PAROKIA YA MT. PETRO MTUME
SARUJI TANGA
DEKANIA TANGA MJINI
RATIBA YA IBADA: |
Mtakatifu Petro Mtume Kanisa la kigango cha |
Waamini baada ya misa wakisalimiana |
HISTORIA YA PAROKIA
Parokia hii iko chini ya uongozi wa Mapadre Warosmini. Wapo Masista kutoka katika Shirika la Mama Yetu wa
Usambara wanaotoa huduma katika Parikia hii.
Parokia ya Mtakatifu Petro-Saruji ipo magharibi ya jiji la Tanga umbali wa kilometa 12 hivi toka katikati ya
Tanga kandokando ya barabara kubwa inayounganisha jiji la Tanga na mji wa Muheza. Parokia hii asili yake ni
kigango mkongwe cha Parokia ya Mtakatifu Antoni Kathedra Tanga. Kanisa la awali la kigango hiki lilikuwa
katika kambi ya mkonge ya Mianzini. Uongozi wa shamba la mkonge la Pongwe ulijenga kanisa hili dogo kwa ajili
ya matumizi ya wafanyakazi wake wa madhehebu ya ki-Katoliki.
Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele idadi ya watu ilizidi kuongezeka katika vijiji vilivyoizunguka kambi. Kadhalika wakazi
walizidi kuongezeka katika mji wa Pongwe na vijiji vya jirani na kukifanya kikanisa cha Mianzini kuwa ni kidogo.
Parokia hii ina vigango vya Pongwe kijijini, Saruji penyewe, Kange, Jaribu tena, Kakindu, Kisimatui, Chote na Kilapula.
Kuna nyumba za masista katika kigango cha Saruji and Pongwe kijijini.
Parokia hii inahudumiwa na mapadre wa Rosmini
Ujio wa Kampuni ya Sementi katika mwaka 1978 uliongeza watu zaidi ambao walikuja kama waajiriwa wa kampuni hiyo na kampuni
nyinginezo zilizotoa huduma mbalimbali kwa wakazi wa kiwanda hicho. Ongezeko hili la watu ambalo pia liliongeza idadi ya
waumini wa ki-Katoliki lilileta changamoto kwa uongozi wa Parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga kuweza kutoa huduma maridhawa
za kichungaji kwa waumini wa kigango hiki cha Pongwe. Mheshimiwa padre Gerard Smith, I.C. aliyekuwa paroko wa parokia hiyo
aliwasiliana na uongozi wa kiwanda cha sementi Pongwe ili walipatie kanisa sehemu ya ardhi kujenga taasisi za kanisa Katoliki.
Uongozi wa kampuni hii ulitoa eneo la kiwanja kikubwa katika eneo ambalo parokia ya Mtakatifu Petro-Saruji ipo hivi sasa.
Mara baada ya kupata eneo hili la kiwanja, basi ujenzi wa majengo ulianza. Jengo la kwanza lilikuwa ni jengo la nyumba ya
mwalimu wa dini ambaye yeye na familia yake walianza kuishi eneo hili. Jengo la pili lilikuwa ni madarasa ya shule ya watoto
wadogo, na baadaye jengo ya kanisa, nyumba ya masista na nyumba ya mapadre yalifuatia. Jengo la kanisa lilibarikiwa na
mhashamu baba askofu wa jimbo katika mwaka 1980. Katika mwaka huo masista wanne wa Shirika la Mama Wetu wa Usambara walitumwa
kuanza kutoa huduma zao katika parokia hii.
Katika mwaka 1985, mheshimiwa padre Gerard Smith alihama toka kwenye parokia ya Mtakatifu Antoni Tanga kuja kuishi katika
nyumba ya mapadre katika kigango cha Mtakatifu Petro-Saruji. Baadaye katika mwaka 1988 kigango hiki kilipewa hadhi ya parokia
inayojitegemea na mheshimiwa padre Smith aliteuliwa kuwa paroko wa kwanza mkazi parokiani hapo. Padre Smith aliendelea
kuiboresha parokia hii ya Mt. Petro-Saruji kwa kuendelea kujenga majengo ya kudumu ya nyumba za ibada na shule za watoto
wadogo katika vigango vya parokia. Majengo mazuri ya ibada yanaweza kuonekana katika vijiji vya Chote, Kisimatui, Kange,
Kakindu, Mkembe, na Jaribu Tena. Katika mji wa Pongwe, padre Smith alipata kiwanja cha kanisa na huko alijenga jengo zuri
la kanisa lililobarikiwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Gerard. Hapo Pongwe, padre Smith aliendelea kujenga nyumba
ya masista na shule ya watoto wadogo.
Padre Gerard Smith alifariki dunia mwaka 2001. Hadi hivi sasa Parokia ya Mt. Petro-Saruji inahudumiwa na mapadre wa
shirika la Rosmini ambao pia wanamiliki na kuongoza Sekondari ya Warosmini ya Saruji.
Parokia hii ina vigango vya Pongwe kijijini, Saruji penyewe, Jaribu tena, Kakindu, Kisimatui, Chote, Mkembe na Kilapula.
Kuna nyumba za masista katika kigango cha Saruji na Pongwe kijijini.
Mapadre wazawa wa Parokia hii ya Mt. Petro-Saruji ni: Pd. John Mahundi (1986) (R.I.P),
Joseph Mbena (1987) na Richard Kimbwi (2004).