SONI SEMINARI
JIMBO KATOLIKI TANGA
SONI LUSHOTO
JUBILIE YA MIAKA 50
![]() SONI SEMINARI(1976) |
![]() |
![]() |
Baadhi ya madarasa |
![]() |
Tuanze Hall |
NENO LA UFUNGUZI: GAMBERA SONI SEMINARI
Pd. Gerard Kabarega

- -----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
-
NENO LA UZINDUZI WA JUBILEI YA DHAHABU YA MTAKATIFU YOSEPH SONI TAREHE 18 JANUARI 2025
Historia kwa ufupi
Majengo haya ambayo ni seminari kwa sasa yalikuwa ni shule ya watoto wa Wazungu waliokuwa wakifanya biashara kubwa ya kilimo katika mashamba makubwa ya chai, Kahawa na Mkonge. Shule hii ilijulikana kama St. Michael's school na ilikuwa ikimilikiwa na Shirika la Mapadre Warosmini.
Baada ya uhuru wa Tanganyika Mwaka 1961, na sera za nchi baada ya uhuru; Wazungu wengi waliona Tanganyika sio mahali rafiki pa kuendeleza biashara zao. Hivyo wazungu wengi waliondoka Tanganyika na shule kuanza kupoteza wanafunzi, na hatimaye kufungwa kabisa.
Mwezi Julai mwaka 1975 Mhashamu Baba Askofu Maurus Komba baada ya kuona hitaji kubwa la makuhani na wakati huo huo nafasi ambazo jimbo la Tanga linapewa kupeleka waseminari katika seminari ya majimbo ya Mtakatifu Petro Morogoro ni chache aliomba majengo haya ili kuanzisha seminari katika jimbo la Tanga. Lengo kubwa la kuanzishwa kwake lilikuwa ni kupata makuhani wengi watakaotoa huduma ndani na nje ya Jimbo la Tanga.
Seminari hii iliangaliwa na kusaidiwa kwa karibu sana na Askofu Maurus Komba pamoja na Maaskofu wote waliofuata baada yake. Kutokana na uangalizi huu wa maaskofu wote, Seminari hii imeweza kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Mapadre 56 wa Jimbo la Tanga wamelelewa katika seminari hii. Seminari hii pia imelea baadhi ya Mapadre katika majimbo ya Morogoro na Dar es salaam. Vilevile wako Mapadre wa Mashirika ya Rosmin, Benedictine, Shirika la Damu Azizi (Precious Blood), Shirika la Passionist, Shirika la Wakapuchini wa Conventuale, Shirika la Mungu Mwokozi (Salvatorian), Shirika la (Parotine) na Shirika la Carmelite waliopata malezi katika Seminari hii. Zaidi sana Seminari hii imetoa Askofu ambaye ndiye Askofu wetu wa Jimbo la Tanga Mhashamu Askofu Thomas John Kiangio. Vilevile Mheshimiwa sana Padre Thadei Mhagama aliyekuwa Abate wa Shirika la Wabedictine Hanga alipata malezi katika Seminari hii.
Seminari hii pia imetoa viongizi na watumishi wema katika serikali yetu na katika vyama vya Siasa. Pia kutoka Seminari hii tunao walimu wazuri wa dini,viongozi wa Halmashauri za Walei na Waamini wema wanaoeneza Habari Njema ya Upendo wa Kristo ulimwenguni kote.
Yapo matunda mengi lakini kwa haya machache tuliyoyataja, tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa miaka 49 ya uwepo wa Seminari hii.
Dhamiri kubwa ya Mwaka wa Jubilee ni kumshukuru Mungu, kuwakaribisha wanafamilia ya Soni wakiwemo Alumni kuweza kuiona Soni yao na kudhamiria kuiboresha kwa vizazi vijavyo. Pamoja na Seminari yetu kukaribisha wanafamilia, Seminari yetu katika mwaka huu wa kutembea kuelekea kilele cha Jubilei itafanya azimio la kuzitembelea Parokia na taasisi ambazo zimekuwa na mahusiano/ ushirikiano wa muda mrefu na seminari. Ratiba ya matembezi hayo itapangwa na kamati ya Jubilei itakayoundwa na Mhashamu Baba Askofu katika ngazi ya jimbo.
Lengo la sherehe ya Jubilei hii ya Dhahabu ni kujenga Soni Seminari mpya yenye nguvu za kutosha. Lengo hili litawezekana iwapo Soni Seminari itapata ushirikiano wa karibu toka kwa Alumni, marafiki na ndugu wote wa Soni Seminari. Tunawaombea wote Baraka katika Mwaka huu wa uzinduzi wa Jubilei ya Dhahabu. Kanibuni sana.
Fr. Gerard Kabarega Gambera.(18/01/2025)
|
DAWATI LA: Pd. Severine Msemwa:

- -----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
-
KUTOKA 'ST. MICHAEL SEMINARY' YA GERALD, (1975) HADI 'ST. JOSEPH SEMINARY' YA GERALD, 2025:
Nakumbuka sana, nikiwa Padre mpya kabisa wa Juni 29, 1975, Mhashamu Askofu Maurus Komba alinituma kwenda kupaandaa ST. MICHAEL INTERNATIONAL SCHOOL pawe SONI SEMINARY SECONDARY SCHOOL. Marehemu Pd. James McCathy IC, aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo iliyomilikiwa na Wamisionari WAROSMINI, alikuwa anajiandaa kuyakabidhi majengo yale kwa Chama au Serikali wakati ule. Wakatoliki wema walishtuka, wakamtaarifu Askofu Maurus Komba. Azma ya Mhash. Maurus ilikuwa kuanzisha Seminari-Kitalu cha kulelea Mapadre wa Jimbo letu la Tanga. Majengo hayo yalipopatikana, akanituma kupasafisha na kupanga vifaa mbalimbali ili ifikapo August 1975 pawe tayari kuwapokea WANAFUNZI WAASISI kuanza Kidato cha KWANZA. Kazi ilifanyika kikamilifu na kukubalika rasmi tarehe 15/08/1975. Katika Misa rasmi ya kumshukuru Mungu kwa kutusimamia, tuliomba mvua kwa ajili ya wananchi, naye akajibu mara hata kabla Misa kumalizika. Waamini walilazimika kabaki Kanisani kwa saa mbili ili mvua ipungue.
Siku chache baadaye nikapelekwa St. Peter's Seminary Morogoro, nilipowakuta waseminari TITUS MDOE kwa sasa ni ASKOFU wa MTWARA, Padre Paul Mshami Paroko wa Donge, na Padre Silas Singano, Paroko wa St. Mathias Mulumba, Tanga. Wakati huo huo, naye Marehemu Padre Gerard Chilambo ambaye alikuwa GOMBERA MWASISI WA ST. MICHAEL SEMINARY SEC. SCHOOL, akaanza kuwakusanya wanafunzi wa awali wa Soni baadhi yao ni Pd. JOSEPH MBENA, VG wetu, Pd. LEOPALD NYANDWI (Mkalamo), Pd. SEVERINE YAGAZA (USA).
JINA LA UVUVIO: Upenzi kwa Mtakatifu Yosef kama BABA, na MLEZI kulimfanya Askofu Maurus abadili MSIMAMIZI wa Seminari. MWAKA 1980 Machi alimtangaza MT. YOSEFU kuwa MSIMAMIZI wa Seminari. Baada ya tangazo hilo Askofu akaanza kuugua, ikasemwa kwamba MT. MIKAEL amekasirika….. amenyang'anywa usimamizi wa Seminari. Jimbo likaanza maombi, sala, novena kwa ajili ya Askofu. Hatimaye tarehe 19 MACHI 1981, SIKUKUU YA MT. YOSEFU, alfajiri, akiwa hospitalini LITEMBO katika uangalizi wa Dr. Wier, Askofu alipata nafuu na kukutwa na Dr akiwa msalani ananawa. Tangu hapo ikawa rasmi kuwa MT. YOSEFU NDIYE MSIMAMIZI WA SEMINARI YETU YA SONI. Ndiyo maana Mt. Yosefu ni Msimamizi wa Seminari kwa UVUVIO wa Mungu mwenyewe kwa Mtumishi wake Askofu Maurus Komba …. RIP.
Msgr Severine Msemwa.(Janari 11,2025)
|
Pd. Severine Yagaza:
na kuuendea mwaka wa 50 wa Soni Seminari

- -----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
-
KUSHIRIKISHANA KUUENDEA MWAKA WA 50 YA SONI SEMINARI (na spy)
UTANGULIZI:
Nikiwa kidato cha pili pale Soni Seminari, baba Msgr. Msemwa alirudi toka safari ya kimisionari St. Peter’s Morogoro, kuja kuijenga seminari ya jimbo letu kama jalimu na lilezi. Kipindi hicho kilikuwa ni mkiani mwa kimbunga cha kipindupiundu, gonjwa lililotuzuia mengi katika jamii. Ujio wa baba Msemwa mara ya pili Soni ulikuwa ni nuru kubwa kwa seminari yetu changa ambayo ilikuwa na uhaba mkubwa wa majalimu. Akiwa padre mteke, baba Msemwa alikuja na mawazo lukuki ya kuisimamisha na kuimarisha Soni yetu. Alikuwa mwalimu wa Kiswahili mbobezi na haswa haswa katika karakana ya Fasihi na maeneo mengine mengi. Moja ya tunu aliyotugawia katika kipindi kile ilikuwa ni kuipenda “Fasihi Andishi.” Kwa mfano baada ya kukisoma kitabu cha “Diwani ya Kandoro,” baba Msemwa aliweza kuja darasani na kuandika ubaoni, “Kandoro ni mwana siasa, JADILI.”
Insha yangu ya kwanza kumjibu baba Msemwa ilikuwa ni uandishi wa robo ukurasa. Mtindo huo wa uandishi ulituelekeza kwenya alama “0 au F.” Hapo nikafahamu “uchoyo” wa huyu kijana wa ki-Ngoni.
Baba Msemwa amekuwa mtu wa viwango vya juu sana. Baada ya kuvuvumka naye katika safari ya taaluma na malezi na baadaye tufahamu kwamba kujadili siyo lelemama, tulibadilisha mwelekeo. Kujadili ni kujadili haswa. Kwa baba Msemwa, “Swali fupi, lina jibu refu,” na ndio toka hapo tuliupata muziki wake wa kuweza kuandika insha ndefu za kurasa 10 hadi 15 kwa kuyajibu maswali yake mafupi.
Mhimizo wa baba Msemwa katika fasihi umeendelea kuwa ni chachu katika safari zetu za masomo katika ngazi mbalimbali za taaluma. Uandishi na uchambuzi havikuwa haba. Asante baba Msemwa kwa mateso matakatifu uliyotupa wakati ule. Basi tunapoiendea jubilee ya miaka 50 ya Soni Seminari, baba Msemwa ametualika kuchangia kumbukumbu kadha wa kadha za kila mmoja wetu katika milima na mabonde ya safari tulizopitia katika miaka hiyo. Na hapa ninamuunga mkono:
KILICHOTOKEA KABLA:
Oktoba iliyopita, nilifanya mtihani wa kujiunga na seminari ya mtakatifu Petro, Morogoro nikiwa parokiani Kilole. Mtihani huo nilisimamiwa na mapadre wateke wawili Zakaria Kayanza na Casimiri Magwiza (wapumzike kwa amani) ambao walikuwa mapadre wasaidizi. Majibu kutokea nilipatiwa maelekezo ya kuripoti St. Michael's School Soni badala ya St. Peter’s Morogoro. Hii kwangu ilikuwa chenga ya mwili. St. Michael’s School niliyoifahamu ilikuwa ni shule ya watoto wa kizungu. Nikiwa kinda, familia yangu ilipita maeneo ya shule hii kutoka Kisiwani kwenda kuabudu Maangai ambako kulikuwa na kanisa Katoliki, kigango cha parokia ya Gare. Sikuamini macho yangu kwamba sasa mimi nimekuwa mrithi wa taasisi hii ya wakoloni. Taarifa za kujiunga na St. Michael zilikuwa na ladha ya chachu/chungu. Basi niliyapokea mapenzi ya Mungu ambayo daima ni matakatifu. Tulitaarifiwa kwamba baba mhashamu Maurus Komba alikuwa anaanzisha seminari yake ndogo kwa jimbo letu la Tanga kuweza kuwa na karakani/kitalu cha kulea miito mingi ya kipadre kwa ajili ya jimbo lake. Huyu baba alikuwa kweli mwana mapinduzi (JADILI).
JANUARI 17, 1976:
Siku ya kwanza ya kuripoti shule ilikuwa ni Jumamosi Januari 17, 1976 ambapo nilipiga moyo konde kujisogeza hapo seminari ya mtakatifu Mikaeli kuanza rasmi safari ya malezi. Ni siku hii pia ndiyo ilikuwa siku ya kuiaza safari ya mashangilizi ya jubilei ya dhahabu tunayoyaendea hapo Januari 2026. Katika kuongeza uzito wa siku hii ya kuijongelea seminari, mzee Pius alichukua jukumu la kunifikisha hapa kitaluni kwani ilinibidi kuwa na vifaa lukuki vilivyozidi uwezo wa misuli yangu teke. Vifaa hivyo vilikuwa sanduku langu lililokuwa na lebo ya "KILLED," (bila kujua maana yake na jina lililoniwangia kwa muda), jembe, mpini, kwanja, na upanga. Pengine huu ungekuwa ni mzigo mkubwa kidogo kwa kijana mdogo toka nchi ya Kilole. Ni siku hii basi niliweza kukutana na vijana wenzangu wengine 24 toka pembe mbalimbali za jimbo letu la Tanga. Ilikuwa ni siku yangu ya kwanza kuanza maisha ya bweni mbali na wazazi, ndugu na marafiki niliowazoea nyumbani. Baada ya mzee Pius kunikabidhi seminarini kwa wahusika, basi nilikuwa sina chaguo lingine zaidi kujizingirisha na vijana hawa ambao sikuwa nimekutana nao kabla yake. Polepole nilifungua macho yangu ya mwili na roho kuweza kujenga mtandao wa kushirikiana na kuijenga familia hii mpya. Baadhi ya vijana hawa waliingiana kwa karibu kutokana na ushirika wao wa kutokea parokia moja. Mfano toka Pongwe walifika vijana watatu, Joseph Sahani Mbenna (Taso), Ignas Sokoro (Mpimbwe) na John Felician Mahundi. Toka Mlingano walifika Leopold Nyandwi na Rafael Mzuka. Ukiachilia Mkuzi, Kwai, Gare, Mhelo (Lushoto) ambazo zilikuwa na waasisi zaidi ya mmoja. Baadhi yetu walipafahamu hapo seminarini kwani walishakaa pamoja mwaka uliotangulia kwa kipindi fulani. Ninakumbuka siku yangu ya kwanza seminarini Soni sikuwa na amani sana kwani mseminaristi Ignas Sokoro toka Pongwe alikuwa kijana mchakaramu sana na siku ya mwanzo kabisa alifika shuleni na gazeti lake la Uhuru (lililokuwa linauzwa wakati huo senti 30) likiwa na kichwa cha, "Savimbi akimbia Nova Lisboa." Ignas alipita huko na huko akikirudia kichwa hicho cha habari kwa ukakamavu ambao ulinifanya nimkodolee macho kwa ushujaa wake. Pamoja na mshituko huo wa siku ya kwanza nikiwa pekee toka Kilole, nilifarijika kufahamu kwamba kijana mmoja mwembamba na mrefu toka Mlingano (Leopold) alikuwa na mahusiano ya karibu sana na babu yetu mzee Gozera Mbisa aliyekuwa akiishi kambi ya Mlingoti kule Kicheba. Kwa muunganiko huu basi Leopold na mimi tulijenga ukaribu kwa muda mrefu mbele yetu.
YALIYOFUATIA:
Waswahili husema, "Mgumu, mwanzo au Mwanzo, mgumu" Ni kweli. Mara mara baada ya kuwasili, nadhani gambera alikuwa baba Msgr. Mavunga lakini mara moja alihamishiwa Lulago na hapo baba Msgr. Odillo Mtoi alikabidhiwa kijiti cha uongozi wa Soni pia akibaki kuwa paroko wa Kilole. Zaidi ya ugambera wake, baba Mtoi alikuwa profesa wetu wa mwanzo kabisa akitufundisha ki-Ingereza, Bibilia na katekesimo. Ni baadaye kidogo tu, baba askofu alimpata Bwana Ndomba toka sekondari ya Tanga ambaye alikubali kuacha ajira yake ya ualimu serikalini kuja kumuunga mkono baba mhashamu Komba ambaye alikuwa paroko wake kule Peramiho. Bwana Ndomba alikuwa ni mbobezi katika nyanja historia na siasa. Uwezo Bwana Ndomba katika lugha ya uNg’eng’e, ulituhamasisha katika taalumu na kutufanya kuona misuli ya taaluma Soni Seminari. Kwa kuwa yeye alikuwa ni mwalimu wa historia katika ngazi za vidato vya tano na sita, alizoea sana kufundisha kwa njia za “lectures” na hivi lecture yake ya kwanza tunaikumbuka sana ikiwa na mwanzo wa, “The earliest man on earth was Homo?????” Tulimpenda jinsi ambavyo alikuwa akimwaga lugha ya kigeni na mdomo wake umepinda.
Polepole miezi ilipopita, tuliweza kumpata Fr. Oliver Stansfield, I.C kutufundisha ki-Ingereza. Huyu alipachikwa jina la “Peko of Amazon Forest,” kutokana na lecture aliyoirudia kwa kipindi toka kitabu cha “Learning Through Language.” Akiwa Soni Seminari, Fr. Oliver pia alikuwa akisaidia kufundisha kwenye shirika lake kule Gare na Lushoto. Ni baadaye kidogo ndipo pia tuliweza kumpata Fr. Beda Pavel, OSB ambaye alitufundisha masomo ya Elimu ya Viumbe na Kemia kidogo na kwa muda kadhaa alikuwa msarifu wa seminari na pia gambera. Katika siku hizo za awali tulibahatika pia kupata kwa muda mfupi masista wawili wa Maryknoll (Sr. Maria na Sr. Katarina) waliokuwa wakifundisha Sekondari ya wasichana Korogwe na kukubali kuja Soni Seminari kwa mwaliko wa baba askofu. Stafu ya walimu Soni Seminari katika mwaka 1976 ilikuwa rojorojo kidogo. Hivi tulikuwa na muda mfupi darasani na muda mrefu katika mtaala wa ziada. Uhaba wetu wa walimu, ulitufanya tuzingatie kwa karibu maarifa ya wale walimu waliopo na tulikunywa kila kilichomwagika toka vichwani mwao. Tulibahatika kuwa maktaba nzito ambayo tuliirithi toka shule ya watoto wa kizungu iliyofungwa punde. Hivi tuliweza kujisukuma kujisomea maktaba muda mwingi japo kwa kujikokota kutokana na vitabu vingi kuwa katika lugha ya kizungu. Pamoja na changamoto hiyo ya walimu, tulijikita katika nidhamu ya kusoma, kusali, kufanya kazi za mikono, na kucheza.
CHANGAMOTO ZA SHULE MPYA:
Changamoto ya kuanzisha shule mpya, ilimsukuma baba mhashamu Maurus Komba kuwatuma mababa Martin Maganga na Egno Ndunguru (na baadaye baba Msemwa) kwenda kusomea diploma ya elimu katika chuo cha ualimu cha Chang'ombe kule Dar-Es-salaam ili kuja kuisimamisha Soni yetu. Kwa unyenyekevu mkubwa mababa hawa walikwenda Chang'ombe na waliporudi waliweza kuongeza nguvu ya taaluma na malezi.
STAREHE:
Pamoja na changamoto zetu, bado jumuia ya wanafunzi tulijitahidi kufurahia Maisha. Mchezo mkubwa mwaka ule wa mwanzo ulikuwa ni mpira wa miguu. Kwa kuwa tulikuwa 25 tu shule nzima, kila mmoja wetu alipata nafasi ya kucheza kabumbu mara nyingi. Hatukua na mwalimu wa michezo na kwa hivi wanafunzi wenyewe tulijipanga kuweza kujiongoza katika michezo, kazi, sala na masomo. Baadhi yetu kama baba Mbenna alifika Soni akiwa na ufahamu mkubwa wa mpira wa miguu kwani alikuwa ni mchezaji wa timu mahiri katika nchi ya Pongwe, timu iliyojulikana kama Tambaza ikiwa chini ya kocha maarufu bwana Mkebe. Mbenna, Mahundi, Ignas Sokoro (wote wa Pongwe) wakiungana na +John Mndolwa na George Mganga (kutoka Gare) waliufanikisha sana mchezo huu wa kabumbu. Japo nilijitapa kwamba mimi ni namba 7 maarufu katika nchi ya Kilole, kujitapa kwangu kuligonga ukuta nilipoingizwa uwanjani ambapo nilileta maudhi kwa wanaoijua kabumbu. Pengine mara njingi nilimkwaza baba Mbenna kutokana na kukosa ujuzi wa kiwango uwanjani. Baba Mbenna alikuwa na mapafu ya simba kuweza kucheza kitovu (namba 5) lakini kuuzunguka uwanja mzima (nyuma, katikati na mbele) kuja kutusaidia akina sisi vijungu jiko. Baba Mbenna alituhimiza sana kuweza kujenga pumzi katika kulisakata kabumbu kwa kuweka sheria ya kukimbia toka seminari pengine hadi Mbuzii na kurudi au mpaka Mheza (mwelekeo wa Mponde) na kurudi. Ninakumbuka siku moja nilimkasirisha baba Mbenna nikiwa kwenye timu yake kwa kuendelea kushindwa kufunga magoli ya wazi. Hapo pamoja na kuwa upande wake nikiwa na mpira alikuja akanifyekelea mbali na wengi walisikia kilio cha “mama weeeeeeeee.” Sidhani kwamba Mbenna alinichukia, bali alinikomaza.
MWENDELEZO WA CHANGAMOTO:
Pamoja na changamoto za walimu, mwaka ule wa mwanzo tulikuwa na changamoto kadha wa kadha. Hatukuwa na mpira wa miguu na hivi tulijikuta tukiitumia mipira ya rugby tuliyorithi toka kwa watoto wa kizungu kuwa ndiyo mipira yetu ya kabumbu. Kama ujuavyo, mpira wa rugby upoupo na una utapiamlo wa kukosa umbo la mduara na hivi ulihitaji nguvu za ziada kuucheza na kuufanya uzunguke. kuubatiza kuwa mpira wa kabumbu. Pamoja na hangaiko hilo, starehe na burudani iliendele kupatikana vyema uwanjani.
Tatizo lingine lililotukabili lilikuwa ni tatizo la lishe. Uongozi wa mwanzo ulijipanga vyema kuhakikisha kwamba tuna unga wa kutosha kwa ajili ya uji na ugali. Kwa kuwa yalinunuliwa magunia mengi na unga ulikwisha sagwa na walaji tulikuwa wachache, unga uliamua kutususia kwa kuharibika. Swala la kuutupa unga halikuwa katika utaratibu na hali halisi ya uchumi wa wakati ule. Hivi kwa muda mrefu tulipambana na hali yetu ya kula unga uliokuwa chini ya kiwango. Siku zilisonga mbele. Changamoto nyingine ilikuwa ni la upungufu wa mboga ambalo lilituvaa kwa karibu. Kiasi cha maharagwe kilikuwa ni kidogo. Hivi wapishi wetu ilibidi kupika kiasi kidogo cha maharagwe ambacho kilituletea majanga. Waliokuwa wakipata maharagwe walikuwa ni mabwana bwalo. Wengine tuliishia kula ugali na mchuzi wa maharagwe. Tunamshukuru Mungu kwamba wakati tulipofika Soni, bado ardhi ya seminari ilikuwa na rutuba kubwa ya kuruhusu mbogamboga zilizojiotesha mashambani kumea. Hivi mara nyingi tuliingia kwenye maeneo yetu kujichumia mboga mbalimbali za kienjeji kama vile mbwembwe, kihindoi, unkhutu, au mnavu. Basi kila mmoja wetu alileta fungu la mboga jikoni na kumkabidhi mpishi wa jiko kuweza kutengeneza mboga za kulia ugali. Makabila yote hayo ya mboga yalikutana kwenye chungu kimoja na kuweza kujitengeneza katika ladha mpya. Mang’amuzi haya ya sufuria la mboga limekuwa somo langu kubwa katika safari yangu ya maisha iwe ni kule uChagani Kibosho, uNgonini Peramiho, uSambaani Soni au huko poroni ninakoishi sasa. Somo la chungu cha mboga ni kwamba mkikutana kwenye sufuria basi kazi yenu ni kushirikiana na kutengeneza kisindikiza ugali. Amina.
KARO YA SHULE:
Tulipoanza shule pale 1976, karo ya seminary kwa mwaka ilikuwa shilingi 350.00. Ha! Ha! Ha! Mwingine atasema kiasi kidogo sana. Ni kweli ni kidogo lakini kutokana wengi wetu tulitoka kwenye familia za kawaida kama za mzee Pius na mke wake Martha, kiasi hicho kilikuwa ni changamoto ambacho kililipwa kwa ngama kubwa. Sijui kama mzee Pius na mke wake walifanikiwa kumaliza kulipa kiasi hicho cha ada au kuweza kulipa kwa wakati. Kiasi hicho hakikuwa kikubwa hivi na hivi kiliathiri uendeshaji wa shule kuweza kupata mahitaji ya lazima katika malezi. Pengine ni katika miaka ya mbele kidogo, mheshimiwa baba gambera Egno Ndunguru alisisitiza sana malezi ya kiroho ya “kujisadaki” (JADILI). Pamoja na kulipa kiasi hicho kidogo cha ada, ilitubidi tujenge moyo wa sadaka yaani kuyapokea maumivu yanayotukumba kwa moyo mkunjufu. Pengine ugumu wa kulipa karo hii kutoka kwetu kulileta ugumu kwa uongozi wa shule kujipanga kisayansi kuisimamisha shule.
BARAKA YA SIKU ZA AWALI:
Nikizikumbuka siku za awali za mama Soni, siwezi kumaliza sura hii bila ya kuwataja mihimili ya seminari yetu ambayo ni masista wa COLU wa wakati ule waliopangiwa kuwa walezi seminarini. Nikiwataja wachache kabisa ni Sr. Beatina aliyekuwa ni kila kitu na Sr. Dorothea ambaye alikuwa ni mpishi wa chakula cha wanafunzi. Masista hawa na wenzao ambao waliishi nyumba ya awali sehemu ilipo sasa bweni la Ndunguru, waliishi maisha ya kujisadaki. Katika uhaba wa vitendea kazi, walitulea na kutuhimiza kama watoto wao. Wote wa masista hawa wametangulia mbele za haki na roho zao zipumzike pema peponi. Pamoja na masista hawa ni mashahidi wazee wetu wafanyakazi kama vile akina mseremala Musa, mzee Saidi na akina mzee Pita. Hawa nao walijisadaki kuilea seminari yetu. Wazee hawa hawakutamani utajiri bali walitamani kuisimamisha Soni yetu. Kila siku ya kazi fundi Musa alitembea kwa miguu toka nyumbani kwake maeneo ya mbelei na kufika seminarini kufanya kazi zote za kiseremala na jioni tena kutembea kurudi nyumbani. Pengine ndiyo maana wazee wale hawakupata magonjwa tunayoyapata siku hizi kutokana na maisha ya mazoezi mazito na unyofu wao wa moyo. Wote hawa wametangulia mbele ya haki.
MWITO:
Tunapokiendea kilele cha miaka 50 ya mama Soni hapo Januari 2026, tunamshukuru baba askofu Thomas John Kiangio kumbariki gambera wa sasa baba Gerald Theodori Kabarega kulitandika jamvi ili familia ya mama Soni kuuzindua mwaka wa Jubile tangia Januari 2025 ili tupate muda wa kutosha kufikiri. Jamvi hili ni muhimu sana. Jamvi hili linamualika kila mwanafamilia ya Soni awe ni mwana alumni (mlelewa), au mlezi, au mzazi au mwanandugu wa walelewa, au aliyefanya biashara na Soni kuketi kitako jamvini kuzama katika masimulizi na tafakuri za kuutambua ukoo na familia yetu, kuzijua tunu zilizoisimamisha Soni yetu kwa miaka 50 pasi kupumua.
Inatubidi kufungua kumbukumbu zetu kuwataja kwa majina yao waliomsimamisha mama Soni katika miaka yote hii. Je hao ni nani? Walifanya nini? Wakati gani? Walifanikiwaje? Walishindwaje? Walipopiga mieleka, je ilikuwa mieleka ya mende? Kama siyo ya mende, walisimamaje? Masimulizi haya yatatusaidia kuwaenzi kila mmoja aliyechangia kiasi chochote kile kumsimamisha mama Soni. Masimulizi haya yatatupatia dira angavu ya kuona ni jinsi gani ya kuisimamisha Soni yetu kwa vizazi vingi vijavyo.
Katika miaka ya sabini katika maadhimisho ya sikukuu ya SabaSaba mwana-mashairi mmoja alipokuwa anasimulia mafanikio ya chama cha TANU alitoa kibwagizo na kuihoji kadamnasi, “Timng’he mbwai TAAAANU?” Nami nikiwa mlelewa, mlezi na mwanafamilia ya mama Soni, ninapenda kukikopa kibwagizo hicho na kuwauliza wanafamilia ya Soni yetu, “Timng’he mbwai Soni seminai.” Leo hii tunajivunia mno faida kubwa iliyofanywa na seminari yetu.
Seminari yetu ifikapo mwakani itakuwa imesomesha zaidi ya wanafunzi 2000 ambao hivi sasa wametawanyika katika kada mbalimbali na sehemu mbalimbali mbinguni, ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. Ndani yetu wapo makada wa Imani ambao wanaichapa Injili ya Kristu kwenda mbele wakitumia upadre wa ubatizo wao. Seminari imezalisha makada wa siasa, wanamuziki wa kutupwa, wanasayansi, watumishi wa serikali na taasisi binafsi. Tunao mapadre ndani ya jimbo la Tanga na nje ya jimbo katika taasisi mbalimbali. Seminari imezalisha abate mstaafu kule Hang na mwaka jana seminari imetunukiwa kumpata askofu. Mama Soni anazo sifa za kumshukuru Mungu na pia kujivuna kama siyo kujivunia.
TAMATI:
Poleni kwa yeyote atakayeisoma tungo hii. Tungo hii haina haikelenga udadavuzi wa mada ya kitafiti. Tungo hii imefukuliwa tu katika kumbukumbu za mwandishi na kushirikishwa kwa wale waliokaa jamvini wakisubiri kuoshwa mikono ili wapate kikombe cha mchaichai. Tungo hii siyo historia ya miaka 50. Tungo hii ni punje ndogo ya haladari inayojikita kuuangalia ule mwaka wa kwanza wa seminari yetu. Tungo hii haina undani wa kina imeparua kile kidogo katika kuchimba kumbukumbu tukifahamu kwamba kumbukumbu nazo zinachuja. Pamoja na hali yake hiyo, tungo hii ninaiwasilisha kwa mwalimu wetu aliyetusukuma ku-JADILI na kuandika kwa kirefu mada zilizo mezani. Pengine ikimpendeza naye aipitie na kuikosoa kama ilivyo ada. Jalimu hili ni baba Monsinyori Severine Severine Msemwa (Mhangileki). na haswa Sisi tuliokuwepo wakati huo, inatubidi kuzishirikisha kumbukumbu hivi kwa vizazi vyote ili vizazi hivi viweze kumfahamu mama Soni alikotoka, alipo na anapokwenda siku za usoni. Kumbukumbu hizi ni tunu (madini) ambayo zinabidi kuchimbuliwa na kushirikishwa ili mila zenye afya zijengeke na kushirikishwa Pamoja na yote haya, siku hazikuganda. Siku zilikwenda mbele kwa mbele. Tuliweza kufahamiana vizuri ndani ya jumuia ya wanafunzi. Tulishirikiana vyema na walezi wetu (mapadre, masista). Tuliijenga familia yetu ya Soni. Tulielimishana kwa kulia pamoja na kucheka pamoja. Tulijifunza pamoja.
Pd. Severine P. Yagaza.(Janari 16,2025)
|
Picha mbalimbali katika uzinduzi:
![]() |
Baadhi ya waliosoma Soni Seminari |
![]() |
Picha siku ya uzinduzi kuelekea jubilei |