PAROKIA YA MT. YOSEFU MFANYAKAZI
SAKHARANI TANGA
DEKANIA YA LUSHOTO
Parokia ya Mt. Yosefu Mfanyakazi (1976) RATIBA YA IBADA: |
Mt. Yosefu Mfanyakazi Nyumba ya Padre |
Nyumba ya masista |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Sakharani ipo ndani ya milima ya Usambara kilometa chache toka mji mdogo wa Soni kandokando ya barabara itokayo mji wa Soni kwenda mji
mdogo wa Bumbuli. Parokia ya Sakarani ina mizizi ya kina kutokana na uwepo wa wamonaki wa ki-Benediktini waliokuja katika nchi ya Sakharani kutoka
Abasia ya ki-Benedikitini ya Ndanda katika Jimbo la Mtwara katika mwaka 1946. Abasia ya Ndanda ilinunua shamba hili la la Sakharani kwa lengo la kuwa
na nyumba ndogo ya mapumziko ya watawa wake kulikimbia joto la nchi ya Ndanda. Baada ya ununuzi wa shamba hili, abate wa Ndanda aliwatuma mapadre na
mabruda kuja kuishi na kufanya kazi ndani ya shamba hili. Kwa miaka, watawa hawa hawakujishughulisha na shughuli za kichungaji za maeneo haya.
Waliofanya shughuli za kichungaji katika eneo hili walikuwa ni mapadre waki-Rosmini toka Parokia ya Gare. Wamonaki wa shamba la Sakharani waliendelea
na utume wao wa kutoa ukarimu kwa watawa wenzao waliowatembelea hapo kwa mapumziko ya mwili na roho. Shughuli zao kubwa zikiwa ni kilimo, ufugaji wa
wanyama, uwashi, na useremala.
Katika mwaka 1970, mheshimiwa padre Burkard Schneider, O.S.B. ambaye alikuwa ni mmoja wa viongozi wa nyumba ya Sakharani aliomba toka uongozi wa shirika
lake pamoja na uongozi wa Jimbo la Tanga aweze kujishughulisha na shughuli za kichungaji. Uongozi wa Abasia ya Ndanda na uongozi wa Jimbo la Tanga chini
ya mhashamu askofu Maurus Komba ulimruhusu padre Burkard kufanya uchungaji katika maeneo yaliyozunguka Sakharani. Padre Burkard aliaza kufanya uchungaji
katika vijiji vya Masange na vijiji vingine vinavyolizunguka shamba la Sakharani. Baadaye mheshimiwa padre Edwin Frank, O.S.B. toka shamba la Sakharani
alivutiwa pia kufanya shughuli za kichungaji. Naye pia aliruhusiwa kufanya hivyo na kuweza kumuunga mkono padre Burkard.
Utume wa mapadre Burkard na Edwin katika nchi hii ya Sakharani ulichachusha mwamko wa Injili na kuifanya jumuia ya ki-Katoliki kukua kwa kasi. Kukua
kwa idadi ya wa-Katoliki iliwasukuma mapadre Burkard na Edwin kujihusisha kujenga majengo ya parokia. Mapadre Burkard na Edwin waliomba toka uongozi
wa abasia Ndanda eneo la kujenga parokia katika shamba la Sakharani. Abate wa Ndanda aliwapatia mapadre hawa heka kadhaa pembeni mwa shamba la Sakharani
waweze kujenga parokia ya Sakharani. Wingi wa zao la mbao ndani ya shamba la Sakharani na pia uwepo wa mabruda wa-Benediktini kwenye shamba hilo wenye
utaalamu wa majengo, vilichangia ubora wa ujenzi wa haraka wa parokia hii. Majengo yote yaliyojengwa katika parokia hii muda wa mwanzo yalikuwa ni ya
mbao zilizotoka katika shamba la Sakharani. Mapadre hawa walijenga jengo la kanisa, nyumba mbili za mapadre, nyumba ya masista, nyumba ya wageni wa
parokia, shule ya chekechea na nyumba ya kuhifadhia mizigo ya parokia. Ujenzi wa parokia hii ulikamilika na parokia ilifunguliwa kwa kutabarukiwa
kanisa la parokia katika mwaka 1976.
Mapadre Burkard na Edwin waliendelea kuinjilisha nchi ya Sakharani na vitongoji vyake. Mapadre hawa walifahamika kama mitume wa nchi ya Sakharani na
vitongoji vyake siyo tu kwa waumini wa madhehebu ya ki-Katoliki lakini pia wa wa-Islamu na wa-Luteri wa maeneo haya. Kwa juhudi zao waliweza kujenga
makanisa ya kudumu na nyumba za wahumu katika vigango vyote vya parokia hii ikiwa ni vigango vya Baga, Kwesine, Kwehangala, Tekwa, Msamaka, and Nkelei.
Mapadre Burkard na Edwin hawakufungua tu vigango vya matofali na mchanga, waliweza kupanda upendo wa ki-Mungu ndani ya roho za watu wa sehemu hizo.
Parokia ya Sakharani imekuwa ni udongo mzuri wa miito mitakatifu. Wasichana wengi toka parokia hii wamejiunga na maisha ya kitawa katika shirika la
masista wetu wa Mama Yetu wa Usambara.
Mapadre wazawa kutoka Parokia ya Sakharani ni: Msgr Ernest Seng’enge (1981) (R.I.P.), Anthony Mtungunja (1991),
Placidus Mtunguja, O.S.B. (2001) (R.I.P.), Clement Kihiyo Jandu (2008) na Valentine Kaniki, O.S.B (2011).