PAROKIA YA MT. FRANCIS XAVIER
MTINDIRO MUHEZA TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Mtakatifu Francis Xavier Nyumba ya mapadre |
Ndani ya kanisa la Parokia Mtindiro |
HISTORIA YA PAROKIA
Mtindiro ni kijiji maarufu kwa ukulima wa machungwa ambacho kipo kilometa kadhaa kusini ya mji wa Muheza katika barabara ndogo ya mkato
inayounganisha miji ya Muheza na Pangani kupitia Boza. Mtindiro kwa muda mrefu ilikuwa ni kigango maarufu cha Parokia ya Muheza. Mapadre
waliofika kigangoni hapo na vigango vingine jirani walitokea parokiani Muheza.
Wananchi wengi wa kijiji hiki cha Mtindiro na vijiji vya jirani ni wa-Bondei. Pia kutokana na ubora wa ardhi ya nchi ya Mtindiro, wananchi
wengi wa kutoka katika mikoa ya bara ambao wengi wao walikuwa wakifanya kazi katika mashamba ya mikonge, waliishia kuhamia katika kijiji na
vijiji jirani kuwa wakulima. Hivi uwepo Mtindoro na maeneo yanayozunguka ni rahisi kukutana na watu wengi wenye asili ya mikoa ya Ruvuma,
Iringa, Njombe, Mbeya, na hata Kigoma na Morogoro.
Kigango cha Mtindiro kimekuwa na msisimko mkubwa wa maisha ya kiimani na pia maendeleo kutokana na mchanganyiko wa wauumini wake toka sehemu
mbalimbali za Tanzania. Pia wana-Mtindiro wamekuwa mbele sana katika kuboresha ubora wa kigango chao. Kwa muda mrefu wamekuwa na kanisa zuri
kuweza kukidhi mahitaji yao ya kuabudu.
Katika miaka ya 2006, Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi alimpa ruhusu mheshimiwa padre Nazzareno Natale, I.C. kuweza kuiinua Mtindiro toka
ngazi ya kigango kwenda kuwa parokia inayojitegemea. Padre Nazzareno alifika kigangoni hapo na kupata uwanja mkubwa wa kujenga parokia hii
mpya. Alijenga kanisa jipya kubwa kukidhi idadi ya waumini wa sasa. Pamoja na jengo la kanisa, padre Nazzareno alijenga nyumba ya mapadre.
Mara baada ya kamilika ujenzi huu, baba askofu alifika kulitabaruku kanisa hili na kuyabariki majengo ya haya na pia kuweza kuitangaza
Mtindiro kuwa parokia mpya inayojitegemea. Katika mwaka 2011 padre Nazzareno aliikabidhi parokia hii kwa jimbo na baba askofu alimteua
mheshimiwa padre Elias Maivaji kuwa paroko mwanajimbo wa kwanza kuiongoza parokia hii mpya.
Padre mzawa kutoka Parokia ya Mtindiro ni: Bernard Chissi (1994)(R.I.P.-2011)