre Mbuya, bado parokia ilikuwa haina nyumba ya padre. Paroko wa kwanza
wa parokia hii aliendelea kuishi kwenye parokia mama ya Kilole. Paroko wa pili wa parokia hii mheshimiwa padre James Kweka (R.I.P)
alifika hapo parokiani na kuanza kuishi kwenye jengo dogo la pembeni ambalo lilitumika wakati wa ujenzi wa kanisa kama kambi ya
wajenzi na pia sehemu ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi. Ni katika kipindi cha uongozi wa mheshimiwa padre Silas Singano ambapo
nyumba rasmi ya mapadre ilijengwa.
Katika kipindi cha uongozi wa padre Kweka, jengo la shule ya chekechea lilijengwa japo matumizi yake hadi hivi sasa siyo mazuri
mno kutokana na jengo hilo kuwa katika eneo pweke na uwanja mbaya wa mporomoko.