PAROKIA YA EKARISTI TAKATIFU
LUSHOTO TANGA
DEKANIA YA LUSHOTO


Parokia ya Ekaristi Takatifu (1950)
S.L.P. 26, Lushoto, Tanga
Tanzania

RATIBA YA IBADA:
JUMAPILI:
Misa 1: saa 01:30 Asubuhi.
Misa 2: saa 03:30 Asubuhi.

SIKU ZA JUMA;
Jumatatu hadi Jumamosi saa 12:30 Asubuhi
Alhamisi saa 10:30 jioni Kuabudu

Mapadre:
Pd. Tarimo Firmati: Paroko
Pd. Potentinus Mutekanga: Paroko Msaidizi


Ekaristi Takatifu
somo wa Parokia.
Sherehe yake ni kila
Alhamisi baada ya Jumapili ya Utatu Mtakatifu

Shule ya awali parokiani Lushoto

HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Lushoto ipo ndani ya mji wa Lushoto, mji ulio katikati ya milima ya Usambara magharibi. Katika mwaka wa 1950 ambapo Vatikani iliitangaza Tanga kuwa Prefekture inayojitegemea toka kwenye Vikariate ya Kilimanjaro, uongozi wa kanisa la Tanga ulifikiria kuiandaa Lushoto kuwa makao makuu ya Jimbo la Tanga. Kwa mawazo haya, uongozi ulitafuta sehemu ya kujenga makao haya na uliweza kupata eneo ambalo Parokia ya Lushoto imo hivi sasa. Eneo hili lilimilikiwa na mfanya biashara mmoja mgeni aliyekuwa ana biashara ya mgahawa/hoteli. Uongozi wa Tanga uliweza kulinunua eneo hili na mara kuanza kujenga kanisa lenye hadhi ya kiaskofu. Mheshimiwa padre Benedict, I.C. na bruda Fortunatus, O.S.B walishirikiana kujenga jengo hili la kanisa. Jengo hili lilikuwa kubwa na zuri na hadi hivi leo linaupendezesha mji wa Lushoto. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo hili la kanisa, wahashamu maaskofu Eugene Arthurs, I.C. na Edgar Aristide Marantha, O.F.M.Cap., askofu wa Jimbo la Dar-Es-Salaam walishiriki kulitabaruku kanisa hili. Kujengwa na kutabarukiwa kwa kanisa hili la Lushoto kulileta chachu kubwa ya uinjilishaji katika nchi hii ya Lushoto na katika maeneo yote ya milima ya Usambara magharibi.
Katika mwaka 1953 Shirika la Masista wa Damu Takatifu lilihamishia hospitali yake ya meno toka katika kijiji cha Kifungilo kuja mjini Lushoto. Huko Kifungilo masista walishakuwa na hospitali hiyo pamoja na shule ya watoto yatima machotara. Ujio wa hospitali hii ya meno Lushoto uliongeza ubora wa mji wa Lushoto na pia ubora wa kazi ya uinjilishaji. Watu wengi waliopata huduma ya meno toka kwa masista wahudumu wa hospitali hii waliweza kuuona mkono wa Kristu katika maisha yao. Hospitali hii ya meno imeweza kuendelea kutoa ubora mkubwa wa huduma zake chini ya uongozi wa sr. Eileen, C.P.S. na kuwa na mvuto wa wateja wengi toka ngazi zote za watu katika nchi nzima ya Tanzania.
Mradi wa kuifanya Lushoto kuwa makao makuu ya Jimbo Katoliki la Tanga uliyeyukia hewani wakati uongozi wa jimbo ulipotakiwa kujenga makao yake makuu ya jimbo kurandana na makao makuu ya mkoa wa Tanga. Kwa mwendo huu, makao makuu ya Jimbo yalipelekwa kuwa katika eneo la Parokia ya Mtakatifu Antoni Chumbageni mjiniTanga.
Mapadre wa shirika la Rosmini walieendelea kuhudumia parokia ya Lushoto hadi mwaka 1976 walipoikabidhi parokia hii kwa askofu wa jimbo. Katika mwaka huo baba askofu alimtuma mheshimiwa padre Vitus Nkondora kuwa paroko wa kwanza mwanajimbo kuiongoza parokia hiyo.
Parokia ya Lushoto imekuwa ikizungukwa na maendeleo yote ya kukua kwa mji wa Lushoto na vitongoji vyake. Ndani ya parokia ya Lushoto zipo nyumba za masista wa Damu Takatifu na Mama Yetu wa Usambara. Pia zipo shule kadhaa za elimu ya awali, msingi, na sekondari. Ipo shule ya kimataifa, shule ya watoto yatima ya Upendo na chuo cha maarifa ya nyumbani cha Upendo vinavyoongozwa na masista wa Damu Takatifu. Hapo Lushoto kipo chuo cha ualimu cha Motessori kinachoongozwa na masista wa COLU, chuo cha sheria, na nyumba za malezi za mashirika ya Mapendo na Roho Mtakatifu.
Hivi sasa Parokia ya Lushoto ina Hosteli ya Mtakatifu Benedikti na pia shule ya chekechea. Katika miaka ya karibuni, baba askofu ameirudisha Parokia ya Lushoto kuhudumiwa na mapadre wa Kirosmini ambao pia wanasaidia kutoa huduma za kichungaji katika chuo cha ualimu cha Montesori.

Mapadre wazawa wa kutoka Parokia ya Lushoto ni: Francis Gembe (1981) (R.I.P.), Silas Singano (1986), Edwin Kimwemwe (1991), Maximilian Mahonge (1997), na Benedikti Shemfumbwa (2000).