PAROKIA YA MT. YOSEFU MUTESA
AMBONI TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Mtakatifu Yosefu Mutesa Ndani ya kanisa la |
Eneo la Parokia ya Amboni | |
Mbele ya kanisa |
a). Mahali Ilipo Parokia
Parokia ya Amboni imo ndani ya jiji la Tanga katika kitongoji cha Amboni ambacho kipo upande wa kaskazini wa jiji hili. Kuna umbali wa kilometa kumi hivi
tokea katikati ya jiji hadi kuifikia parokia hii. Parokia imejengwa kandokando ya barabara kuu inayounganisha jiji la Tanga na mpaka wa Tanzania na Kenya
kuelekea jiji la Mombasa.
b). Asili ya Amboni
Kitongoji cha Amboni kwa asili yake ilikuwa ni kambi ya shamba la mkonge na baadaye kitongoji hicho kilipanuka sana wakati kiwanda cha
plastiki kilipojengwa hapo kitongojini katika miaka ya awali mwa 1970. Hivi wenyeji wa kitongoji hiki wengi wao walikuwa ni waajiriwa katika shamba hili la
mkonge na katika kiwanda hiki cha plastiki. Sehemu kubwa ya waajiriwa hawa ilikuwa ni watu kutoka mikoa ya bara. Wenyeji asilia wa Amboni na vitongoji vya
mwambao wa Tanga ni wa kabila la ki-Digo ambao wamekuwa wakijishughulisha na ukulima mdogomdogo na biashara za mazao ya baharini. Wengi wa wenyeji wa maeneo
haya wamekuwa ni wa-Islamu wenye historia ndefu ya u-Isilamu na mila za Mashariki ya kati.
c). Asili ya Parokia
Kwa asili Parokia ya Amboni imekuwa toka katika ngazi ya kigango cha parokia ya Mtakatifu Antoni Kathedra iliyopo kitongoji cha Chumbageni jijini Tanga. Kanisa
la awali la kigango cha Amboni lilikuwa ni jengo dogo ndani ya kambi ya mkonge ya Amboni ambalo lilijengwa na utawala wa shamba hilo kwa kuwahudumia waajiriwa
wake waweze kupata sehemu ya kuabudu. Kujengwa kwa kiwanda cha maplastiki cha Amboni katika miaka ya kati mwa 1970, kuliongeza idadi ya watu na hata wa-Katoliki
katika maeneo ya Amboni na hivi kulifanya jengo la kanisa kuwa dogo. Ongezeko hili la watu na la wa-Katoliki katika nchi ya Amboni lilitoa changamoto kubwa kwa
uongozi wa Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga wa kutafuta mbinu za kuweza kutoa huduma bora za kichungaji kwa waumini wa maeneo haya.
d). Maendeleo ya Baadaye
Mheshimiwa padre Gerard Smith (R.I.P) aliyekuwa paroko wa Parokia ya Mtakatifu Antoni kwa wakati huo aliona hitajiko hilo. Hivi katika miaka ya mwishoni mwa 1970 na
mwanzoni mwa 1980, padre Smith (R.I.P) alijitahidi kuomba kiwanja cha ujenzi wa kanisa jipya kutoka kwenye uongozi wa shamba la mkonge la Amboni. Ombi hilo lilikubaliwa
na katika kipindi hicho na mara moja ujenzi wa kanisa la Amboni ulianza. Pamoja na ujenzi huu wa jengo la kanisa, padre Smith (R.I.P) alijenga nyumba ya katekista mkazi
na pia alijenga ukumbi mkubwa wa mikutano na shughuli mbalimbali za kichungaji hapo kigangoni. Ujenzi huu ulikamilika haraka na hivi waumini wa kigango cha Amboni
kuanza kusalia katika kanisa jipya. Kanisa jipya lilibarikiwa na mhashamu baba askofu Maurus Komba (R.I.P) aliyeliweka kanisa hilo chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu
Mukasa. Historia ya kigango cha Amboni haitamsahau katekista mkazi wa kigango hiki mwalimu Shitundu ambaye alifanya kazi kubwa ya kupanda Injili katika maeneo
haya.
e). Safari ya Kuwa Parokia
Amboni iliendelea kuwa ni kigango cha Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga hadi miaka ya mwisho ya 2000 wakati Mhashamu baba askofu Anthony Banzi (R.I.P) alipokitangaza kigango
hicho kuwa parokia tarajiwa. Katika tamko hilo, baba askofu alimtuma mheshimiwa padre Francis Gembe (R.I.P) kuwa padre mkazi wa parokia hii tarajiwa. Katika kipindi hiki
idadi ya waumini wa parokia tarajiwa iliongezeka sana na hapo Julai 5, 2011 baba askofu aliipa parokia tarajiwa ya Amboni kuwa parokia kamili inayojitegemea na
akamteua mheshimiwapadre Odillo Shedafa kuwa paroko wa kwanza wa parokia hii mpya.
f). Changamoto la Parokia
Pamoja na miradi mingi ya kuiboresha parokia hii, padre Odillo Shedafa alianza mchakato wa kujenga nyumba ya mapadre wakati huo yeye akiishi katika chumba kidogo
ndani ya jengo la ukumbi wa parokia ambamo kuna chumba kimoja cha kuishi padre. Baada ya yeye kuondoka padre Roman Shekumkai alishika nafasi yake kama Paroko, lakini
hata yeye akuendelea na wazo la ujenzi wa nyumba ya padre. Padre Anthony Mtunguja ameshika nafasi ya paroko na amejitahidi kubadilisha nyumba ilikuwa inatumiwa na
katekista mwanzoni kuifanya iwe nyumba ya mapadre ikiwa na ofisi na huduma nyingine ndani yake. Nyumba ina vyumba kadhaa vya kuweza kuishi mapadre na hata kupokea mgeni.