PAROKIA YA BIKIRA MARIA MAMA WA MATESO
MAZINDE NGUA TANGA
DEKANIA YA KOROGWE
Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mateso (1951) RATIBA YA IBADA: |
Bikira Maria wa mateso Nyumba ya Mapadre |
Eneo la Parokia |
HISTORIA YA PAROKIA
Hapo awali Mazinde ilikuwa ni kigango cha parokia ya Kilole. Mapadre toka Parokia ya Kilole walifika hadi Mazinde kutoa huduma
za kichungaji. Baadaye Mazinde ilifanywa kuwa kigango cha Parokia ya Gare. Parokia ya Mazinde ipo chini ya milima ya Usambara
magharibi umbali wa kilometa mbili kaskazini mwa barabara kuu inayounganisha miji ya Korogwe na Moshi. Parokia hii ipo umbali
wa kilometa 15 magharibi ya mji wa Mombo.
Mheshimiwa padre Francis Hubsch alijenga kanisa la mwanzo katika sehemu hii ya Mazinde katika mwaka wa 1923. Kanisa hili lilikuwa
dogo sana lakini lilitosho idadi ndogo ya waumini waliokuwepo wakati huo. Baadaye katika miaka ya 1938-39 lilijengwa kanisa kubwa
ambalo lilitabarukiwa katika mwaka wa 1940.
Baadaye mheshimiwa padre Dick Foley, I.C. alijenga nyumba kubwa ya mapadre. Mapadre wengi wamisionari wa wakati huo walikuwa
wakisafiri kati ya miji ya Arusha, Moshi, Tanga na Dar-es-salaam waliweza kupiga kambi hapo kwa mapumziko.
Idadi kubwa ya waumini wa ki-Katoliki katika Parokia ya Mazinde ni ya wenyeji wa milima ya Usambara. Familia nyingi zinazoishi
hapa zina mizizi katika sehemu mbalimbali za wilaya ya Lushoto. Aina nyingine ya waumini wa-Kikatoliki ni ya watu kutoka mikoa
ya bara ambao walifika Mazinde kufanya kazi kwenye mashamba ya mikonge. Vingango vingi vya Parokia hii vimo katika kambi za mashamba
ya mikonge au vijiji vilivyoanzishwa na waliokuwa wakazi wa mashamba hayo baada ya zao hilo kupoteza umaarufu wake katika soko la
dunia.
Mazinde ilifanywa kuwa parokia inayojitegemea katika mwaka wa 1951. Uwepo wa masista wetu wa Shirika la Mama Yetu wa Usambara
(COLU) umekuwepo parokiani Mazinde kwa muda mrefu na hivi kuleta chachu njema ya maisha ya ki-Kristu kwa wananchi wa Mazinde.
Tume za masista hawa zipo katika kumshuhudia Kristu kwa maisha yako ya kitawa, na pia katika kufundisha mafundisho ya dini na
pia katika ufundishaji kwenye mashule ya msingi ya Mazinde-Ngua na pia katika huduma ya tiba katika kituo cha afya parokiani hapo.
Parokia hii ambayo ilikuwa ikipata huduma za kichungaji kutoka kwa mapadre wa ki-Rosmini toka kuasisiwa kwake, ilikabidhiwa kwa
askofu wa jimbo katika miaka ya 1980 na tokea hapo askofu amekuwa akiwatuma mapadre wazalendo wa jimbo kutoa huduma za kichungaji.
Parokia ya Mazinde imekuwa na baraka ya mito mingi ya kipadre na kitawa kwa akina mama. Wapo masista wengi katika shirika la Mama
Yetu wa Usambara waliotokea katika parokia ya Mazinde.
Mapadre wazawa toka Parokia ya Mazinde ni: John Kika Zuakuu (1987), Paul Semkuya (1991),
Passian Salimu Kika (1994) na Askofu Thomas Kiangio (1997).