PAROKIA YA YESU KRISTO MFALME
POTWE TANGA
DEKANIA YA KOROGWE
Parokia ya Yesu Kristo Mfalme (1953) RATIBA YA IBADA: |
Yesu Kristo Mfalme Nyumba ya Mapadre |
Ndani ya kanisa siku ya kipaimara | |
Waamini wanapokea ugeni |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Potwe ipo ndani ya milima ya Usambara ya kati ikiwa ni kama kilometa 10 hivi kaskazini mwa barabara kuu ya
Tanga-Korogwe. Kuelekea Parokia ya Potwe ipo barabara ndogo inayotokea kijiji cha Maguzoni kwenda huko. Hapo awali
parokia hii ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Mlingano lakini baadaye ikawekwa kuwa chini ya Parokia ya Kilole. Mapadre
waliokuwa wakihudumia Parokia ya Kilole walisafiri kwa garimoshi toka Korogwe hadi kituo cha garamoshi cha Mnyuzi na toka
hapo kituoni basi walitembea kwa miguu hadi Potwe.
Kanisa la Potwe lilijengwa kwa kutumia nguvu za waumini wa hapo wakishirikiana na mapadri wao. Waheshimiwa mapadri wamisionari
Bredan Bonnelly I.C., Ted Cronin, I.C., Jackie Reid, I.C. Dick Downing, I.C. na Mhashamu Askofu Eugen Arthurs, I.C. walichangia
sana uanzishwaji wa parokia hii katika mwaka wa 1953. Mheshimiwa padre Sean Madden, I.C. alianza harakati za ujenzi wa nyumba ya
mapadre kabla ya kuanza ujenzi wa kanisa.
Kwa kuwa Potwe na sehemu nyingi zinazozunguka Potwe katika mashamba ya mikonge kulikuwa na waajiriwa wengi waliotokea katika mikoa
ya kusini mwa Tanzania, kulimsukuma mhashamu askofu Eugene kuomba msaada wa mapadre wamisionari toka majimbo ya kusini mwa Tanzania
ambao walifahamu mila na desturi ya wafanyakazi hao. Ombi pekee lilipelekwa kwa askofu wa Jimbo la Songea ambaye kwa ukarimu wake
aliwatuma waheshimiwa mapadre Eligius Kapinga na Bernard Ndunguru kuja kufanya kazi Jimbo la Tanga katika parokia ya Potwe.
Parokia ya Potwe imekuwa ni parokia ya kihistoria na ya mfano bora wa muunganiko wa kazi za kitume zilizofanywa katika mseto wa
kitume kati ya mapadre wananchi na mapadre wamisionari. Mifano michache inathibitisha hili kwani padre Bernard Ndunguru alifanya
utume na padre Tom Hubbart, I.C. Padre Denis Sweeney, I.C. alifanya kazi na padre Odilo Mtoi na mapadre Benedict Forsight, I.C.
na Ignas Safari walifanya kazi pamoja.
Mapadre waliofanya kazi katika Parokia ya Potwe waliweza kupata msaada wa fedha katika miradi kadha wa kadha ya maendeleo ya
wananchi. Miradi hiyo ni ile ya maji safi kwa wananchi wa Potwe na mradi wa kuvuta umeme wa TANESCO kuifikia parokia na pia
kutawanywa kwa wananchi. Kadhalika miradi mingine ni ile ya ujenzi wa shule ya msingi na kituo cha afya.
Padre mzawa wa Parokia ya Potwe ni: Peter Amandrus Mapunda (2003) (R.I.P.).