PAROKIA YA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
MARAMBA TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili
|
Parokia ya Maramba imejengwa chini ya milima ya Usambara mashariki kandokando ya barabara ndogo ichepukayo toka barabara kuu ya Tanga - Mombasa kwenye kijiji cha
Mabokweni na kuelekea mji wa Korogwe kupitia Daluni, Mashewa na Magoma. Hapo awali Parokia ya Maramba ilianza kuwa kigango cha Parokia ya Mtakatifu Antoni wa Padua
iliyopo jijini Tanga. Eneo la Maramba na vijiji vya jirani yake ni maeneo ya mashamba makubwa ya mazao ya kokoa na mkonge. Wananchi wa asili wanayo mashamba yao
binafsi wanayolima mazao ya chakula. Mashamba makubwa ya kokoa yanaweza kuonekana katika vitongoji vya Maramba na Mwele wakati mashamba ya makubwa ya mkonge yapo
katika vitongoji vya Lugongo na Kwamtili.
Mapadre wamisionari wa ki-Rosmini toka Parokia ya Mtakatifu Antoni Kathedra Tanga wamekuwa wakifika maeneo ya Maramba kwa huduma za kichungaji hata kabla ya miaka
ya 1970. Inasemekana kwamba wakati mapadre hawa walipokuwa wakifika sehemu za Maramba kwa huduma za kichungaji, waliweza kupata ukarimu wa kujihifadhi kwenye nyumba
ya meneja wa shamba la mkonge la Lugongo.Walipofika Maramba kwa misa na uchungaji, walivitembelea vijiji vya Lugongo na Mwele vilivyokuwa na ukulima wa mkonge kwa
huduma za misa. Uongozi wa mashamba ya mkonge ya Lugongo na Mwele waliweza kujenga vikanisa vidogo katika kambi za
watumishi wa mashamba hayo kuwawezesha wafanya kazi wao kupata sehemu ya kuabudu.
Katika miaka ya awali ya 1970, mheshimiwa padre Moris Reen, I.C. aliweza kupata eneo la kujenga kanisa katika kitongoji cha Maramba. Alianza ujenzi huo mara moja.
Mara baada ya kukamilisha ujenzi wa kanisa, padre Reen alijenga nyumba ya padre. Inasemwa kwamba katika harakati za ujenzi wa kanisa la Maramba, waumini wa Maramba
na vitongoji vyake walihamasika mno. Pamoja na kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa kanisa, waliweza kuchanga juml ya shilingi 12,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa
itakayokuwa parokia yao. Ujenzi wa kanisa la Maramba na nyumba ya mapadre ulikamilika 1972 ambapo Mhashamu Baba Askofu Maurus Komba alifika kulibariki kanisa hili.
Katika mwaka 1970, Mhashamu Askofu Maurus Komba, askofu wa pili wa jimbo la Tanga alifanya ibada ya misa kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa mara ya kwanza jimboni
katika kitongoji cha Maramba. Kwa kuwa hakukuwa na jengo la kanisa, ibada hiyo iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka katika vitongoji mbalimbali vya Maramba
ilifanyika nje. Wale waliohudhuria ibada hii walikuwa siyo wa-Katoliki tu, bali pia wa-Kristu wa madhehebu mengine na hata wa-Islamu.
Mapadre wazawa wa Parokia ya Maramba ni: Msgr. Martin Maganga (1972) (R.I.P), Sylvester Nitunga (1999),
Diomedi Nitunga I.C. (2005), na Odillo Shedafa (2006).