KANISA KATOLIKI TANGA

SHIRIKA LA MAPENDO:

Rosminian Fathers/Brothers

Rosmini Chaple Lushoto

Shirika la Mapendo lilianzishwa mwaka 1828 na Mwenye Heri Antonio Rosmin. Huyu alikuwa Mwana Falsafa liyejulikana sana. Mwaka 1932, nyumba ya Malezi ilianzishwa huko Ireland. Nyumba hii ikawa chachu ya Miito mingi. Mwaka 1938 Chuo kilichopewa jina la Rosmini kilifunguliwa huko Roma. Jumuia ya Warosmini ilianza kukua. Walifanya kazi huko Thailand. Mwaka 1942 walishauriwa kuelekeza utume wao Barani Afrika. Kwa kupitia Vikarieti ya Kilimanjaro chini ya Mhashamu Askofu Joseph Byrene hatimaye mwaka 1945 Warosmini wakwanza waliingia Tanganyika. Wawili kati yao ni Pd. Walter Dich na Pd. Francis Kennedy.

 

Warosmini waliofika Kilimanjaro walipewa kwanza jukumu la kufundisha Chuo cha Singachini huko Moshi. Pd Walter akawa Mkuu wa Chuo. Mapadre wengine walifuata baadaye. Mhashamu Askofu Joseph Byrne aliwatuma Warosmini wafanye kazi Tanga. Hatimaye Pd. Eugen Arthurs aliteuliwa kuwa Prefekti wa Kitume Tanga ilipokuwa Prefectura, na baadaye akawa Akofu wa Jimbo la Tanga mwaka 1958.

Makao makuu ya Shirika la Warosmini katika Afrika Mashariki yapo Mwambani hapa Tanga. Makao makuu Kiulimwengu ni Monte Calvario huko Domodossola katika kingo za Milima ya Alps kwenye mpaka kati ya Italia na Uswisi. Shirika hili limesambaa mahali pengi Duniani.

Warosmini wamefanya kazi kubwa za Kichungaji hapa Jimboni Tanga. Parokia nyingi za Jimbo zimeanzishwa na Warosmini. Hadi sasa hivi wanasimamia parokia kadhaa Jimboni. Baadhi ya Parokia hizo ni Gare, Kwalukonge, Mombo, Saruji, Lushoto na Kwai. Wanazo nyumba za malezi ya vijana huko Lushoto na Gare. Pia wanasimamia Shule ya Sekondari ya Rosmini ambayo zamani ilijulikana kama Saruji.

Pamoja na kufanya kazi kubwa ya kichungaji kwa zaidi ya miaka hamsini hapa Tanga, Shilika hili halikufanya jitihada za kutosha kuvutia vijana wengi kutoka Tanga kuupenda wito wa Upadri katika Shirika lao. Hadi sasa, vijana waliopewa Daraja Takatifu la Upadre kutoka Tanga ni wachache ukilinganisha na muda wa uchungaji waliofanya hapa tanga..