PAROKIA YA MABUGHAI

KANISA KATOLIKI JIMBO LA TANGA

Mt. Benedikto wa Nursia, mlinzi wa parokia yetu, utuombee!

(Angalia ukurasa huu kwa kiingereza)

HISTORIA YA PAROKIA

Parokia ya Mabughai imo ndani ya milima ya Usambara umbali wa kilometa 12 hivi kutoka mjini Lushoto. Parokia hii ndani ya kijiji cha Mabughai . Kijiji cha Mabughai kimejengwa kandokando ya barabara inayounganisha miji ya Lushoto na  Mlalo au Mtae.
Hapo awali Mabughai ilikuwa ni moja ya vigango vya Parokia ya Lushoto. Mapadre toka parokiani Lushoto walifika hapo kigangoni kila Jumapili kwa madhehebu ya misa na masakramenti ya kanisa. Waumini wengi wa Mabughai wamekuwa ni wananchi wenyeji wa mazingira haya lakini pia waajiriwa wengi katika taasisi zilizonguka kigango hiki. Taasisi hizo zilikuwa chuo cha maendeleo ya akina mama Mazinde Juu (hivi sasa sekondari ya wasichana Mazinde Juu), chuo cha maendeleo ya wananchi Mabughai, sekondari ya wavulana ya Magamba (ambayo sasa ni chuo kikuu cha Askofu Sebastian Kolowa), chuo cha ufundi cha Magamba na viwanda vya mbao vilivyozunguka maeneo ya kijiji cha Magamba.
Mara kadha wa kadha mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu wenye nyumba yao ya wanovisi katika kijiji cha Magamba waliweza kushirikiana kiuchungaji katika kigango hiki. Pia mheshimiwa padre Damian Milliken, O.S.B.  ambaye alikuwa akifundisha shule ya sekondari ya Magamba katika miaka ya mwishoni mwa 1970 na mwanzoni mwa 1980 aliweza kushiriki katika shughuli za kichungaji katika kigango hiki.
Katika miaka ya mwisho ya 1980 padre Damiani alipata ruhusu toka jimboni kuweza kuanzisha shule ya ya sekondari ya Mazinde Juu  ambayo iliweza kufunguliwa rasmi mwaka 1989. Shughuli za uboreshaji na ujenzi wa sekondari ya Mazinde Juu umeenda sambamba na shughuli za uboreshaji wa jingo la kanisa la kigango cha Mabughai. Kutojana na ujirani wa shule ya sekondari ya Mazinde Juu na kigango cha Mabughai, ushirikano wa karibu wa taasisi hizo mbili ulijengeka. Siku zilivyozidi kusonga mbele idadi ya waumini ilizidi kuongezeka katika maeneo ya kijiji cha Mabughai na vijiji vya ujirani. Kutokana na ongezeko hilo jengo la asili la kanisa la kigango halikuweza kutosha kwa idadi ya waumini waliopo. Kwa ushirikiano wa waumini wa Mabughai na wafadhili toka nje, padre Damiani aliweza kufanikiwa kujenga jengo kubwa la kanisa hapo Mabughai.
Baada ya kutabarukiwa jengo hili jipya la kanisa la Mabughai, mhashamu baba askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Tanga alikiinua kigango cha Mabughai kuwa Parokia ya Mabughai na kumteua mheshimiwa padre Damian Milliken, O.S.B. kuwa paroko mwasisi wa parokia

Upendo na nia ya padre Damiani kwa ubora na maendeleo ya kielimu kwa wananchi wa Mabughai na majirani zake ni mkubwa mno. Moja ya mradi mkubwa ambao ameuanzisha parokiani ni shule ya Mtakatifu Benedikto ya ki-Ingereza. Shule hii inawasaidia vijana wa maeneo haya kuwa na uwezo wa lugha ya ki-Ingereza, hesabu, na sayansi kama sehemu ya maandalizi yao kuweza kujiunga na shule bora za sekondari nchini na pia elimu hiyo kuwasaidia kuendelea vyema katika masomo yao hayo katika shule za sekondari na katika elimu ya juu. Kutokana na maandalizi haba ya vijana hawa, mara nyingi huko nyuma wameshindwa kupata nafasi za masomo katika shule bora nchini. Shule hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa watoto na familia za maeneo haya.

Padre Damiani anaendelea kuiboresha Parokia ya Mabughai. Hivi sasa yumo katika harakati za kujenga nyumba ya mapadre na pia nyumba ya masista. Ni lengo lake kwamba baada ya kukamilisha mradi huu, basi mapadre na masista waishi hapa parokiani katika kazi ya uinjilishaji wa wana Mabughai.

Padre mzawa toka katika Parokia hii ya Mabughai ni: Augustino Mahonge (2009) ambaye ni padre wa Jimbo Kuu la Chikago, USA.