WASIFU WAKE
KUZALIWA:
Padre Casmir Paul Magwiza alizaliwa tarehe 21 Desemba 1948 katika kijiji cha Migambo/Mkuzi, Wilayani Lushoto katika Mkoa wa Tanga. Akiwa ni
mtoto wa tatu (3) kati ya watoto wa nne (4) wa Mzee Paul Magwiza na Mama Katarina Mbilu.
ELIMU:
Elimu ya Msingi: Ni katika kijiji cha Migambo/Mkuzi Padre Casmir Magwiza alipata Elimu ya Msingi, katika shule ya Msingi Mkuzi kuanzia
mwaka 1959 – 1962, ambapo alisoma Darasa la I - IV.
Baadaye alijiunga na Seminari ya Mt. Petro – Bagamoyo kwa masomo ya Darasa V – Darasa X/Kidato cha II, mnamo mwaka 1963 – 1967.
Elimu ya Sekondari: Mwaka 1968 – 1969, Padre Casimir Magwiza aliendelea na masomo katika Seminari ndogo ya Mt. Karoli, Itaga/Tabora kwa malezi ya Upadre.
Katika seminary ya Itaga alisoma Kidato cha III na IV.
Seminari Kuu Kibosho/Moshi: Baada ya kuhitimu Kidato cha nne (4), aliendelea tena na malezi ya upadre katika Seminari Kuu ya Kibosho kwa Masomo ya Falsafa.
Yaani kuanzia mwaka 1970 – 1971.
Seminari Kuu Kipalapala/Tabora: Padre Casimir Magwiza alijiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala kwa masomo ya Teolojia mnamo mwaka 1972 – 1975.
DARAJA LA USHEMASI:
Mnamo tarehe 29 Juni, 1974, Padre Casimir Magwiza alipewa Daraja Takatifu la Ushemasi, katika Kanisa Kuu la Jimbo, Mt. Anthony wa Padua – Chumbageni/Tanga.
Na Mhashamu Maurus Komba, aliyekua Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.
DARAJA LA UPADRE:
Tarehe 29 Juni 1975, Padre Casimir Magwiza alipewa Daraja Takatifu la Upadre katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Tanga, la Mt. Anthony wa
Padua – Chumbageni/Tanga. Na Mhashamu Maurus Komba, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.
SEHEMU ALIZOWAHI KUISHI NA KUFANYA KAZI KATIKA MAISHA YAKE:
Marehemu Padre Casimir Magwiza aliwahi kuishi na kufanya kazi katika sehemu zifuatazo:
- Parokia ya Kilole: Baada ya Daraja Takatifu la Upadre, Padre Casimir Magwiza alifanya kazi katika Parokia ya Kilole – Korogwe, kama Paroko Msaidizi (03. 08. 1975 mpaka 12. 08. 1977).
- Parokia ya Mlingano: Mnamo tarehe 12. 08. 1977 Padre Casimir Magwiza alitumwa kwenda kufanya kazi katika Parokia ya Mlingano katika nafasi ya Paroko Msaidizi, mpaka alipohama tarehe ya 05. 03. 1978.
- Masomo ya Muda mfupi kwaajili ya “Maendeleo ya Jamii”: Mnamo mwaka 1978, Padre Casimir Magwiza alihudhuria mafunzo ya mwaka mmoja kwaajili ya “Maendeleo ya Jamii” – Dar es salaam.
- Parokia ya Mt. Theresia/Barabara 20 - Tanga: Baada ya kuhitimu mafunzo yake, Padre Casimir Magwiza alitumwa kwenda kufanya kazi katika Parokia ya Mt. Theresia/Barabara 20 katika nafasi ya Paroko Msaidizi. Pamoja na nafasi hiyo ya Uparoko Msaidizi, Padre Casimir Magwiza aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Caritas Jimbo la Tanga. Hii ilikuwa ni tarehe 05. 03. 1979 – 18. 05. 1980.
Mnamo tarehe 18. 05. 1980, Padre Casimir Magwiza aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mt. Theresia Barabara 20 – Tanga, aliendelea kuwa Paroko wa Parokia
hiyo mpaka tarehe 05. 06. 1995.
Pamoja na majukumu hayo, akiwa katika Parokia ya Mt. Theresia/Barabara 20, Marehemu Padre Casimir Magwiza aliendelea kuwa Mkurugenzi wa Caritas Jimbo la Tanga.
Alikuwa pia Mkuu wa Kanda ya Tanga (Dean). Alikuwa pia Katibu wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Jimbo. Aliteuliwa pia kuwa Mshauri wa Askofu
(College of Consultors/Jopo la Washauri wa Askofu).
Mnamo mwaka 1994, Padre Casimir Magwiza aliteuliwa na wenzake wa Jopo la Washauri wa Askofu (College of Consultors) kuwa Kiongozi wa Jimbo
(Diocesan Administrator) kuliongoza Jimbo Katoliki la Tanga wakati wa mpito ambapo Jimbo halikuwa na Askofu, baada ya Uhamisho wa Mhashamu Telesphor Mkude kutoka Jimbo la Tanga na kuhamia Jimbo la Morogoro.
Aliliongoza Jimbo kwa muda wa mwaka mmoja mpaka tulipopata Askofu wa Jimbo.
Katika Parokia hii ya Mt. Theresia/Barabara 20, ndipo Marehemu Padre Casimir Magwiza aliishi kwa muda mrefu takribani miaka 16, akimtumikia Mungu kwa uaminifu na upendo.
- Parokia ya Mt. Anthony wa Padua – Chumbageni/Tanga: Mnamo tarehe 05. 06. 1995, Padre Casimir Magwiza alihama kutoka Parokia ya Mt. Theresia/Barabara 20 na kwenda kuwa Paroko wa Kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua – Chumbageni/Tanga.
Pamoja na nafasi ya Uparoko aliyokuwanayo katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua, mnamo tarehe ya 12. 06. 1995 Padre Casimir Magwiza, aliteuliwa na Mhashamu Anthony Banzi Askofu wa Tanga kuwa Naibu wa Askofu wa Jimbo la Katoliki la Tanga (Vicar General). Kazi aliyoifanya kwa muda wa miaka kumi na mitatu (13), yani toka tarehe 12. 06. 1995 – 21. 05. 2008.
- Parokia ya Kabuku: Mnamo tarehe 27. 10. 2000, Padre Casimir Magwiza alihama kutoka Parokia ya Mt. Anthony wa Padua na kwenda kuwa Paroko wa Parokia ya Kabuku. Pamoja na jukumu hilo, aliendelea pia kuwa Wakili/Naibu wa Askofu wa Jimbo la Tanga.
- Parokia ya Kilole: Mnamo tarehe 24. 09. 2002 Padre Casimir Magwiza alihama kutoka katika Parokia ya Kabuku na kwenda kufanya kazi katika Parokia ya Kilole. Wakati huo huo, Padre Casimir Magwiza alikuwa Dean wa Kanda ya Korogwe, pia aliendelea kuwa Wakili/Naibu wa Askofu wa Jimbo la Tanga.
- Uaskofuni – Raskazone/Tanga: Mnamo tarehe 26 Mei 2008, Padre Casimir Magwiza alihama kutoka Parokia ya Kilole na kwenda kuishi Uaskofuni – Raskazone/Tanga kwa mapumziko kwa ajili ya kutazamia afya yake, ili awe karibu na madaktari na huduma za afya.
UGONJWA NA MAUTI:
- Padre Casimir Magwiza alikua akisumbuliwa na Ugonjwa wa Kisukari kwa muda mrefu wa uhai wake. Lakini mnamo mwaka 2007 akiwa anaishi Kilole, afya yake ilizidi kuwa mbaya na kudhohofika siku baada ya siku. Udhaifu wake uliendelea huku akiwa anapata matibabu sehemu mbalimbali na katika Hospitali, Vituo vya Afya na Dispensary mbalimbali ndani ya Mkoa wetu na hata nje ya mkoa.
Baada ya hali yake kuwa dhaifu zaidi, kiasi cha kupooza sehemu za viundo vyake ndipo alipohama kutoka Kilole na kuja Tanga, Uaskofuni/Raskazone ili awe karibu na Huduma za Afya.
Padre Casimir Magwiza alipata matibabu katika sehemu mbalimbali: Kituo cha Afya Kwamndolwa, MED-ED-CLINIC - Dar es salaam kwa Dr. Lwakatare, Hospital ya Dr. Ngayomela – Tanga, Kituo cha Afya Tumaini/Tanga, Hospital ya Regency – Dar es salaam, Hospital ya Rufaa Bombo (Kwa Dr. Chrisantus Kalenzi aliyekuwa akimfanyia mazoezi ya viungo) na Hospital ya Rufaa KCMC – Moshi (ambapo alikuwa anakwenda kwa Clinic yake kila baada ya muda kadiri alivyoandikiwa na Daktari).
Afya ya Padre Casimir Magwiza iliendelea kuwa dhaifu kiasi cha kuendelea kupooza (Paralize) karibu sehemu kubwa ya mwili wake. Hata hivyo, Padre Casimir Magwiza aliendelea kupata tiba na ushauri katika Hospitali mbalimbali nchini, juu ya ugonjwa wake.
- Mnamo tarehe 02 Machi 2013, siku ya Jumamosi, majira ya saa saba (7) Mchana Mpendwa wetu Padre Casimir Magwiza ndipo alipoiaga dunia katika Kituo cha Afya Tumaini – Tanga.
- Leo tarehe 06 Machi 2013, siku ya Jumatano, ndipo tunapomuaga na kumsindikiza ndugu yetu Mpendwa Padre Casimir Paul Magwiza, aliyeishi kwa miaka Sitini na tano (65) ya uhai wake. Na miaka thelathini na minane (38) kama Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga.
SHUKRANI:
Mhashamu Baba Askofu Anthony M. Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, pamoja na Mapadre wa Jimbo Katoliki la Tanga, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote walioshiriki katika jitihada mbalimbali za kumsaidia Padre Casimir Magwiza wakati wa ugonjwa wake.
1. Shukrani zimfikie Mhashamu Askofu Telesphor Mkude – Askofu wa Morogoro kwa kuwa tayari kuungana nasi katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu Padre Casimir Magwiza.
2. Shukrani ziwafikie Madaktari na Wauguzi wote wa Hospitali na Vituo vya Afya: Hospital ya MED-ED-CLINIC Dar es sallam kwa Dr. Lwakatare, Hospitali ya Rufaa KCMC, Hospital ya Regency – Dar es salaam, Kituo cha Afya Kwamndolwa, Hospital ya Dr. Ngayomela - Tanga, Dr. Chrisantus Kalenzi wa Bombo/Tanga aliyekuwa akimfanyia mazoezi ya viungo na Kituo cha Afya Tumaini, ambapo Padre Casimir Magwiza alipata Huduma.
3. Shukrani zetu pia ziwafikie ndugu wa Marehemu Padre Casimir Magwiza: Kaka yake Bw. John Magwiza wa Mkuzi/Lushoto, Dada yake Mama Maria Kileo wa Mkuzi/Lushoto, Mdogo wake Bw. Daniel Magwiza wa Dar es salaam, Mdogo wake Bw. John Shemkunde wa Arusha, Mdogo wake Dr. Mathew Mganga wa Tanga, mototo wa kaka yake Bw. Alex Magwiza wa Dar es salaam pamoja na wajomba zake ambao daima walifika Raskazone, walifika pia katika Kituo cha Afya Tumaini kumjulia hali Padre, na kumtia moyo wakati wa ugonjwa wake.
4. Tunamshukuru pia Kijana: Felix Kileo ambaye ni mjomba wa Marehemu Padre Casimir Magwiza daima alikua karibu katika kumhudumia Padre, na kwa muda mwingi yeye ndiye aliyekuwa naye karibu. Tunamshukuru sana.
5. Tunazishukuru Parokia za Mt. Theresia – Barabara Ishirini na Mt. Mathias Mulumba – Sahare, kwa kuwa tayari kuchangia Fedha kwaajili ya kuwatunza na kuwahudumia Mapadre wetu wagonjwa waliopo katika Kituo chetu cha Afya Tumaini, akiwemo Marehemu Padre Casimir Magwiza.
6. Tunawashukuru Mapadre: Mheshimiwa Sana Padre Martin Maganga (VG), Padre Maurus Shemdoe (Chaplain wa Wagonjwa), pamoja na Mapadre wote wa Parokia za Mt. Anthony wa Padua, Mt. Theresia, Mt. Mathias Mulumba na Amboni ambao walikua tayari kushiriki utaratibu waliojipangia wa kuwahudumia na kuwatunza mapadre wenzao wagonjwa waliopo katika Kituo cha Afya Tumaini.
7. Tunawashukuru pia Jumuiya ya Uaskofuni, Jumuiya ya Masista wa Tumaini pamoja na Sr. Phillipina Arudika ambao daima wanafika Kituo cha Afya Tumaini kuwapelekea wagonjwa chakula.
8. Tunawashukuru pia ndugu jamaa na marafiki wa Padre Casimir Magwiza waliofika kila wakati kumjulia hali alipokua katika Matibabu katika Kituo cha Afya Tumaini.
9. Tunawashukuru pia Wakristo mbalimbali pamoja na watu wenye mapenzi mema waliofika Hospitalini kumjulia hali Marehemu Padre Casimir Magwiza.
10. Tunawashukuru pia Wahudumu wa Mortualy katika Hospitali ya Bombo – Tanga kwa ushiriano wao. Tunawashukuru pia Madereva walioshiriki katika zoezi zima la kumpeleka Padre Casimir Magwiza katika Matibabu yake, kupeleka mwili wake Mortualy na kuuleta hapa Kilole kwa Mazishi. Tunawashukuru wote.
11. Tunawashukuru waombolezaji wote mliofika hapa leo hii katika kumsindikiza na kumuaga Mpendwa wetu Padre Casimir Magwiza, wengine toka jana mlikuwa tayari kukesha na mwili wa Marehemu pale katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua. Bila kuwasahau wale wote waliochimba na wanaoendelea kuchimba Kaburi huko nje, wale watakaoandaa mishumaa pamoja na Mataji kwaajili ya kupamba Kaburi la Mpendwa wetu Padre Casimir Magwiza.
12. Tunaishukuru Radio Huruma, pamoja na Idara ya Habari Jimbo Katoliki la Tanga kwa kuendelea kutupatia taarifa hizi za msiba wetu wa Padre Casimir Magwiza.
13. Tunazishukuru Kamati zote mbili za Maziko kutoka Jimboni na hii ya hapa Parokia ya Kilole kwa kuratibu shughuli zote za maziko na msiba huu.
14. Tunamshukuru sana Mama Mkuu wa Shirika la Masista Kwamndolwa, pamoja na uongozi wake, kwa kuwa tayari kushiriki msiba huu kwa kuchangia baadhi ya vitu mbalimbali ili kufanikisha shughuli hizi za mazishi. Tunawashukuru wote.
15. Shukrani kwa Uongozi wa UMAWATA Taifa. Pamoja na Mapadre, Masista na watu mbalimbali waliopo nchini na nje ya nchi; ambao wameshindwa kushiriki nasi katika Ibada hii ya maziko ya Padre Casimir Magwiza, lakini kwa namna ya pekee wameungana nasi kwa kututumia salamu za rambirambi. Napenda kuwatambua kama ifuatavyo:
- Fr. James Flynn, IC (aliyekuwa Mkuu wa Rosmini Duniani)
- Mama Mkuu Mstaafu, Sr. Leonia Mdoe (Italia)
- Askofu Mteule, Mhashamu Titus Mdoe
- Familia ya Mr. Kempenaar (Holland)
- Mons. Faustin Mushi (Nairobi)
- Pd. Joseph Shetui na Pd. Severine Yagaza (U.S.A)
- Fr. Richard Kimbwi na Pd. Sylvester Nitunga (Ulaya)
- Masista wa COLU (Italia)
- Pd. Alex Masangu na Pd. Thaddeus Mkamwa (SAUT – Mwanza)
- Pd. Clement Jandu (Ntungamo Seminary – Bukoba)
- Fr. Joseph Shio, CSSp (Italia)
Imeandaliwa na Kusomwa na,
Fr. Peter s. Kagaba,
KATIBU MKUU – JIMBO KATOLIKI LA TANGA.
Raha ya Milele Umpe Ee Bwana,
Na mwanga wa milele Umuangazie,
Apumzike kwa Amani =========== AMINA.
catholic diocese of Tanga © 2024
|