PAROKIA YA KRISTO MFUFUKA
MUHEZA TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Kristo Mfufuka Nyumba ya mapadre zamani |
Eneo la Parokia ya Muheza |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia ya Muheza ni parokia pekee iliyo katika mji wa Muheza. Parokia hii ipo kilomita 35 magharibi ya jiji la Tanga kandokando ya barabara
kuu itokayo Tanga kwenda Korogwe. Kabla ya kuanzishwa parokia hii, Muheza ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Mlingano.
Katika mwaka 1969 Mhashamu askofu Arthurs, IC akisaidiwa na mheshimiwa padre Jack Reid, I.C., walijenga kanisa katika eneo hili. Pia walijenga
nyumba ndogo ya kuishi mapadre. Ni baadaye tu ndipo mheshimiwa padre Tom Coffey, I.C. aliweza kujenga nyumba kubwa na ya kudumu ya mapadre.
Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa nyumba ya mapadre, mapadre wa-Rosmini waliikabidhi parokia hii kwa askofu wa jimbo ambaye alimteua mheshimiwa
padre Vincent Ushaki kuwa paroko wa kwanza mwanajimbo.
Katika kipindi cha hivi karibuni, jumuia mbili za masista zimefika katika mji wa Muheza kuishi. Masista wa ki-Rosmini wamejenga nyumba yao
ya wanovisi na masista wa shirika la Mama Yetu wa Usambara wamejenga makao yao madogo pamoja na kituo cha afya. Uwepo wa jumuia hizi mbili
za masista katika nchi ya Muheza umeongeza chachu ya uinjilishaji katika eneo hili. Mapadre toka parokiani Muheza wanajihusisha kwa karibu
katika maisha ya kichungaji katika jumuia hizi mbili.
Mwisho wa Karne ya 20 na mwanzo wa Karne ya 21 kumeendelea kuwa na ongezeko la watu katika maeneo yote nchini Tanzania. Kadhalika hali hii
imejionyesha katika mji wa Muheza. Mji wa Muheza umeendelea kupanuka mno katika idada ya watu na pia katika idadi ya makazi ya watu. Hali hii
imeongeza pia idadi ya wa-Katoliki wanaoabudu katika kanisa la Parokia ya Muheza hata kulifanya jengo la kanisa lilijengwa mwaka 1969 kuwa
halikidhi mahitaji. Katika miaka ya karibuni uongozi wa Parokia ya Muheza chini ya paroko wake mheshimiwa padre Martin Kihiyo ulikaa chini
na kutathimini kile linachohitajika kufanyika kiparokia kujibu swali la udogo wa jengo la kanisa. Kwa kauli moja uamuzi ulifanyika kwamba
parokia haina budi kukubali ukweli kwamba hitajiko la jengo kubwa na la kisasa ni muhimu. Ujenzi wa jengo jipya la kanisa parokiani hapo
ulianza mwaka 2008. Kwa kuzishirikisha nguvu za waumini wa parokia yote pamoja na marafiki wa parokia ndani na nje ya parokia, ujenzi
umeendelea hatua kwa hatua kuliinua hekalu hili. Ni mategemeo kwamba kwa hatua hii ya ujenzi jengo hili litaweza kuwa tayari kutumika katika
mwaka huu wa 2013. Hadi kukamilika kwake jengo hili litakuwa na uwezo wa kuchukua watu 1000 (elfu moja). Jengo la kanisa la mwaka 1969 ambalo
linaendelea kutumia hadi sasa limekuwa lina uwezo wa kuchukua watu 150 (mia moja hamsini) na kuwafanya waumini wengi kuwa nje ya jengo wakati
wa ibada.
Waumini wa Parokia ya Muheza wamejawa nguvu na furaha tele ya kupambana na zoezi hili kabambe la ujenzi wa jengo la kanisa lao jipya na la
kisasa. Hivi sasa wamekamilisha jengo hilo kama lionekanavyo katika picha na pia kwa nguvu hiyo hiyo wamefanikiwa kujenga pia nyumba kubwa
ya mapadre, chini ya uongozi wa Pd. Martin Kihiyo mwaka wa 2024