WASIFU WAKE
KUZALIWA:
Padre Egino Yakobo Ndunguru alizaliwa tarehe 24 Agosti 1942 katika kijiji cha Kipika, Wilayani Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma.
Akiwa ni mtoto wa kwanza (1) kati ya watoto wa tano (5) wa Mzee Yakobo Yapesa Ndunguru na Mama Elizabeth Kandumu Mbele.
ELIMU:
Elimu ya Msingi: Ni katika kijiji cha Kipika Padre Egino Ndunguru alipata Elimu ya Msingi, katika shule ya Msingi Mbinga kuanzia
mwaka 1948 – 1959 alipohitimu Elimu ya Msingi.
Elimu ya Sekondari: Mwaka 1960 – 1963, Padre Egino Ndunguru alijiunga na Seminari ndogo ya Jimbo Katoliki la Songea, Likonde Seminari
kwa malezi ya Upadre.
Seminari Kuu Peramiho: Baada ya kuhitimu Kidato cha nne (4), aliendelea tena na malezi ya upadre katika Seminari Kuu ya Peramiho kwa Masomo
ya Falsafa na Theolojia. Yaani kuanzia mwaka 1963 – 1972. Ambapo alihitimu na kupata Shahada ya Kwanza katika Masomo ya Theolojia
(Baccalaureate in Theology) kutoka katika Chuo Kikuu cha Urbaniana – Roma/Italy.
DARAJA LA USHEMASI:
Mnamo mwaka 1969, Padre Egino Ndunguru alipewa Daraja Takatifu la Ushemasi, huko Jimboni Songea. Na Mhashamu Jacob Komba, aliyekua Askofu
wa Jimbo Katoliki la Songea.
Mnamo mwaka 1971, Padre Egino Ndunguru akiwa bado ni Shemasi, kwa hiari yake mwenyewe aliamua kuhama kutoka Jimbo Katoliki la Songea na
kuhamia katika Jimbo Katoliki la Tanga.
DARAJA LA UPADRE:
Tarehe 09 Aprili 1972, Padre Egino Ndunguru alipewa Daraja Takatifu la Upadre katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Tanga, la
Mt. Anthony wa Padua – Chumbageni/Tanga.
SEHEMU ALIZOWAHI KUISHI NA KUFANYA KAZI KATIKA MAISHA YAKE:
Marehemu Padre Egino Ndunguru aliwahi kuishi na kufanya kazi katika sehemu zifuatazo:
- Parokia ya Mt. Anthony wa Padua: Baada ya Daraja Takatifu la Upadre, Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika Parokia ya
Mt. Anthony wa Padua – Chumbageni/Tanga, kama Paroko Msaidizi.
- Chuo cha Ualimu: Mnamo mwaka 1975 Padre Egino Ndunguru alijiunga na Chuo cha Ualimu; National College – Dar es salaam, ambapo
alihitimu na kupata Diploma ya Ualimu.
- Soni Seminari: Baada ya kuhitimu mafunzo ya Ualimu katika ngazi ya Stashahada, Padre Egino Ndunguru alitumwa kufanya kazi katika
Seminari ndogo ya Jimbo la Tanga, Soni Seminari kama Mwalimu na Mlezi. Kwa muda wa mwaka mmoja.
- Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM): Baada ya mwaka mmoja wa kufundisha katika Seminari ya Soni, yaani mnamo mwaka 1978 Padre
Egino Ndunguru alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwaajili ya Shahada ya Kwanza (Bachelor of Arts in Education). Alihitimu
masomo yake mnamo mwaka 1981.
- Soni Seminari: Baada ya kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Padre Egino Ndunguru alirudi tena kufundisha
katika Seminari ya Soni. Na mnamo mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Rector/Gombera wa Seminari ya Soni mpaka mwaka 1988 alipomaliza muda wake.
- Mkurugenzi wa Habari Jimbo Katoliki la Tanga: Mnamo mwaka 1989, Padre Egino Ndunguru aliteukiwa kuwa Mkurugenzi wa Habari Jimbo
katoliki la Tanga.
- Parokia ya Hale: Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika Parokia ya Hale kama Paroko. Mpaka alipohama tarehe 27 Machi 1995.
- Parokia ya Mt. Anthony wa Padua: Mnamo tarehe 27 Machi 1995 mpaka tarehe 12 Aprili 2000, Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika
Parokia ya Mt. Anthony wa Padua, kama Paroko Msaidizi. Pamoja na jukumu hilo, pia aliendelea kufanya kazi katika Idara ya Habari Jimbo
kama Mkurugenzi wa Idara hiyo. Pia akiwa katika Parokia ya Mt. Anthony wa Padua, Padre Egino Ndunguru alihudumia Wafungwa na Mahabusu
waliopo katika Gereza la Maweni – Tanga. Kazi aliyoifanya kwa moyo na upendo.
- Parokia ya Maramba: Mnamo tarehe 12 Aprili 2000 mpaka tarehe 09 Septemba 2002, Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika Parokia ya
Maramba kama Paroko.
- Parokia ya Potwe: Mnamo tarehe 17 Novemba 2002 mpaka tarehe 30 Julai 2004, Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika Parokia ya
Potwe kama Kaimu Paroko.
- Parokia ya Mt. Theresia/Barabara Ishirini: Mnamo tarehe 30 Septemba 2004 mpaka tarehe 31 Januari 2006, Padre Egino Ndunguru aliishi
katika Parokia ya Mt. Theresia/Barabara Ishirini – Tanga.
- Parokia ya Kongoi: Mnamo tarehe 28 Februari 2006 mpaka 02 Januari 2009, Padre Egino Ndunguru alifanya kazi katika Parokia ya Kongoi
kama Paroko Msaidizi. Mnamo tarehe 02 Januari 2009, Baada ya Paroko wa Kongoi kuhama, Padre Egino Ndunguru aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia
ya Kongoi, ambapo aliendelea kuwa Paroko mpaka tarehe 17 Agosti 2009 alipohama kutoka Parokia ya Kongoi.
- Parokia ya Mt. Mathias Mulumba – Sahare: Mnamo tarehe 17 Agosti 2009, Padre Egino Ndunguru alipangwa kuishi katika Parokia ya
Mt. Mathias Mulumba – Sahare/Tanga. Mpaka afya yake ilipoanza kudhoofika alikua akiishi katika Parokia ya Mt. Mathias Mulumba.
UGONJWA NA MAUTI:
- Padre Egino Ndunguru alikua akisumbuliwa na Ugonjwa wa Kansa ya Kibofu cha Mkojo. Pamoja na operesheni aliyopata katika Hospitali ya
Rufaa KCMC – Moshi, hiyo ilikua ni jitihada za kumpatia tiba itakayomsaidia kupona tatizo lake. Bado Padre Egino Ndunguru aliendelea kuwa
dhaifu kiasi cha kupooza (Paralize) kuanzia sehemu za kiuno chake na kushuka miguuni. Hata hivyo, Padre Egino Ndunguru aliendelea kupata tiba
na ushauri katika Hospitali mbalimbali nchini, juu ya ugonjwa wake.
- Mnamo tarehe 25 Oktoba 2012, siku ya alhamisi, majira ya saa tatu (3) Asubuhi Mpendwa wetu Padre Egino Ndunguru ndipo alipoiaga dunia
katika Kituo cha Afya Tumaini – Tanga.
- Leo tarehe 30 Oktoba 2012, siku ya Jumanne, ndipo tunapomuaga na kumsindikiza ndugu yetu Mpendwa Padre Egino Yakobo Ndunguru, aliyeishi
kwa miaka Sabini (70) ya uhai wake. Na miaka Arobaini (40) kama Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga.
SHUKRANI:
Mhashamu Baba Askofu Anthony M. Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, pamoja na Mapadre wa Jimbo Katoliki la Tanga, tunapenda kutoa shukrani
zetu za dhati kwa wale wote walioshiriki katika jitihada mbalimbali za kumsaidia Padre Egino Ndunguru wakati wa ugonjwa wake.
1. Shukrani ziwafikie Madaktari na Wauguzi wote wa Hospitali na Vituo vya Afya: Hospitali ya KCMC, Muhimbili, Bugando, Peramiho, Ocean
Road na Kituo cha Afya Tumaini, ambapo Padre Egino Ndunguru alipata Huduma.
2. Shukrani zetu pia zimfikie Abate wa Abasia ya Peramiho na Abasia nzima ya Peramiho kwa moyo wao wa kuwa tayari kumpokea na kumtunza
Padre Egino Ndunguru wakati wa ugonjwa wake.
3. Tunawashukuru pia Vijana: Joseph, Bahati pamoja na Felix Kileo ambao daima walikua karibu katika kumuhudumia Padre Egino Ndunguru wakati
akiwa katika Kituo cha Afya Tumaini – Tanga.
4. Tunazishukuru Parokia za Mt. Theresia – Barabara Ishirini na Mt. Mathias Mulumba – Sahare, kwa kuwa tayari kuchangia Fedha kwaajili ya
kuwatunza na kuwahudumia Mapadre wetu wagonjwa waliopo katika Kituo chetu cha Afya Tumaini, akiwemo Marehemu Padre Egino Ndunguru.
5. Tunawashukuru Mapadre: Mheshimiwa Sana Padre Martin Maganga (VG), Padre Maurus Shemdoe (Chaplain wa Wagonjwa), pamoja na Mapadre wote wa
Parokia za Mt. Anthony wa Padua, Mt. Theresia, Mt. Mathias Mulumba na Amboni ambao walikua tayari kushiriki utaratibu waliojipangia wa
kuwahudumia na kuwatunza mapadre wenzao wagonjwa waliopo katika Kituo cha Afya Tumaini.
6. Tunawashukuru pia Jumuiya ya Uaskofuni, Jumuiya ya Masista wa Tumaini pamoja na Sr. Phillipina Arudika ambao daima wanafika Kituo cha
Afya Tumaini kuwapelekea wagonjwa chakula.
7. Tunawashukuru pia ndugu zake Padre Egino Ndunguru kutoka Mbinga na humu Jimboni mwetu Tanga waliofika kila wakati kumjulia hali alipokua
katika Matibabu katika Kituo cha Afya Tumaini.
8. Tunawashukuru pia Wakristo mbalimbali pamoja na watu wenye mapenzi mema waliofika Hospitalini kumjulia hali Marehemu Padre Egino
Ndunguru.
9. Tunawashukuru pia Wahudumu wa Mortualy katika Hospitali ya Bombo – Tanga kwa ushiriano wao. Tunawashukuru pia Madereva walioshiriki
katika zoezi zima la kumpeleka Padre Egino Ndunguru katika Matibabu yake, kupeleka mwili wake Mortualy na kuuleta hapa Kilole kwa Mazishi.
Tunawashukuru wote.
10. Tunawashukuru waombolezaji wote mliofika hapa leo hii katika kumsindikiza na kumuaga Mpendwa wetu Padre Egino Ndunguru, wengine toka
jana mlikuwa tayari kukesha na mwili wa Marehemu pale katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua. Bila kuwasahau wale wote waliochimba na
wanaoendelea kuchimba Kaburi huko nje, wale watakaoandaa mishumaa pamoja na Mataji kwaajili ya kupamba Kaburi la Mpendwa wetu Padre Egino
Ndunguru.
11. Tunaishukuru Radio Huruma, pamoja na Idara ya Habari Jimbo Katoliki la Tanga kwa kuendelea kutupatia taarifa hizi za msiba wetu wa
Padre Egino Ndunguru.
12. Kwa Namna ya pekee tunapenda kuwashukuru vijana waliokua tayari kumchangia damu Padre Egino Ndunguru. Vijana hao ni MARTIN KURWA,
DUTSAN ALOYCE na PASCHAL KUNAMBI kutoka Parokia ya Mt. Theresia – Barabara Ishirini/Tanga. Mwenyezi mungu awabariki sana.
13. Tunazishukuru Kamati zote mbili za Mazishi kutoka Jimboni na hii ya hapa Parokia ya Kilole kwa kuratibu shughuli zote za mazishi na
msiba huu.
14. Tunamshukuru sana Mama Mkuu wa Shirika la Masista Kwamndolwa, pamoja na uongozi wake, kwa kuwa tayari kushiriki msiba huu kwa kuchangia
baadhi ya vitu mbalimbali ili kufanikisha shughuli hizi za mazishi. Tunawashukuru wote.
Imeandaliwa na Kusomwa na,
Pd. Peter S. Kagaba,
KATIBU MKUU – JIMBO KATOLIKI LA TANGA.
Raha ya Milele Umpe Ee Bwana,
Na mwanga wa milele Umuangazie,
Apumzike kwa Amani =========== AMINA.
catholic diocese of Tanga © 2024
|