WASIFU WAKE
Padre Thaddeus Gabriel Ponera alizaliwa 16 Januari 1963, katika kijiji cha Mruazi, kata ya Mnyuzi, Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga. Padre
Thaddeus Gabriel Ponera ni mtoto wa saba(7) kati ya watoto kumi (10) wa familia ya Bwana Gabriel Kazipombe na Mama Lufina Komba.
MAISHA YA SAKRAMENTI:-
Padre Thaddeus Gabriel Ponera Alipata Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Komunyo Takatifu na Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mlingano.
ELIMU:-
Elimu ya Msingi na Sekondari:-
Padre Thaddeus Gabriel Ponera alisoma Shule zifuatazo:-
1968 - 1969:- Shule ya awali (kindergarten) Shule ya Awali Kibaranga,
1970 - 1977:- Darasa la I - VII katika Shule ya Msingi ya Kibaranga,
1978 - 1981:- Kidato cha I- IV katika seminari ndogo ya Soni.(Mt. Joseph Mfanyakazi).
MALEZI NA MAJIUNDO YA UPADRE:-
Padre Thaddeus Gabriel Ponera, Baadaye alijisikia kuitwa kumtumikia Mungu katika Daraja Takatifu ya Upadre. Alisoma na kupata malezi ya majiundo
katika seminari zifuatazo:-
Seminari ya Kibosho/Moshi:-
Mwaka 1982-1984 Padre Thaddeus Gabriel Ponera alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho/ Moshi na kuhitimu masomo ya Falsafa.
Seminari Kuu ya Kipalapala/Tabora:-
Mwaka 1984 - 1989 Padre Thaddeus Gabriel Ponera alijiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala kwa masomo ya Tauhidi/Teolojia.
Mwaka 1987 - 1988 alifanya mwaka wa Kichungaji katika Parokia ya Hale, Tanga. Na Mwaka 1989 alifanya kozi ya Kichungaji kuhusu Nasaha kwa
Wagonjwa (Clinical Pastoral Education), katika Chuo cha Afya Bugando, Mkoani Mwanza.
DARAJA TAKATIFU LA USHEMASI:-
Tarehe 13 Januari, 1989, Padre Thaddeus Gabriel Ponera alipewa Daraja Takatifu la Ushemasi katika Kanisa Kuu la Mt. Antoni wa Padua, Chumbageni
Tanga na Mhashamu Askofu Telesphore Mkude aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.
DARAJA TAKATIFU LA UPADRE:-
Tarehe 19 March, 1990, Padre Thaddeus Gabriel Ponera alipewa Daraja Takatifu la Upadre katika Kanisa Kuu la Mt. Antoni wa Padua, Chumbageni
Tanga na Mhashamu Askofu Telesphore Mkude aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.
SEHEMU ALIZOWAHI KUISHI NA KUFANYA UTUME KATIKA MAISHA YAKE:-
Padre Thaddeus Gabriel Ponera, wakati wa uhai wake, baada ya kupewa daraja la Upadre alitumwa kufanya kazi mbalimbali na kushika nyadhifa mbalimbali
kama Paroko na Msaidizi wa Paroko katika Parokia kama ifuatavyo:-
1990 - 1991:- Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mt. Antoni wa Padua,
1991 - 1994:- Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kilole, Korogwe,
1994 - 1999:- Paroko Msaidizi wa Parokia ya Pangani,
1999 - 2001:- Paroko Msaidizi wa Parokia ya Lushoto,
2001 - 2002:- Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kongoi, Lushoto,
2002 - 2004:- Paroko wa Parokia ya Kwediboma, Handeni,
2004 - 2024: Paroko wa Parokia ya Mazinde Ngua, Korogwe,
2004 - 2011:- Paroko wa Parokia ya Maramba,
2011 - 2011:- Paroko wa Rangwi, Lushoto,
Mei 2011 - Novemba 2014:- Paroko wa Parokia ya Mazinde Ngua, Korogwe,
Novemba 2014 - July 2024:- Paroko wa Parokia ya Tekwa, Lushoto.
UGONJWA, MATIBABU NA MAUTI:-
Siku ya tarehe 02.07.2024, mnamo saa 2 usiku, Padre Paul Semng'indo alipigiwa simu na Sr. Ponera akisema kuwa Padre Thaddeus Gabriel Ponera, yupo
Nyumbani kwa wazazi Tanganyika anaumwa na akilalamika maumivu makali, hivyo wanahitaji gari achukuliwe apelekwe hospitali. Mhe. Padre Paul Semng'indo
alimpa taarifa Mhashamu Baba Askofu Thomas J. Kiangio. Aliruhusu aende haraka na Dereva kwenda kumchukua Padre Thaddeus Gabriel Ponera. Pia Padre Paul
Semng'indo alimjulisha Padre Simon Chakusaga ambaye yupo Parokia ya Muheza, ili afike mapema, alimkuta mgonjwa akiwa katika maumivu, hali ilibadilika
ghafla. Mnamo saa 02:30 Usiku mpendwa wetu Padre Thaddeus Gabriel Ponera, Mwenyezi Mungu alimwita katika makao yake ya milele. Padre Thaddeus Gabriel
Ponera amefariki akiwa na miaka 61 ya kuzaliwa na miaka 34 ya utume kama Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga.
“Raha ya milele umpe ee Bwana, apumzike kwa Amani"
SHUKRANI:-
Mhashamu Baba Askofu, Thomas J. Kiangio, wa Jimbo Katoliki la Tanga, pamoja na Mapadre wa Jimbo Katoliki la Tanga, tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wale wote walioshiriki katika jitihada za kusaidia katika ugonjwa na kuokoa maisha ya mpendwa wetu Padre Thaddeus Gabriel Ponera.
1. Tunamshukuru Mhashamu Baba Askofu Titus Mdoe, Askofu wa Jimbo la Mtwara kwa kujitoa kwake tangu msiba utokee na kuja kutoka Mtwara mpaka Tanga, kushiriki na kuadhimisha Misa Takatifu na maziko ya Padre Thaddeus Gabriel Ponera, hapa Kilole.
2. Tunakushukuru sana Mama Mkuu, Sr. Gaspara Kashimba, wa Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara - Kwamndolwa, pamoja na uongozi mzima, kwa utayari wa kushiriki katika msiba huu na michango yenu ya hali na mali ili kufanikisha shughuli zote za mazishi ya Mpendwa wetu. Asanteni sana.
3. Tunapenda kutoa shukrani kwenu Madaktari, Wauguzi na Wafanyakazi wa Kituo chetu cha Afya Tumaini, Hospitali ya Bombo, kwa kuuhifadhi kwa Moyo wa upendo mwili wa Padre wetu mpendwa.
4. Tunawashukuru viongozi wa Kanisa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo la Tanga, Viongozi mbalimbali wa Parokia ya Tekwa na Jimbo zima na wote mliojitoa kumsindikiza katika safari yake ya mwisho Mpendwa wetu.
5. Shukrani zetu ziwafikie pia ndugu wote wa Marehemu Padre Thaddeus Gabriel Ponera. Kwa namna ya pekee tunamshukuru Sr. Ponera, Bw. Gerard Ponera na wale wote walioguswa na msiba huu.
6. Tunawashukuru sana Padre Simon Chakusaga na Padre Paul Semng'indo, waliojitoa ili kunusuru maisha ya mpendwa wetu.
7. Tunawashukuru Mapadre, Masista, Wakristo na wale wote wenye mapenzi mema kwa Sala na maombezi yenu kwa Padre Thaddeus Gabriel Ponera.
8. Tunawashukuru Wahudumu wa Mortuary katika Hospitali ya Bombo kwa ushirikiano wao. Tunawashukuru wale wote waliojitoa kuandaa mwili wa marehemu.
9. Tunawashukuru Radio Huruma, Radio Maria, St. Anthony online Media, UMTV, Idara ya Habari Jimbo Katoliki la Tanga, kwa matangazo na taarifa za msiba huu.
10. Kwenu Waombolezaji wote mliofika hapa leo hii katika kumsindikiza na kumuaga Mpendwa wetu Padre Thaddeus Gabriel Ponera, nanyi pia mliojitoa kuiandaa nyumba yake anamolazwa Mpendwa wetu, ninyi waandaaji wa mashada na waweka mishumaa nyote mpokee shukurani kwa moyo wenu huo wa kujitoa.
11. Tunatoa shukrani kwa taasisi mbalimbali, viongozi mbalimbali wakiwemo wa Kisiasa na Kidini tukitambua uwepo wenu pamoja nasi, nanyi nyote ndugu, jamaa na marafiki tunatambua uwepo wenu, asanteni sana.
12. Tunawashukuru kamati zote za Maziko kutoka Jimboni na Parokia ya Kilole kwa kuratibu shughuli zote za maziko na msiba huu. Mungu awabarikini.
Imeandaliwa na kusomwa na:-
Padre Benedicto E. Nyangao-Katibu Mkuu-Jimbo Katoliki Tanga.
RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA,
NA MWANGA WA MILELE UMUANGAZIE,
APUMZIKE KWA AMANI. AMINA.
catholic diocese of Tanga © 2024
|