PAROKIA YA MOYO MT. WA YESU
RANGWI TANGA
DEKANIA YA LUSHOTO
Parokia ya Moyo Mt. wa Yesu (1953) RATIBA YA IBADA: |
Moyo Mt. wa Yesu Nyumba ya Mapadre |
|
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Rangwi ipo katika milima ya Usambara magharibi umbali wa kilometa 45 toka mji wa Lushoto. Parokia hii imo kandokando ya barabara itokayo
Lushoto kuelekea mji wa Mtae. Parokia hii imeanzishwa chini ya uwepo wa nyumba kuu ya awali ya shirika la masista wa Mama Yetu wa Usambara (COLU)
ambayo imeambatana na nyumba ya wanovisi ya shirika hilo. Mapadre walezi wa masista hawa walikuwa wakarimu wa kutoa huduma za kichungaji kwa wanavijiji
wa-Katoliki wa Rangwi ambao wengi wao walifika kupata huduma hizo katika kanisa la masista. Mapadre Jackie Reid, I.C. na Dick Walter, I.C.
wanakumbukwa kwa karibu na waumini wa kale wa Rangwi kwa bidii yako ya kuchunga roho zao. Uwepo wa nyumba ya masista katika kijiji cha Rangwi
umekuwa ni chachu kubwa ya makuzi ya imani Katoliki katika nchi nzima ya Rangwi na vitongoji vyake.
Inazungumzwa kwamba hata kabla ya masista kuanza nyumba yao Rangwi baadaye, mheshimwa padre Francis Hubsch, I.C. aliweza kujenga kikanisa kidogo katika
nchi ya Malindi katika mwaka 1937 kwa ajili ya jumuia ya wa-Katoliki katika maeneo hayo. Inawezekana kwamba padre Hubsch alifika katika nchi ya Malindi
akitokea Gare kupitia Kwai na pia kuweza kuijongelea Rangwi.
Jinsi muda ulivyopita, idadi ya waumini wa-Katoliki katika Rangwi na vitongoji vyake iliongezeka. Hali hii iliashiria hitajiko kubwa la uanzishaji wa
parokia inayojitegemea kuliko kuendelea kutegemea huduma za mapadre walezi wa masista. Hatua za awali za utekelezaji wa wazo la parokia lilikuwa ni
kujenga nyumba ya mapadre pembezoni mwa eneo la masista. Baada ya mradi huu kukamilika, mradi wa ujenzi wa kanisa ulianza mara moja chini ya uongozi
wa mheshimiwa padre Jack O’Kane, I.C. ambayealiweza kuukamilisha mwaka 1953. Kukamilika kwa ujenzi wa kanisa, uliashiria kutangazwa kuzaliwa kwa parokia
ya Rangwi.
Mapadre wamisionari wa ki-Rosmini wamekuwa wakihudumia parokia hii na vigango vyake tangu kuzaliwa kwake hadi mwaka 1992 walipoikabidhi parokia hii
kwa askofu wa jimbo. Muda huo baba askofu aliyemtuma padre mwananchi, mheshimiwa padre Ernesti Seng’enge kuwa paroko wa kwanza mwananchi wa Parokia
ya Rangwi.
Chachu ya uinjilishaji wa masista katika nchi ya Rangwi na vitongoji vyake imejionyesha sana katika matunda mengi na mazuri ya miito mitakatifu toka
parokiani hapo. Wasichana wengi toka sehemu ya Rangwi wameweza kuvutwa na maisha ya kitawa katika shirika la COLU. Baadhi ya wasichana hawa ni masista
wetu akina Luka, Ernesta, Miriam, Angelika, Benedikti, na Gaspara.
Mapadre wazalendo wazawa wa parokia hii ni: Joseph Kikoti (1996), Elias Maivaji (1997),
Joseph Sekija (1997) na Paulo Semng’indo (2007).