PAROKIA YA BIKIRA MARIA MALKIA WA MBINGUNI
MLINGANO TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Bikira Maria Malkia wa Mbinguni Nyumba ya mapadre |
Chuo cha Ukatekista Mlingano |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Mlingano imejengwa kilometa kama tano hivi kaskazini barabara kuu inayoinganisha jiji la Tanga na miji ya Muheza na Korogwe.
Kwenda parokiani hapa unachepukia katika kijiji cha Mkanyageni na kuchukua barabara ndogo inapitia kwenye vijiji vya MATI Mlingano,
Mzambarauni, na Vanga.
Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu toka Kilimanjaro walianzisha parokia hii katika mwaka wa 1902. Parokia hii ni moja ya parokia nne za
awali katika eneo la Tanga ambazo zilianzishwa na mapadre hawa wakati eneo la Tanga lilipokuwa chini ya Vikariate ya Kilimanjaro. Wakati
wa Vita Kuu ya II Parokia ya Mlingano ilibakia bila ya huduma ya mapadre. Katika mwaka wa 1950 parokia hii na parokia nyingine tatu za awali
zilikabidhiwa kutoka mapadre wa Roho Mtakatifu kwenda kwa mapadre waki-Rosmini. Waheshimiwa mapadre Edmund Spillane, I.C. na James Murphy,
I.C. walikuwa mapadre wa kwanza wa ki-Rosmini kufanya shughuli za kichungaji parokiani hapa. Baadaye mheshimiwa padre Michael Reen, I.C na
Jackie Reid walitumwa kufanya kazi hapa na kuwa kundi la pili la wahudumu. Timu hii ya pili ilianza kujenga kanisa jipya. Bahati mbaya
ililikumba kundi hili la pili la wahudumu wakati padre Reen alipopata ajali mbaya ya kuangukiwa na mti wakati akiwa katika harakati za
ujenzi wa shule ya msingi. Ajali hii ilimbakiza padre Reen kuwa mlemavu hadi alipofariki dunia mwaka 1979.
Katika mwaka 1964 kundi lingine la mapadre wa ki-Rosmini kutoka Italia lilifika parokiani hapa. Kundi hili lilikuwa ni la waheshimiwa mapadre
Orest Radaeli, I.C. na Luigi Cerana, I.C. Kwa pamoja walifanya shughuli za kichungaji katika maeneo ya Mlingano na vitongoji vingi
vilivyoizunguka parokia. Pia timu hii ya mapadre ilijenga nyumba nzuri ya mapadre ambayo bado inatumika hadi hivi leo. Mapadre wengine
wamisionari walifanya kazi katika parokia hii ya Mlingano ni Benedict Forsyth, I.C., Sean Madden, I.C. Jack O’Kane, I.C. Freddie Callanan,
I.C. Andy Grant, I.C. Nazzareno Natale, I.C., Denis Sweeney, I.C na Donald Sullivan, I.C.
Japo parokia hii imejengwa katika kijiji cha Mlingano, mapadre wa parokiani hapo wamekuwa na kazi kubwa ya uinjilishaji katika makambi mengi
ya mkonge yanayozunguka parokia hii. Katika upande wa mashariki mwa parokia, mapadre walikwenda kuhudumia vigango vya Azimio, Ngomeni, Umba,
hadi Kumburu. Kwa upande wa kusini walikwenda hadi Mkanyageni. Kuelekea kaskazini walifika kwenye vigango vya Kibaranga, Mjesani hadi kupakana
na Maramba. Kwa upande wa magharibi, mapadre walihudumia vigango vya Mlingote, Kicheba, hadi chini ya milima ya Amani.
Katika mwaka 1977 mapadre waki-Rosmini waliikabidhi parokia hii kwa askofu wa jimbo na hapa baba askofu alimtuma mheshimiwa padre Gerald
Chilambo kuwa paroko wa kwanza mwanajimbo.
Mapadre wazawa wa parokia hii ya Mlingano ni: Leopold Nyandwi (1987), Thadeus Ponera (1990) (R.I.P),
Ados Majeta, C.P. na Alex Masangu (2005).