PAROKIA YA BIKIRA MARIA MPALIZWA MBINGUNI NA MT. BERNARD
GARE TANGA
DEKANIA YA LUSHOTO
Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni na Mt. Bernard (1897) RATIBA YA IBADA: Utaratibu wa wiki ya Hija kijimbo |
Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Mt. Bernard Clairvaux |
Maujaji katika ibada kituo cha hija Gare | |
kituo cha hija Gare |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Gare ipo ndani ya milima ya Usambara katika wilaya ya Lushoto. Parokia hii ilinzishwa na wamonaki waki-Trapisti kutoka Abasia ya Natali,
Afrika Kusini katika mwaka wa 1897. Wamisionari hawa walifanya utume wao sehemu hii ya Gare kwa ushirikiano wa karibu na masista wa shirika la Damu
Takatifu waliokuwepo hapo. Katika mwaka 1906 wamonaki hawa waliondoka Gare kurudi Afrika Kusini. Mara baada ya ma-Trapisti kuondoka Gare, wamisionari
wa Shirika la Roho Mtakatifu toka Kilimanjaro walifika Gare na kuanza kufanya kazi za kichungaji wakashirikiana na masista wa shirika la Damu Takatifu.
Utume wa masista wa shirika la Damu Takatifu uliendelea kwenye Parokia ya Gare hadi mwaka 1987 walipoondoka parokiani hapo na kufuatiwa na masista wa
shirika la Mama Yetu wa Usambara (COLU).
Utume wa mapadre wa Roho Mtakatifu katika nchi ya Gare ulioanza mwaka 1906 ulimalizika katika mwaka 1948 walipoondoka na kuwakabidhi utume watawa wa
ki-Rosmini. Mapadre wakwanza wa ki-Rosmini waliofanya utume Parokia ya Gare ni waheshimiwa mapadre Benedict Forsyth, I.C., Dick Downing, I.C. na Arthur
Rafferty, I.C. Katika mwaka 1950 mheshimiwa padre Francis Kennedy, I.C. alifika parokiani hapo na kufanywa kuwa paroko wa parokia hiyo nafasi ambayo
aliishikilia kwa miaka 40 mfululizo hadi kifo chake siku ya Aprili 26, 1995 akiwa na umri wa maika 81. Kifo cha padre huyu kilitokea siku ambayo
wanashirika wa ki-Rosmini walikuwa katika jumuiko la sherehe za miaka 50 ya kazi ya kitume katika Jimbo la Tanga.
Padre Kennedy ni mmoja wa mapadre waki-Rosmini aliyejitoa kwa hali na mali kupanda mbegu ya Injili katika nchi ya Gare. Katika hiki kipindi kirefu cha
uongozi wake katika parokia hii, padre Kennedy alinzisha miradi mingi ya maendeleo ikiwa ni ile ya ujenzi wa shule ya msingi ya kati ya Gare, kanisa
kubwa na zuri ambalo linaing’arisha Parokia ya Gare, kituo cha afya Gare, ukumbi mkubwa wa Mama Yetu, na uboreshaji wa nyumba na huduma za masista
katika nyumba ya masista wa COLU Kongei. Alifanya kazi kwa bidii kuanzisha chuo cha makatekista kule Kwai kuweza kutoa elimu bora ya dini kwa
makatekista wa jimbo na familia zao. Kadhalika alishiriki kwa karibu sana katika ujenzi wa kanisa katika shule ya Mtakatifu Mikaeli Soni ambayo baadaye
ilikuwa seminari ndogo ya jimbo ya Mtakatifu Yosefu.
Utume wa kanisa katika Parokia ya Gare unajionyesha katika maisha ya ki-Kristu ya wananchi wa Gare. Uinjilishaji wa Gare umezaa matunda mengi ya
miito mitakatifu kwa wasichana waliojiunga na tawa mbalimbali za masista na pia vijana wengi walioitikia mwito wa kuwa mapadre.
Hadi kufikia mwezi Augusti 1997 wakati Parokia ya Gare ilipokuwa inasherehekea miaka 100 ya uinjilishaji katika parokia hiyo, kulikuwa na idadi ya
wa-Katoliki 5,086 katika ya watu 21,083 wanaoishi katika maeneo haya.
Kutokana na mizizi ya muda mrefu ya historia ya uinjilishaji katika Parokia ya Gare, uongozi wa Jimbo la Tanga umeiteua Parokia ya Gare kuwa ni
kituo kikubwa cha hija jimboni Tanga. Mara moja kwa mwaka katika mwezi wa Oktoba familia yote ya Jimbo la Tanga inafanya hija ya siku moja parokiani
hapa kuendelea kuizamisha mizizi ya Injili ndani ya roho za wanajimbo wote.
Mapadre wazawa kutoka Parokia ya Gare ni; Odillo Mtoi (1960) (R.I.P.), George Mhuza (1979),
John Chambi (1982) (R.I.P.), Peter Rodoussakis (1982) (R.I.P.),
Romani Shemkai (1982), Askofu Titus Mdoe (1986), Thomas Msagati (1991),
Thadeus Mkambwa (1997), Casmir Mahimbo (1997), Martin Kihiyo (1997).