PAROKIA YA MT. MARTIN WA TOURS
SONI TANGA
DEKANIA YA LUSHOTO


Parokia ya Mt. Martin wa Tours (1989)
S.L.P. 140, Soni, Lushoto, Tanga
Tanzania

RATIBA YA IBADA:
JUMAPILI:
Misa: saa 02:30 Asubuhi.

SIKU ZA JUMA;
Jumatatu hadi Jumamosi saa 01:00 Asubuhi

Mapadre:
Pd. Prosper Ndwewe: Paroko


Mt. Martin wa Tours
somo wa Parokia.
Sherehe yake ni kila
Tarehe 11 Novemba

parokia_chumbageni4

Nyumba ya Mapadre
Parokiani Soni

Screenshot

Nyumba ya Masista

HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Soni ipo pembezoni mwa mji wa Soni uliopo katikati ya milima ya Usambara. Mji wa Soni upo katikati ya barabara inayounganisha miji ya Mombo, Lushoto na mji mdogo wa Bumbuli.
Historia ya Parokia ya Soni ni ndefu kidogo. Mapadre wamisionari wa ki-Rosmini tokea miaka ya nyuma ya 1960 wamekuwa wakiwahudumia wa-Katoliki wa maeneo ya Soni ambao wengi wao walikuwa wakiishi maeneo ya vijiji vya Shashui. Kutokana na idadi hiyo ya waumini katika maeneo haya, wamisionari wa Parokia ya Gare walijenga jengo dogo la kanisa la kingango cha Shashui. Wa-Katoliki waliokuwa wanaishi vijiji vya Soni na majirani ilibidi kutembea kwenda Shashui kupata huduma za kichungaji. Japo kulikuwa na mapadre wa ki-Rosmini katika shule ya bweni ya wavulana wa Kizungu katika kitongoji cha Mawezi/Shashui, mapadre hao hawakujishughulisha na shughuli za kichungaji kwa wananchi wa sehemu. Hivi shughuli zote za kichungaji zililala ndani ya uongozi wa Parokia ya Gare.
Katika miaka ya mwanzoni mwa 1970, wa-Rosmini walipoifunga shule ya bweni ya Mtakatifu Mikaeli. Baada ya kufungwa shule hiyo, wa-Rosmini waliyakabidhi majengo hayo kwa askofu wa jimbo la Tanga. Askofu alimtuma mheshimiwa padre Gerald Chilambo (R.I.P) kufungua seminari ndogo ya jimbo katika 1975. Seminari ndogo ilianzishwa katika majengo hayo ya shule ya Mtakatifu Mikaeli katika mwaka 1976. Baba askofu aliwatuma mapadre wengine kuwa walezi wa waseminari. Mheshimiwa padre Francis Kennedy, I.C. paroko ya Parokia ya Gare aliwaomba mapadre wa seminarini wasaidie kutoa huduma za kichungaji kwenye kigango cha Shashui na ujirani wake. Japo mapadre wa seminarini walitoa huduma za kichungaji kigangoni Shashui, utawala wa kigango hicho ulibakia ndani ya uongozi wa Parokia ya Gare.
Katika miaka ya 1987 idadi ya wa-Katoliki iliongezeka katika vitongoji vya Shashui na mji wa Soni. Mwaka huo mheshimiwa padre Athanas Meixner, O.S.B. toka Abasia ya wa-Benediktini wa Ndanda alifika jimboni Tanga akiwa na nia ya kufanya shughuli za kichungaji. Baba askofu alimpokea padre Athanas na kumruhusu kufanya uchungaji katika maeneo ya Soni. Baada ya kupata kibali hicho, padre Athanas alitafuta eneo la kujenga makao ya Parokia ya Soni. Baadaye padre Athanas aliweza kununua eneo la kujenga makao ya Parokia ya Soni toka kwa mwenyeji mmoja aliyekuwa na eneo lake la kuuza. Baada ya kupata eneo hilo, padre Athanas alianza ujenzi wa kanisa la awali na pia kuendelea na kujenga majengo mengine kama vile nyumba ya mapadre, nyumba ya masista, nyumba za wafanyakazi, ghala, na nyumba ya zahanati ndogo. Ilipofika mwaka 1989 padre Athanas alikamilisha ujenzi wa kanisa kubwa la parokia na mhashamu baba askofu Telesphor Mkude alifika kulitabaruku na kumtaja Mtakatifu Martini wa Tours kuwa msimamizi wa parokia hiyo.
Kutabarukiwa kwa kanisa la Soni kuliitangaza Soni kuwa parokia inayojitegemea toka Parokia ya Gare na Shashui ikabakia kuwa ni kigango kikuu cha Parokia ya Soni. Padre Athanas alitajwa kuwa paroko wa Parokia ya Soni na tangu mwanzo wa utawala wake amepata ushirikiano wa karibu wa kichungaji kutoka kwa mapadre wanaofundisha katika seminari ndogo ya Soni ambao wanasaidiana naye katika kazi za kichungaji parokiani na vigangoni. Parokia ya Soni imekuwa ni mchango mkubwa wa kutoka kwenye Abasia ya Ndanda kwa Jimbo la Tanga.
Hamasa ya uchungaji ya padre Athanas imekuwa haikubaki kwenye upande wa maisha ya kiroho ya waumini wa madhehebu ya ki-Katoliki tu. Hamasa yake ilipanuka pia katika maendeleo ya maisha ya kiuchumi ya maisha ya watu wote wa Soni. Tokea padre Athanas afike katika jamii ya wana Soni amejishirikisha sana katika kuboresha maisha ya wananchi katika ngazi mbalimbali. Upenzi wake wa kilimo umekuwa changamoto kubwa katika ukulima wa zao la kahawa na pia amependa sana kujishirikisha katika miradi ya maji safi na kuleta ubora wa afya za watu kwa kuanzisha zahanati parokiani hapo. Ari ya shughuli za kiamaendeleo toka kwa padre Athanas imegusa vigango vyote ambavyo vimo ndani ya parokia ya Soni na hata sehemu nyingine jimboni.

Padre mzawa toka Parokia ya Soni ni: Severine Msigiti (2008).