+ Pd. Francis Gembe Wasifu wake

WASIFU WAKE

Mheshimiwa Padre Francis Gembe alizaliwa mwezi wa Tano, 1956 katika kijiji cha FUNDOI, MALINDI, LUSHOTO na wazazi wake ni Baba Mpeho Gembe na Mama Maria Kahela.
Alibatizwa tarehe 13/04/1963 Parokiani Lushoto. Na Msimamizi wake alikuwa Mzee Sebastian Theodore.
Komunyo Takatifu trh 16/06/1963
1963 – 1970 Alipata elimu ya Msingi katika shule ya msingi Mhelo – Lushoto.

MAFUNZO YA UPADRE
Padre Gembe Alijiunga na seminari ndogo ya Mt. Petro Morogoro 1971 na kuhitimu elimu ya kidoto cha nne 1974.
1975 -1976 Alijiunga na seminari kuu ya KIBOSHO huko Moshi kwa masomo ya Falsafa.
1977 – 1981 Alipata mafunzo ya Teolojia katika seminari kuu ya Kipalapala Tabora.
09/06/1981 Alipata daraja la ushemasi katika kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua Tanga.
22/11/1981 Alipata Daraja Takatifu la Upadre katika Kanisa Kuu la Jimbo Tanga.

UTUME WAKE
1981 Baada tu ya upadrisho alipangwa kuhudumu katika kanisa kuu la Jimbo la Mt.Anthony wa Padua, Tanga kama Paroko Msaidizi. Baadaye alipangwa kuhudumu katika Parokia ya Lushoto kama Paroko msaidizi.
Baada ya huduma yake katika parokia ya Lushoto alipangwa kuhudumia katika parokia ya Kongoi kama Paroko.
Baada ya utume parokiani Kongoi alitumwa kwenda kuhudumu katika parokia ya Maramba Alipangwa kuhudumia parokia ya Maramba kama paroko.
Baada ya utume katika parokia ya Maramba alitumwa kwenda kuhudumu katika parokia tarajiwa ya Amboni ili aiandae kuwa parokia kwa kujenga miundo mbinu inayohitajika kazi aliyoifanya kwa ufanisi mkubwa.
2016 alihamishiwa katika parokia ya Kanisa Kuu Chumbageni kwa ajili ya uangalizi kutokana na udhaifu wa afya yake.
2022 alihamia nyumba ya malezi ya waseminari na mapadre wazee na wagonjwa ya Neema kule Tanga mpaka umauti ulipompata.

UGONJWA NA UMAUTI
Toka mwaka 2016, Mheshimiwa Padre Gembe alianza kupata udhaifu wa mwili baada ya kupatwa na kiharusi (stroke) iliyopelekea kupoteza uwezo wa kutembea vizuri. Mara kwa mara alikuwa anapelekwa hospital ya KCMC kwa ajili ya kliniki yake na uangalizi. Kwa uvumilivu mkubwa na Imani alipambana na hali hiyo ya maumivu na mateso bila manung’uniko.
Tarehe 2/5/2023 alizidiwa na kupelekwa katika kituo chetu cha Afya Tumaini ambao baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya walimuhamishia katika hospital ya Bombo ambapo aligunduliwa kuwa na tatizo la kufeli kwa figo na Presure yake kuwa juu sana vitu vilivyo pelekea umauti wake alfajiri ya tarehe 5/5/2023.
Raha ya milele umpe ee bwana ………Apumzike kwa Amani……

SHUKRANI:
Jimbo Katoliki la Tanga linamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Padri Gembe, na kwa utume wake mkubwa aliufanya katika Jimbo letu la Tanga. Amebatiza wengi, amefungisha ndoa, amelea wengi kuwa mapadre na watawa na utume mwingine alioufanya. Tunamuomba Mungu amzawadie furaha ya milele kwa hayo aliyotenda.
Kwa namna ya pekee tunawashukuru Padre Silas Singano na Mr. Severine Mkanga ambao walisafiri naye mara nyingi kumpeleka KCMC kwa matibabu. Tunamshukuru paroko wa Kanisa Kuu padre Paul Semng’indo na wasaidizi wake wote kwa kumlea Baba Gembe kwa muda mrefu.
Aidha tunawashukuru Padre Marandu na waseminari wetu pamoja na Bwana Roman Kessy ambao walimsaidia kwa karibu sana baba Gembe pale Neema. Pia tunawashukuru ndugu wa marehemu padre Gembe kwa ushirikiano wao kipindi chote cha ugonjwa wake.
Pia tunawashukuru waganga na wauguzi wa hospitali za KCMC, BOMBO na kituo cha Afya TUMAINI kwa huduma zao kwa padre wetu wakati wa ugonjwa wake.
Mwisho tunawashukuru waumini wote wa Jimbo la Tanga na nje ya jimbo ambao mara nyingi mmekuwa mkimtembelea Baba Gembe na kumfariji katika pale Kanisa Kuu Chumbageni na kwenye nyumba ya malezi Neema na hasa kwa misaada yenu ya hali na mali mliyompelekea. Na kwa kuja kwenu leo kumsindikiza katika safari yake ya mwisho. Mungu awabariki sana.

WALIOTUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MSIMAMIZI WA JIMBO.
Jimbo Katoliki la Tanga limepokea salamu za rambirambi kupitia kwa msimamizi wa Jimbo kutoka kwa: Mapadre: Severine Yagaza, Augustine Temu, Paul Shirima, Richard Kajiru, Richard Kimbwi, Peter Kagaba na Simoni Chakusaga wakiwa nje ya nchi.

catholic diocese of Tanga

© 2024