PAROKIA YA GARE

KANISA KATOLIKI JIMBO LA TANGA

Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni na Mtakatifu Bernard: walinzi wa parokia yetu, mtuombee!

(Angalia ukurasa huu kwa kiingereza)

Parokia inavigango vifuatavyo: Kongei, Boheloi and Kwemashai

HISTORIA YA PAROKIA

Parokia ya Gare ipo ndani ya milima ya Usambara katika wilaya ya Lushoto. Parokia hii ilinzishwa na wamonaki waki-Trapisti kutoka Abasia ya Natali, Afrika Kusini katika mwaka wa 1897. Wamisionari hawa walifanya utume wao sehemu hii ya Gare kwa ushirikiano wa karibu na masista wa shirika la Damu Takatifu waliokuwepo hapo. Katika mwaka 1906 wamonaki hawa waliondoka Gare kurudi Afrika Kusini. Mara baada ya ma-Trapisti kuondoka Gare, wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu toka Kilimanjaro walifika Gare na kuanza kufanya kazi za kichungaji wakashirikiana na masista wa shirika la Damu Takatifu. Utume wa masista wa shirika la Damu Takatifu uliendelea kwenye Parokia ya Gare hadi mwaka 1987 walipoondoka parokiani hapo na kufuatiwa na masista wa shirika la Mama Yetu wa Usambara (COLU).

Utume wa mapadre wa Roho Mtakatifu katika nchi ya Gare ulioanza mwaka 1906 ulimalizika katika mwaka 1948 walipoondoka na kuwakabidhi utume watawa wa ki-Rosmini. Mapadre wakwanza wa ki-Rosmini waliofanya utume Parokia ya Gare ni waheshimiwa mapadre Benedict Forsyth, I.C., Dick Downing, I.C. na Arthur Rafferty, I.C. Katika mwaka 1950 mheshimiwa padre Francis Kennedy, I.C. alifika parokiani hapo na kufanywa kuwa paroko wa parokia hiyo nafasi ambayo aliishikilia kwa miaka 40 mfululizo hadi kifo chake siku ya Aprili 26, 1995 akiwa na umri wa maika 81. Kifo cha padre huyu kilitokea siku ambayo wanashirika wa ki-Rosmini walikuwa katika jumuiko la sherehe za miaka 50 ya kazi ya kitume katika Jimbo la Tanga.
Padre Kennedy ni mmoja wa mapadre waki-Rosmini aliyejitoa kwa hali na mali kupanda mbegu ya Injili katika nchi ya Gare. Katika hiki kipindi kirefu cha uongozi wake katika parokia hii, padre Kennedy alinzisha miradi mingi ya maendeleo ikiwa ni ile ya ujenzi wa shule ya msingi ya kati ya Gare, kanisa kubwa na zuri ambalo linaing’arisha Parokia ya Gare, kituo cha afya Gare, ukumbi mkubwa wa Mama Yetu, na uboreshaji wa nyumba na huduma za masista katika nyumba ya masista wa COLU Kongei. Alifanya kazi kwa bidii kuanzisha chuo cha makatekista kule Kwai kuweza kutoa elimu bora ya dini kwa makatekista wa jimbo na familia zao. Kadhalika alishiriki kwa karibu sana katika ujenzi wa kanisa katika shule ya Mtakatifu Mikaeli Soni ambayo baadaye ilikuwa seminari ndogo ya jimbo ya Mtakatifu Yosefu.
Utume wa kanisa katika Parokia ya Gare unajionyesha katika maisha ya ki-Kristu ya wananchi wa Gare. Uinjilishaji wa Gare umezaa matunda mengi ya miito mitakatifu kwa wasichana waliojiunga na tawa mbalimbali za masista na pia vijana wengi walioitikia mwito wa kuwa mapadre.
Hadi kufikia mwezi Augusti 1997 wakati Parokia ya Gare ilipokuwa inasherehekea miaka 100 ya uinjilishaji katika parokia hiyo, kulikuwa na idadi ya wa-Katoliki 5,086 katika ya watu 21,083 wanaoishi katika maeneo haya.
Kutokana na mizizi ya muda mrefu ya historia ya uinjilishaji katika Parokia ya Gare, uongozi wa Jimbo la Tanga umeiteua Parokia ya Gare kuwa ni kituo kikubwa cha hija jimboni Tanga. Mara moja kwa mwaka katika mwezi wa Oktoba familia yote ya Jimbo la Tanga inafanya hija ya siku moja parokiani hapa kuendelea kuizamisha mizizi ya Injili ndani ya roho za wanajimbo wote.


Mapadre wazawa kutoka Parokia ya Gare ni; Odillo Mtoi (1960), George Mhuza (1979), John Chambi (1982), Peter Rodoussakis (1982), Romani Shemkai (1982), Titus Mdoe (1986), Thomas Msagati (1991), Thadeus Mkambwa (1997), Casmir Mahimbo (1997), Martin Kihiyo (1997), Jerome Mkamwa (2000), Donatus Kingazi (2001), Joseph Shetui (2005), Claudius Mndolwa, SCA (2005), Peter Singano (2011), na Richard Kajiru (2011).