PAROKIA (TARAJIWA) YA MKALAMO

KANISA KATOLIKI JIMBO LA TANGA

 

(Angalia ukurasa huu kwa kiingereza)


Parokia tarajiwa ya Mkalamo ipo kusini magharibi ya mji wa Pangani katika kijiji cha Mkalamo ndani ya kata ya Mkalamo wilayani Pangani. Parokia hii tarajiwa ipo kandokando mwa barabara ndogo inayounganisha pwani ya Bahari ya Hindi upande wa mashariki na vijiji vya Kwamsisi na Mkata kuelekea sehemu za Handeni kwa upande wa magharibi.  Wakati usafiri wa reli ulipokuwa hai, Mkalamo ilikuwa ni kituo kidogo cha garimoshi katika reli iliyounganisha reli ya kaskazi katika stesheni ya Mnyuzi na reli ya kati katika stesheni ya Ruvu.
Hapo awali Parokia tarajiwa ya Mkalamo ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Pangani na kabla ya kuwepo kwa Parokia ya Pangani Mkalamo ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Mtakatifu Teresia Tanga. Kutokana na umbali wa kigango hiki tokea Tanga na hata tokea Pangani na pia kutokana na ugumu wa usafiri kufika maeneo haya ya kusini mashariki mwa mkoa wa Tanga, kuliwafanya mapadre toka Tanga na Pangani kukitembelea kigango hiki kwa huduma za kichungaji mara haba. Waumini wa-Katoliki katika nchi ya Mkalamo na vijiji jirani mara nyingi walihudumiwa na makatekista kwa kipindi kirefu ambacho hakukuwa na padre aliyefika.
Mhashamu baba askofu Anthony Banzi aliona umuhimu mkubwa wa kuinjilisha eneo hili la Mkalamo na hivi mwaka 2007 alimtuma mheshimiwa padre Paulo Semkuya kuanza utume huko Mkalamo kama padre mkazi na pia kukiandaa kigango hiki kuwa parokia inayojitegemea siku za usoni. Tokea muda huo padre Semkuya amekuwa katika harakati za ujenzi wa jengo la kanisa na pia jengo la nyumba ya padre.
Katika harakati za uinjilishaji katika ngazi ya jimbo katika maeneo ya Mkalamo, uongozi wa jimbo ulifanya maadhimisho ya sikukuu ya Ekaristi Takatifu kijimbo Mkalamo mwezi Juni 2012. Mapadre na waumini kadhaa waliweza kufika Mkalamo kwa maadhimisho ya sherehe hiyo iliyofanywa kwa Ibada ya Misa takatifu na baadaye kufuatiwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu. Maadhimisho haya yalikuwa ni ushahidi mkubwa wa imani Katoliki katika nchi ya Mkalamo.
Hadi hivi sasa hakuna padre yeyote mzawa kutoka katika parokia hii tarajiwa ya Mkalamo.